Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ngoma 10 kubwa Afrika, Diamond wa mwisho!

Muktasari:

  • Katika orodha hiyo wasanii wa Nigeria na Afrika Kusini ndio waliotawala kwa kiasi kikubwa, huku Diamond Platnumz kutoka Tanzania akiwa msanii pekee Afrika Mashariki aliyefanikiwa kuchomoza - tena katika nafasi ya mwisho. 

TUNAKELETEA mkusanyiko wa nyimbo 10 za wasanii kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zimepata namba kubwa katika mtandao wa YouTube ambao unatumiwa na mashabiki wengi hapa nchini kwa kutazama kazi za wasanii wanaowapenda.

Katika orodha hiyo wasanii wa Nigeria na Afrika Kusini ndio waliotawala kwa kiasi kikubwa, huku Diamond Platnumz kutoka Tanzania akiwa msanii pekee Afrika Mashariki aliyefanikiwa kuchomoza - tena katika nafasi ya mwisho. 


1. Calm Down - Rema & Selena Gomez

Mwimbaji wa Nigeria, Rema alitoa toleo (version) lingine la wimbo wake, Calm Down (2022) na kumshirikisha Selena Gomez. Uamuzi huo umekuwa na matunda mengi maana wimbo umefanya vizuri duniani hadi kuteuliwa kuwania Grammy.

Huu wimbo umeandika rekodi kama wa kwanza barani Afrika kusikilizwa (streams) zaidi ya mara bilioni moja katika mtandao wa Spotify na umeshinda tuzo ya MTV Video Music Awards Marekani.

Sasa video yake iliyotoka Septemba 7, 2022 ina ‘views’ zaidi ya milioni 999, huku lile toleo la awali likiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 619. Ndio wimbo pekee Afrika uliotazamwa zaidi YouTube Afrika kwa kipindi kifupi.


2. Jerusalema - Master KG & Nomcebo

Wimbo huu ulitoka Novemba 29, 2019 na kupata mapokezi makubwa Afrika Kusini. Video yake ilifuata Desemba 12, 2019 na sasa ndio video iliyotazamwa zaidi YouTube nchini humo ikiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 628.

Wimbo huu una remix mbili, ya kwanza ilitoka Juni 2020 akimshirikisha Burna Boy wa Nigeria, ilifanya vizuri na kuingia chati za  Billboard Marekani. Remix ya pili ilitoka Septemba 2020 na kuwashirikisha Venezuela Micro TDH na Greeicy kutokea Colombia.

Master KG ambaye ni mwanzishili wa dansi maarufu ‘Bolobedu’, kupitia albamu yake, Skeleton Move aliweza kushinda tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) katika kipengele cha Best Artist/Group in the African Electro.


3. Love Nwantiti - Ckay

Msanii wa Nigeria, Ckay hapo Agosti 30, 2019 aliachia EP yake iitwayo ‘Ckay’ yenye nyimbo nane chini ya Chocolate City na Warner Music Group.  Ndani yake ndipo kuna ngoma, Love Nwantiti iliyochiwa Agosti 29, 2019.

Video ya ngoma Love Nwantiti ilitoka Februari 14, 2020 na tayari ina ‘views’ zaidi milioni 518 huku katika remix akiwashirikisha Joeboy na Kuami Eugene.

Wimbo huu umechangia sehemu kubwa ya mafanikio ya EP hiyo ambayo aliweza kuingia kwenye chati za Billboard nchini Marekani, Canada na Uholanzi. Pia iliingia kwenye chati za Ufaransa (SNEP).


4. Magic in the Air - Magic System & Chawki 

Kundi la Magic System lilianzishwa mwaka 1996 huko Abidjan nchini Ivory Coast, wasanii wake ni  Salif “Asalfo” Traore, Narcisse “Goude” Sadoua, Étienne “Tino” Boué Bi na Adama “Manadja” Fanny.

