Ni mwaka mwingine kwa Abigail Chams kukita ngoma!

NI mwaka mwingine ambao mwimbaji  wa Bongofleva, Abigail Chams anatarajiwa kuonyesha zaidi kipaji chake, uimbaji wake, utunzi na uwezo wa kupiga vyombo mbalimbali vya muziki vimeitengenezea chapa yake taswira ya kipekee.

Huyu alianza kujifunza kupiga piano akiwa na umri wa miaka mitano, alipofikisha miaka minane akawa amejua na violini, gitaa, ngoma na filimbi, alianza muziki kwa kuweka kazi zake kwenye mitandao yake ya kijamii na polepole Bongofleva ikampokea.

Utakumbuka mwaka uliopita, Abigail alifanikiwa kusainiwa na Menejimenti ya RockStar Africa na baadaye lebo kubwa duniani, Sony Music Entertainment Africa ikasaini mkataba wa kufanya naye kazi.

Abigail ameufungua mwaka 2023 kwa kuachia wimbo wake mpya 'Nani?' ambao amemshirikisha Marioo, Staa wa Bongofleva aliyeshinda tuzo tatu za muziki Tanzania (TMA) mwaka uliopita.

Hii ni kazi yake ya tatu kutoa rasmi tangu kusainiwa Sony Music, alianza na ngoma 'U & I' kisha ikafuata 'Closer' akimshirikisha Staa wa Konde Music, Harmonize na ngoma zote zimepata mapokezi mazuri ndani na nje.

Miongoni mwa kazi zake za awali zilizoanza kumpa mashabiki kwenye majukwa mbalimbali mtandaoni ni pamoja na Never Enough, I Thought, I'M Yours, Zero to 100, Real One, Reimagine n.k.

Mkongwe wa Bongofleva, TID a.k.a Mzee Kigogo katika hafla ya uzinduzi wa albmu ya Ommy Dimpoz 'Dedication' hapo Novemba 2022 alisema Abigail Chams ni msanii mkali anayevutiwa na uimbaji wake.
Hadi sasa Abigail ameshirikishwa na wasanii wa Bongofleva kama Rosa Ree (Mulla), Rayvanny (Stay), Mimi Mars (Haina Maana), Harmonize (Leave Me Alone), Darassa (King of the Kings) n.k.

Katika tuzo za TMA 2021 Abigail alitajwa kuwania kipengele cha Msanii Bora wa Kike wa Mwaka Chupukizi akiwa na wenzake, Phina, Marry G, Lolo Da Prince na Trixy Tonic.
"Na sasa hivi natazama tuzo za Grammy, nawaza kuzipata kwa miaka miwili ijayo, kwa sababu ziko hapo kwenye malengo na ninaamini nitazipata lakini naamini hata BET nitazipata" Abigail aliliambia gazeti hili.

Ikumbukwe baada ya Abigail kuachia wimbo wake 'Reimagine' alipata nafasi ya kufanya kazi na Shirika la Umoja wa Mataifa Linalohudumia Watoto (UNICEF) Tanzania kama Balozi, pamoja na kutumbuiza kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai.

Akizungumza na Mwanaspoti, Seven Mosha ambaye ni Msimamizi wa Masoko na Maendeleo ya Wasanii Afrika Mashariki chini ya Sony Music Entertainment Africa, amesema kama hujakutana na Abigail huwezi kujua ni kipaji cha aina gani anacho.

"Unaweza kumjua kwa juu juu kwa hizi nyimbo ambazo ameimba au kuangalia mitandao yake ya kijamii, imenichukua muda sana kukutana na msanii mwenye uchu wa kufanya muziki kama Abigail Chams," amesema.

"Ni watu wachache sana katika tasnia wanaweza kusikiliza muziki kwa sikio lake na kubadilisha vitu, anaweza kukuambia kabisa hapana, naomba nibadilishie hii bila kujua vitu vyote vya muziki kama prodyuza," anasema Seven.
Seven anasema Abigail ni mtu ambaye amejifundisha vitu vingi binafsi, hicho ni kipaji kingine, anaimba vizuri kwa Kiingereza na Kifarasa, sio kwamba alienda Ufaransa bali alijifunza pekee yake, na hata jinsi anakitamka, lafudhi yake inavutia sana.

"Ni mtunzi mzuri sana kwa Kiingereza na Kifaransa lakini vile vile anaweza kwa Kiswahili, anajua kucheza piano, vionia na drums, kwa umri wake na amejifunza pekee yake, sio mtu wa kawaida, ni mtu kweli ana kipaji cha ziada," aanasema Seven.

Desemba 15, 2020 ndipo Seven aliteuliwa kushika nafasi hiyo akiwa na uzoefu wa kuwasimamia wasanii kwa zaidi ya miaka 18, amewahi kufanya kazi na wasanii Bongo kama TID, Rose Muhando, Lady Jaydee, Alikiba n.k, na sasa kupitia Sony Music yupo na Abigail Chams, Aslay, Ommy Dimpoz na Young Lunya.

Ikumbukwe Seven umehusika kwenye miradi mbalimbali mikubwa inayohusisha wasanii nchini, mathalani kampeni ya Staying Alive mwaka 2008 iliyolenga kutoa elimu kwa vijana kuhusu Ukimwi ambayo balozi wake alikuwa Kelly Rowland. Na alikuwa sehemu ya mapokezi ya Jay Z nchini mwaka 2006 katika kampeni yake, Jay Z Water for Life Tour akishirikiana na Umoja wa Mataifa (UN).