Rayvanny, Konde Boy hii sasa ni sifa

HADI sasa wakongwe wa Bongofleva, Sugu na Lady Jaydee ndio wasanii wa muziki huo waliofanikiwa kutoa albamu nyingi kwa muda wote ikiwa ni zaidi ya miaka 20 tangu wametambulika katika tasnia hiyo.
Sugu aliyetoka kimuziki mwaka 1993 kisha albamu yake ya kwanza, Ni Mimi (1995) ametoa albamu 10, huku Lady Jaydee aliyetoka na albamu yake, Machozi (2000) chini ya MJ Records, ametoa albamu nane hadi sasa.
Ukiachana na hao, staa wa Bongofleva kutokea Next Level Music (NLM), Rayvanny amejitengenezea dunia yake katika eneo hilo ambapo hadi sasa ametoa EP tano na albamu moja akiwa na miaka minane tu tangu ametoka rasmi kisanii.
Albamu moja na EP tano za Rayvvanny aliyetoka kimuziki mwaka 2016 chini ya WCB Wasafi, zina jumla ya nyimbo 63 ambazo zilimfanya kuandika rekodi kama msanii wa kwanza Afrika Mashariki kufikisha ‘streams’ milioni 100 Boomplay Music.
Ni wazi kuwa mfululizo wa kazi hizo ndio umemuwezesha kushinda tuzo kama Tanzania Music Awards (TMA) 2022, Zikomo Awards (Zambia) 2022, Afrimma (Marekani) 2022, EAEA Awards (Kenya) 2022, DIAFA Awards (Dubai) 2022 n.k.
Utakumbuka kabla ya hapo, tayari Rayvanny alikuwa ameshinda tuzo ya BET (Marekani) 2017 kama ‘Viewers Choice Best New International Act’ akiwa ni msanii wa pili Afrika Mashiriki baada ya Eddy Kenzo wa Uganda 2015.
EP yake ya kwanza, Flowers ilitoka Februari 2020 ikiwa na nyimbo nane huku akiwashirikisha Messias, Mr. Blue na Malkia Karen, hii ni EP iliyofanya vizuri hadi kuingia hatua ya kujadiliwa (consideration) kwa ajili kuwania tuzo za Grammy ila haikufanikiwa.
Kufika Februari 2021 Rayvanny aliachia albamu yake yake ya kwanza, Sound From Africa ikiwa na nyimbo 23 na kuwashirikisha wasanii zaidi ya 20, miongoni mwao ni Diamond, Mbosso, Vanessa Mdee, Young Lunya, Innoss’B, Kizz Daniel, Jah Prayzah, Nasty C n.k.
Albamu hii iliyotoka akiwa bado chini ya WCB Wasafi, iliweza kuweka rekodi Afrika Mashariki kwa kufikisha ‘streams’ zaidi ya milioni 100 ndani ya wiki moja pekee tangu itoke, zikiwa ni jumla ya data kutoka majukwaa yote ya kusikiliza muziki.
Mwaka 2022 Sound From Africa ilishinda tuzo kama Albamu Bora Afrika kutoka Zikomo Awards za nchini Zambia, huu ni uthibitisho kuwa albamu hiyo ilikuwa kali na tangu wakati huo hajatoa nyingine zaidi ya kuwapa mashabiki wake EP.

Baadaye akaachia EP yake ya pili, New Chui iliyotoka Oktoba 2021 ikiwa na nyimbo sita na kumshirikisha msanii mmoja tu ambaye ni Abigail Chams aliyesikika katika wimbo, Stay.
Utakumbuka Abigail Chams ni mmoja wa wasanii wa kike wanaokuja kwa kasi Tanzania na Afrika Mashariki, tayari amesainiwa na Sony Music Africa akiwa ni mwanamuziki wa pili wa kike katika historia Tanzania kupata nafasi hiyo baada ya Rose Muhando.
EP ya tatu ya Rayvanny, Flowers II ilitoka Februari 2022 ikiwa na nyimbo tisa na kuwashirikisha wasanii watano ambao ni Roki, Nadia Mukami, Guchi, Ray C na Marioo. Kumbuka EP hii na ile ya mwanzo zote zitoka Februari kwa ajili ya msimu wa wapendanao.
Na baada ya kuachana rasmi na WCB Wasafi hapo Julai 2022, Rayvanny aliachia EP yake ya nne, Unplugged Session iliyotoka Novemba 2022 ikiwa na nyimbo nane, hii ndio EP ya kwanza kutoka ikisimamiwa rasmi na rekodi lebo yake, Next Level Music (NLM).
Haikuishia hapo, Mei 2023 Rayvanny akaachia EP yake ya tano, Flowers III ikiwa na nyimbo tisa na kuwapa shavu wasanii wanne ambao ni Jay Melody, Bahati, Phina na Mac Voice ambaye kamsaini NLM.
Wakati Rayvanny akifululiza kutoa EP, Harmonize a.k.a Konde Boy naye amefululiza kutoa albamu, huyu akiwa bado WCB Wasafi ndipo aliachia EP yake ya kwanza na ya mwisho, Afro Bongo (2019) ikiwa na nyimbo nne alizowashirikisha Burna Boy, Yemi Alade na Mr. Eazi.
Alipoachana na WCB Wasafi aliachia albamu ya yake ya kwanza, Afro East (2020), kisha High School (2021), Made For Us (2022) na Visit Bongo (2023) na alifanya hivyo ndani ya miaka minne mfululizo na albamu hizo zina jumla ya nyimbo 70.
Hii ni tofauti kabisa na aliyekuwa bosi wao, Diamond ambaye ametoa albamu tatu na EP moja, huyu amekuwa akizipa muda kazi zake, albamu yake ya kwanza, Kamwambie ilitoka mwaka 2010, kisha ikafuata, Lala Salama (2012), A Boy From Tandale (2018) na EP, First of All (FOA) (2021).