Nyimbo za Bongo Fleva zilizotazamwa zaidi YouTube 2025
Muktasari:
- Kwa kulizingatia hilo, tunakuletea orodha ya nyimbo 10 za Bongo Fleva ambazo video zake zimetoka mwaka huu na kutazamwa sana YouTube, mtandao unaotumiwa na mashabiki wengi zaidi nchini.
TANGU mwaka 2025 ulipoanza hadi sasa anapokaribia kutia nanga, wasanii wa Bongo Fleva wametoa nyimbo nyingi zilizopokelewa vizuri na mashabiki wao na hata kupata namba za juu mtandaoni hasa YouTube.
Kwa kulizingatia hilo, tunakuletea orodha ya nyimbo 10 za Bongo Fleva ambazo video zake zimetoka mwaka huu na kutazamwa sana YouTube, mtandao unaotumiwa na mashabiki wengi zaidi nchini.
1. Pawa (Mbosso) - Imetazamwa mara milioni 51
Ni wimbo kutoka katika EP ya pili yake Mbosso, Room Number 3 (2025), video yake iliachiwa Juni 19 ikiwa imeongozwa na Director Folex, mshindi wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023.
Hadi sasa video ya 'Pawa', wimbo uliotayarishwa na S2kizzy, imetazamwa zaidi ya mara milioni 51 YouTube, ikiwa ndio video ya Bongo Fleva iliyofanya vizuri zaidi 2025, pia iliyotazamwa zaidi ndani ya muda mfupi.
2. Nairobi (Marioo) - Imetazamwa mara milioni 44
Wimbo huu uliotayarishwa na Kaniba ndio uliofanya vizuri zaidi katika albamu yake ya pili, The God Son (2024) chini ya Bad Nation Label, na video yake iliyosimamiwa na Director Kenny ikiachiwa Januari 6.
'Nairobi', wimbo ambao Marioo kamshirikisha Bien kutokea Kenya, tayari video yake imetazamwa mara milioni 44 YouTube, ikiwa ni video yake ya kwanza kupata namba kubwa hivyo kwa mwaka mmoja.
3. Tete (Marioo) - Imetazamwa mara milioni 36
Iliachiwa rasmi Aprili 16 ikiwa imeongozwa na Director Kenny huku S2kizzy akihusika upande wa audio. Hadi sasa imetazamwa mara milioni 36, ikiwa ndiyo video pekee aliyofanya na Paula kupata namba kubwa zaidi.
Ikumbukwe kabla ya Tete, Paula alishatokea katika video za nyimbo za Marioo kama Lonely (2023), Tomorrow (2023), Sing (2023), Hakuna Matata (2024), Unachekesha (2024) na My Daughter (2024).
4. Furaha (Harmonize) - Imetazamwa mara milioni 31
Ni wimbo uliotayarishwa na Kimambo, huku video yake iliyotoka Februari 14 chini ya Verse Network hadi sasa ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 31 YouTube, mtandao unaomilikiwa na kampuni ya Google.
Katika video hii Harmonize ameigiza pamoja na kucheza na mwanamuziki mwenzake, Abigail Chams ambaye wameshirikiana katika nyimbo kama Closer (2022), Leave Me Alone (2022), Me Too (2025) na Lala (2025).
5. Me Too (Abigail Chams) - Imetazamwa mara milioni 28
Mshindi wa tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2021, Director Kenny ndiye ameongoza video hii iliyotoka Februari 28, na Abigail Chams ameshirikiana na Harmonize kutokea Konde Music.
Tayari video ya 'Me Too', wimbo uliotayarishwa na B Boy Beats, imetazamwa mara milioni 28, na mradi huu ulichangia Abigail kuchaguliwa BET 2025 akiwa ni msanii wa kwanza kike Afrika Mashariki kuwania tuzo hizo.
6. Salama (Barnaba) - Imetazamwa mara milioni 26
Huu ni wimbo wa pili kwa Barnaba kumshirikisha Diamond Platnumz baada ya hapo awali kutoa 'Hadithi' uliojumuishwa katika albamu yake ya tatu, Love Sounds Different (2022) iliyoshinda tuzo ya TMA 2022.
Wimbo 'Salama' umetayarishwa na S2kizzy, video yake iliyotoka Mei 31 imeongozwa na Director Folex, na hadi sasa imetazamwa zaidi ya mara milioni 26, na ikiwa ndio namba moja YouTube kwake.
7. Looking For Love (Darassa) - Imetazamwa mara milioni 15
Tunaweza kusema wimbo huu uliotayarishwa na Kaniba, ndio uliopokelewa vizuri zaidi kutokea katika albamu yake ya pili, Take Away The Pain (2025) chini ya lebo yake, Classic Music Group (CMG).
Video yake ilitoka Februari 14 chini ya Mjukuu Visuals na tayari imetazamwa zaidi ya mara milioni 15 huko YouTube, ikiwa ni video yake ya nne kufanya vizuri katika mtandao huo kwa muda wote.
8. Jirani (Jay Melody) - Imetazamwa mara milioni 14
Ni wimbo unaopatikana katika albamu yake ya pili, Addiction (2025) yenye nyimbo 12 na kushirikisha wasanii watatu (Alikiba, Jux & Mwana FA). Ulitengenezwa na Chibby huku video yake ikiachiwa Mei 28.
Director Hanscana ndiye ameongoza video hiyo ambayo tayari imetazamwa zaidi ya mara milioni 14, ikipanda hadi nafasi ya nane katika orodha ya video zake zilizofanyika vizuri kwa muda wote YouTube.
9. Amanda (Zuchu) - Imetazamwa mara milioni 14
S2kizzy ndiye ametayarishwa wimbo huu ambao ulikuja baada ya Zuchu kuwa kimya kwa zaidi ya miezi sita akiipa nafasi ya kufanya vizuri albamu yake ya kwanza, Peace and Money (2024) yenye nyimbo 13.
Video yake iliachiwa Agosti 1 ikiwa imeongozwa na Director Ivan na hadi wakati hii imeshatazamwa zaidi ya mara milioni 14 huko YouTube, huku remix yake ambayo Zuchu kamshirikisha Spice ikifikia milioni 2.2.
10. Katam (Diamond Platnumz) - Imetazamwa mara milioni 13
Ilitoka rasmi Julai 6, na mikono ya Director Folex ndio imehusika katika video hii ambayo imeshatazamwa YouTube mara milioni 13, ikiwa ndiyo video ya Diamond iliyofanya vizuri zaidi 2025 kati ya tano alizoachia.
Wimbo huo umetayarishwa na S2kizzy kutokea studio za Pluto Republic, huku Diamond akimshirikisha Bien, mwanachama wa kundi la Sauti Sol kutokea Kenya ambao ni washindi wa tuzo ya MTV EMAs 2014.