Paula amtabiria haya mwanaye ajae

Muktasari:

  • Sio kila jamii itakufikiria au kukuchukulia upande wa mazuri tuu, kuna watakaokuwazia mabaya. Maisha yanaenda.

UMAARUFU sio kazi ndogo. Ili uwe unasikika na kuonwa mara kwa mara kuna ujasiri wake. Mastaa wengi hawajafika walikofika pasipo vizingiti tofauti tofauti.

Sio kila jamii itakufikiria au kukuchukulia upande wa mazuri tuu, kuna watakaokuwazia mabaya. Maisha yanaenda.

Hata hivyo wapo wasanii na watu wengine maarufu ambao umaarufu wao umewapa changamoto nyingi na hawatamani watoto wao wapitie huko. Wanajuta kuwa maarufu.

Paula, mtoto wa mwigizaji maarufu nchini, Kajala Masanja aliyezaa na mtayarishaji mkubwa wa muziki nchini, P Funk Majani, ni juzi tu amefanya sherehe ya kutambulisha ujio wa mwanaye 'Baby Shower' na kuhudhuriwa na mastaa wengi akiwamo baba wa mtoto ajaye, Marioo.

Sherehe ilifana na siku chache baadaye Mwanaspoti lilimtafuta Paula na kuongea naye juu ya mwanaye huyo mtarajiwa na kufunguka mambo mawili.

Kubwa aliloanza nalo kipi hataki kwa mwanaye huyu ambaye anatarajiwa kuwa wa kike.

Paula anasema hatataka mwanae apitie njia alizopita yeye za kuongelewa mitandaoni, kwani ameshaona hasara zake kutoka kwa watu mitandaoni.

"Mimi nazidi kumwomba Mungu nijifungue salama  mtoto wangu wa kike, ila sitataka mtoto wangu awe wa mitandao, kuzungumziwa zungumziwa kama mimi kila wakati iwe kwa mazuri au mabaya, nimejifunza kitu na nimeona sana hasara za kwenye mitandao."

Anasema kama alivyoona mama yake alivyokuwa anafanyiwa mitandaoni kwa kushambuliwa, amepitia huko na sasa kwa mtoto wake, hataki hayo yafanyike.

"Watu wa mitandaoni baadhi yao hapana kabisa, mimi ilifikia hatua hadi nilimwonea mama yangu huruma vile walivyokuwa wakimshambulia kwa maneno, hata kwangu, Nilipoweka wazi mahusiano yangu ya kwanza na haya ya pili. Tulishikama na mama kwa kulia wote na kucheka wote na hadi sasa tulipofikia tunasema asante Mungu," amesema Paula.

La pili analosema kuhusu mwanaye ni angetamani afanane na baba yake (Marioo) kwani anaamini inaleta furaha kwa mtoto kufanana zaidi na baba.

Anasema mtoto kufanana na baba inampa imani baba hajaibiwa, hivyo Mungu ni mwema anamwomba azidi kumpa uhai wa kuishi salama na kujifungua salama.

"Kwa hapa nilipofikia kwenye mahusiano yangu na kumpenda baba mtarajiwa wa mtoto wangu, natamani mwanangu nitakayejifungua afanane na baba yake. Asikwambie mtu ukijifungua mtoto raha afanane na baba yake ili kumpa imani mwanaume hajaibiwa," amesema Paula.

Paula kabla hajaingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanamuziki Marioo, aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki Rayvanny  na kusababisha msanii huyo kuachana na mzazi mwenzake Fahma waliyejaaliwa kupata mtoto moja wa kiume.