Penzi la Zari, Shakib lafikia mwisho, waachana
Muktasari:
- Kutokana na taarifa ambayo imeandikwa na wote wawili, imeeleza kuwa baada ya muda mrefu wa kutafakari na kufanya uamuzi kwa kina, wameona ni vyema kila mmoja kuendelea na maisha yake kutokana na tofauti ambazo hawakuweza kuzitatua.
Mwanamuziki na mfanyabiashara maarufu kutoka Uganda, Zarinah Hassan maarufu kama ‘Zari The Boss Lady’ na mumewe wa muda mrefu Shabiki Lutaaya ametangaza kuachana rasmi baada ya kudumu kwa miaka mitano.
Kutokana na taarifa ambayo imeandikwa na wote wawili, imeeleza kuwa baada ya muda mrefu wa kutafakari na kufanya uamuzi kwa kina, wameona ni vyema kila mmoja kuendelea na maisha yake kutokana na tofauti ambazo hawakuweza kuzitatua.
“Baada ya miaka 5, baada ya tafakari na kufikiri kwa kina, tunaamini ni bora kwetu kuachana kutokana na tofauti ambazo haziwezi kupatanishwa. Ingawa haikuwa uamuzi rahisi, tunaona huu ndiyo uamuzi sahihi kwa kila mmoja wetu. Tunathamini muda tuliokuwa pamoja, kumbukumbu tulizounda, na sapoti tuliyopeana,”imeeleza taarifa hiyo.
Wawili hao wameweka wazi kuwa hakuna chuki wala kinyongo kati yao, wakisisitiza kwamba wakati mwingine watu wawili wanaweza kukua na kuelekea katika njia tofauti za maisha.
Zari na Shakib wameeleza kuwa wataendelea kuwa marafiki wenye kuheshimiana na kuelewana, huku kila mmoja akimtakia mwenzake furaha, mafanikio na kila la heri katika maisha mapya.
Zarinah Hassan na Shakib Cham walifunga ndoa ya Kiislamu (Nikah) Aprili 16, 2023 jijini Pretoria, Afrika Kusini, ambapo sherehe hiyo ilifanyika kwa siri na baada ya tetesi kuenea katika mitandao ya kijamii wawili hao waliamua kuthibitisha huku wakiposti picha zao za ndoa.
Ikumbukwe mapema mwaka huu kulizunga tetesi za wawili hao kutengana na kuwa Shakibi aliaamua kubeba virago vyake na kurudi Uganda lakini baada ya muda aliweka wazi kuwa taarifa hiyo ilikuwa ni uvumi tuu kwani wao bado wako pamoja. Hata hivyo mpaka wanaachana wawili hao hawajafanikiwa kupata mtoto.
Kabla ya kuingia katika uhusiano na kufunga ndoa na Shakibi, Zari alikuwa na uhusiano na staa kutoka Tanzania, Diamond Platnumz ambapo katika uhusiano wao walifanikiwa kupata watoto wawili ambao ni Tiffa na Nillan.
Zarinah na Diamond Platnumz walitengana rasmi mwaka 2018, baada ya Zari kutangaza kuachana naye kupitia mitandao ya kijamii siku ya Valentine’s Day (Februari 14, 2018).