Patrick: Ni ngumu kumsahau Kanumba

INAKARIBIA miaka 12 tangu Steven Kanumba ‘The Great Pioneer’ kufariki dunia Aprili 7, 2012, lakini bado anaendelea kuishi kwenye nafasi za wasanii walioibuliwa naye na hata wale waliojitosa kwenye sanaa ya uigizaji kupitia kipaji alichokuwa nacho enzi za uhai wake.

Kanumba aliyetamba kuanzia kwenye uigizaji wa michezo ya kwenye runinga kisha kujitosa kwenye filamu na kujitengenezea jina kubwa, alikumbwa na mauti nyumbani kwake akiwa na aliyekuwa mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na kuitikisa fani ya Bongo Movie aliyokuwa akiibeba mabegani mwake na kuibua wasanii wengi chipukizi.

Miongoni mwa wasanii walioibuliwa na kutengenezewa njia rahisi kwenye fani ya uigizaji ni Othman Njaidi ‘Patrick’ ambaye kwa sasa amekuwa na jina kubwa kwenye fani hiyo akitamba kupitia tamthilia na filamu mbalimbali, anayekiri ni ngumu kwake kulisahau jina la Kanumba hata kama miaka kibao imepita tangu alipoiaga dunia na kuzikwa jijini Dar.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na Patrick anayekimbiza kwa saa kwenye tamthilia ya Toboa Tobo’, ambapo amefungua mambo kadhaa na kuweka bayana kwamba, hata kama kuna wasanii hawapendi kukiri, lakini pengo la Kanumba linaendelea kuitesa Bongo Movie kutokana na namna nyota huyo alivyojituma na kuitangaza nchi kimataifa.


ALINUSA KIPAJI

Patrick anayetumia jina la Aktari kwenye tamthilia hiyo ya Toboa Tobo, anasema licha ya kwamba anatoka katika familia ya wasanii na kupigwa sana tafu na mama yake ambaye naye ni muigizaji mahiri nchini, Hidaya Njaidi, lakini alipaishwa sana na Kanumba kupitia filamu mbalimbali alizoshiriki na kumtambulisha katika Bongo Movie.

Anasema mara baada ya mama yake kubaini naye ana kipaji cha sanaa, aliamua kumpeleka kwa Kanumba na nyota huyo wala hakuremba, akatengeneza kazi ya kwanza iliyomtambulisha ya Unce JJ aliyoichezea akiwa na umri wa miaka minane sambamba na Hanifa Daudi ‘Jenifer’.

Kisha zikafuatia filamu nyingine zilizomjengea jina kama This is It na nyingine kabla ya Kanumba kukumbwa na mauti kisha ikatengenezwa After Death iliyoelezea maisha ya kina Patrick na Jenifer baada ya Anko wao kufariki na ikawa mwanzo wa msanii huyo kupata jina la kujingenezea maisha hadi leo akiwa amecheza filamu kibao.


KIBABE ZAIDI

Patrick anawaambia mashabiki kuwa amerudi kwa kishindo kupitia Toboa Tobo na kuwataka wategemee kumuona sana katika kazi mbalimbali na nzuri kwa kuwa anafanyakazi na watu wenye misingi mizuri katika sanaa.

Kuhusu alipokuwa kwa kipindi chote mpaka sasa anaonekana kuwa barubaru kwa sasa, anasema mbali ya masomo, lakini alikuwa akijaribu kujifunza namna ya kuzalisha kazi za filamu hivyo akawa zaidi nyuma ya kamera.

“Hadi sasa tayari nina kazi ambazo nimeshiriki kuziandaa, ila bado tu hazijatoka, lakini naomba mashabiki wangu zitakapoingia mtaani basi wasiache kunisapoti. Kwa kuwa ndoto yangu sio tu katika kuigiza kila siku, na ndio maaana nimeanza kujifunza kidogokidogo kutengeneza filamu,” anasema Patrick mwenye umri wa miaka 22 kwa sasa.


SIO KUIGIZA TU

Patrick anasema mbali na koneksheni ya mama yake kwa Kanumba, lakini hata yeye alikuwa akipenda kuigiza na alionyesha dalili za kipaji hicho tangu akiwa na miaka mitatu.

“Mimi napenda sanaa ikiwemo kuimba, kusikiliza muziki na nilikuwa napenda kuigiza tangu nikiwa na miaka mitatu wakati bado sina ufahamu vizuri,” anasema.

Anasema yeye anapenda kuimba hadi leo na anafuatilia sana sanaa za nje ili kuzidi kujifunza mambo mapya ya kuboresha kipaji alichonacho akiamini pia kitamsaidia kwenye fani mpya ya utayarishaji na uongozaji anayoanza kupambana nayo mdogo mdogo.


