Ni zamu ya Jaydee, asimulia alivyoanza

Muktasari:
- Jide ametoa historia hiyo alipokuwa akitambulishwa kufanya shoo katika tamasha la Bongo Fleva Honors linalofanyika nchini chini ya Deiwaka World inayoongozwa na mkongwe mwingine wa muziki, Joseph Mbilinyi (Sugu).
MKONGWE wa muziki wa kizazi kipya nchini, Judith Wambura maarufu Lady Jay Dee au Jide amesimulia alivyoimba kwa mara ya kwanza wakati akitafuta kutoka kimuziki.
Jide ametoa historia hiyo alipokuwa akitambulishwa kufanya shoo katika tamasha la Bongo Fleva Honors linalofanyika nchini chini ya Deiwaka World inayoongozwa na mkongwe mwingine wa muziki, Joseph Mbilinyi (Sugu).
Jide atakonga nyoyo za mashabiki wa Bongo Flava, Oktoba 25, kwenye ukumbi wa WareHouse Masaki, Dar es Salaam akiwa mwanamuziki wa kwanza mkongwe wa kike kufanya shoo kwenye tamasha hilo.

Tamasha hilo limemkumbusha Jide historia yake ya muziki, akieleza alivyoimba kwa mara ya kwanza akimtaja Dj Bon Luv ni mtu wa kwanza kumpa maiki ili aimbe.
“Hakuna kitu nakifurahia kama siku nitakayopafomu Bongo Flava Honors, akiwepo pia Dj Bon Luv, ambaye ni mtu aliyenipa maiki kwa mara ya kwanza niimbe,” alisema Jide.
Akieleza historia hiyo, Jide alisema wakati huo alikuwa akirap, Dj Bon Luv ndiye alimpa maiki kwa mara ya kwanza aimbe na baada ya miaka kadhaa Oktoba 25 atakuwa naye kwenye shoo ya Bongo Flava Honors.
“Nakwenda kufanya shoo ya kihistoria, nafasi niliyopewa ya kuwa mwanamuziki wa kwanza mwanamke kufanya shoo kwenye tamasha ili la wakongwe wa muziki nchini nitaitendea haki, mashabiki watafurahi,” alisema Jide.
Mwanamuziki huyo ambaye amekuja na staili ya tofauti akiwa na kapu la Jide amesema, siku hiyo kutokana na ukubwa wa shoo atakayoifanya, wale watakaofurahi hawapaswi kumtuza kwa kumpa pesa mkononi.
“Wataweka kwenye kapu hili, naamini kwa namna nitakavyopafomu, watalijaza siku hiyo,” alisema Jide akionyesha kapu hilo.
Akizungumzia tamasha hilo, mratibu wake, Joseph Mbilinyi (Sugu) alisema baada ya mwanamuziki AY kufanya shoo mwezi Aprili, kisha kundi la Daz Nundaz mwezi Julai, sasa heshima ya wakongwe wa muziki inakwenda kwa Jide aliyemtambulisha ni dada wa Bongo Flava aliyeitendea haki na ameendelea kutamba hadi sasa.
“Hakuna asiyemfahamu Jide au binti Komando kwenye gemu, huyu ni dada wa gemu, Oktoba 25 utakuwa ni usiku wa Jide kwenye Bongo Flava Honors,” alisema Sugu.
Mbali na kufanya shoo, siku hiyo pia kutakuwa na makala maalumu inayoelezea safari ya muziki ya Jide kuanzia anatoa wimbo wake wa kwanza hadi sasa.
Dj Bon Luv alisema makala hiyo maalumu itaonyeshwa kwenye shoo hiyo itakayofanyika laivu ukumbini hapo.
Akizungumzia namna wanavyochagua wanamuziki wa kuimba, Sugu alisema kigezo cha kwanza ni kuwa amefanya muziki kati ya 2005 kushuka chini.
Kwa mujibu wa Sugu, ukiachana na tamasha la kila baada ya miezi mitatu, Deiwaka World inajipanga kufanya tamasha jingine moja ambalo litahusisha wanamuziki wote waliopafomu kwenye Bongo Flava Honors kwa mwaka husika ambalo watalipa jina la All Stars.