DEFAO, WACKO JACKO

Patrick anasema kwa kuwa kipindi hicho filamu za Bongo zilikuwa hazijachanganya kihivyo, alikuwa akiwatazama zaidi wasanii wa nje wakiwemo Arnold Schwarzenegger wa Marekani, Shah Rukh Khan wa India, Jet Li na Jackie Chan aliovutiwa nao enzi hizo akienda kuangalia muvi zao kupitia mabanda ya uswahilini.

Na hata sasa bado anapenda sana kufuatilia muvi za nje katika kupata ujuzi, lakini ni mgonjwa wa muziki na alianza kuvutiwa zaidi tangu zamani na Defao kutoka DR Congo, ambaye sasa ni marehemu, Michael Jackson ‘Wacko Jacko’ na kwa hapa nchini alimzimia mno Sir Juma Nature ‘Kiroboto’.

Kwa upande wa uigizaji, alivutiwa na kundi la Kaole Sanaa, lililowaibua wakali mbalimbali nchini akiwamo Kanumba, Ray Kigosi, Johari na wengineo.


KANUMBA ANAISHI

Patrick anafichua kwamba, wakati anaigiza filamu ya ‘This Is It’ na ‘Uncle JJ’, hakumbuki kwa mara kwanza ilikuwaje, lakini baadaye alipokuwa mkubwa na kuona namna ile filamu inavyopendwa, alijiona ni mtu mwenye bahati kwani kwa kipindi kile kufanya kazi na Kanumba ilikuwa ni ndoto ya kila mtu, hivyo alikuwa ni mmoja wa watu aliokuwa wakiishi kwenye ndoto za watu.

“Yaani kila nikiangalia filamu zile na Uncle Kanumba, naona Mungu alikuwa mwema na anaendelea kuwa mwema kwangu,” anasema Patrick.

Kuhusu kitu ambacho amekimisi kutoka kwa Kanumba tangu alipofariki, Patrick anasema kubwa uwepo wake kwani mbali na kazi pia nje walikuwa na uhusiano mzuri kama mtu na mdogo wake, mtu na mtoto wake au mtoto na mjomba, huku akikiri pengo la mkali huyo litachukua muda kuzibwa kwani alikuwa ni msanii wa kipekee aliyejitoa.

SANAA YA SASA    

Akizungumzia tofauti ya uigizaji wa sasa na wa zamani, Patrick anasema umebadilika kwa kiasi kikubwa na kama wewe ni msanii unayependa kazi yako pia lazima ubadilike nayo.

Pamoja na mabadiliko hayo yakiwemo ya kiteknolojia, msanii huyu anasema moja ya changamoto kubwa anayoiona ni kwamba watu hawazalishi filamu nyingi na hivyo kutokuwa na uwanda mpana wa kwenda kushindana nje ya nchi ukizingatia ni lazima tasnia ya filamu nayo ikue.

“Tunashukuru kwa namna TV za hapa nyumbani zimekuwa zikisapoti kwa kupokea kazi zetu, lakini lazima pia tutazame na soko la nje, tusijifungie tu ndani kwa kuwa huko nako kuna fursa nyingi za kupeleka tasnia yetu mbele zaidi.”

Kuhusu anapojiona miaka mitatu ijayo, Patrick anasema anajiona mbali ikichagizwa na kufanya kazi zilizo bora.


YEYE NA JENIFER

Wakati watu walikuwa wakisema yeye na Jenifer Kanumba ni wapenzi, Patrick amelikanusha hilo akieleza inachangiwa zaidi na ukaribu walionao tangu walipoanza kuigiza wakiwa wadogo.

“Siku zote uhusiano wa karibu sana kati ya mwanamke na mwanaume, lolote linaweza kusemwa nasi tulilitegemea hilo na huwezi kuwazuia watu wasiseme, lakini ukweli hakuna chochote kinachoendelea baina yetu, hatuna uhusiano wa kimapenzi kati yetu,” anasema msanii huyo, japo mama yake mzazi aliwahi kukaririwa anatamani Jenifer aolewe na kijana wake huyo.

KAZI ALIZOSHIRIKI

Ukiondoa filamu za Uncle JJ na This is It alizoingiza na Kanumba, nyota huyo pia amecheza filamu mbalimbali kabla ya kuibukia kwenye tamthilia akitamba na Pazia kisha Sultana akitumia jina la Jabal Junior kabla ya sasa Toboa Tobo iliyoanza hivi karibuni kuzidi kumpa ujiko akishirikiana na wakali kadhaa akiwamo Muhogo Mchungu na wengineo.