Mwaka 2014 waliachia wimbo wao, Magic in the Air wakimshirikisha Chawki kutokea Morocco, ni miongoni mwa nyimbo zilizotoka kwa ajili ya kusherehesha fainali za Konde la Dunia zilizofanyika Brazil  2014.

Video yake ilitoka Machi 17, 2014 na hadi sasa ina ‘views’ zaidi ya milioni 481 YouTube na kuzidi kuliweka kundi katika ramani baada ya kufanya vizuri Afrika Magharibi na mtindo wa dansi ya Zouglou.


5. On The Low - Burna Boy

Ngoma yake, On The Low ambayo ni mchanganyiko wa Afrobeat na Dancehall imempatia mafanikio makubwa mwimbaji huyo kutokea Nigeria ambaye alivuma zaidi mwaka 2012 baada ya kuachia ngoma, Like to Party kutoka kwenye albamu yake, L.I.F.E (2013).

Video ya wimbo huo uliyotayarishwa na Kel P ilitoka Novemba 16, 2018 ikiongozwa na Meji Alabi, tayari imefikisha ‘views’ zaidi ya milioni 405, vilevile video ya wimbo wake, Last Last iliyotoka Mei 13, 2022 tayari ina ‘views’ zaidi ya milioni 298. 

Ikumbukwe Burna Boy ambaye mwaka 2017alisaini na Bad Habit/Atlantic Records ya Marekani na Warner Music Group, ameshinda tuzo nne za BET na moja ya Grammy kupitia albamu yake ya tano, Twice As Tall.


6. Rush - Ayra Starr

Ndio video ya kwanza ya msanii wa kike solo kufikisha ‘views’ zaidi ya milioni 300 YouTube nchini Nigeria na sasa ikiwa na milioni 398, ilitoka rasmi Septemba 26, 2022 chini ya Mavin Records ambayo inamsimamia Rema pia.

Wimbo huu kutoka katika albamu yake, 19 & Dangerous (2021) ulianza kuvuma TikTok na baadaye kila sehemu, ulimpa Ayra Starr nafasi ya kuwania tuzo za Grammy 2024 akichuana na Asake, Burna Boy, Davido na Tyla aliyeibuka mshindi.

Ukiachana na Ayra Starr na Rema, Mavin Records inayosimamiwa na Don Jazzy, tayari imewatoa wasanii wakubwa Nigeria kama Tiwa Savage, Wande Coal, Reekado Banks, Iyanya na kadhalika.


7. Fall - Davido

Mwimbaji huyo wa Nigeria alianza muziki katika kundi la KB International, Davido alipata umaarufu mwaka 2011 alipoachia ngoma yake, Dami Duro ambayo ni ya pili kutoka kwa albamu yake ya kwanza, Omo Baba Olowo.

Mwaka 2017 baada ya kurekebisha mkataba wake na Sony Music, Davido alitoa nyimbo tano ukiwemo ‘Fall’ ambao ulifanya vizuri hadi chati za Billboard, video yake iliyotoka Juni 2, 2017 imefikisha ‘views’ milioni 294.

Kupitia X (Twitter) mwaka 2016 Davido alitangaza kusaini mkataba na Sony Music, miezi michache baadaye alianzisha lebo yake, Davido Music Worldwide (DMW) na kuwasaini Dremo na Mayorkun.


8. Joro - Wizkid

Ni mwimbaji kutokea Nigeria, ameshinda tuzo zote kubwa Afrika, pia ameshinda BET na Grammy kupitia wimbo, Brown Skin Girl aliyopewa shavu na Beyonce katika albamu yake, The Lion King: The Gift.

Hapo Septemba 30, 2019 aliachia video ya wimbo wake, Joro na hadi sasa ina ‘views’ milioni 265, ikifuatiwa na video ya wimbo wake ‘Essence’ akimshirikisha Tems ambayo ina ‘views’ zaidi ya milioni 202 tangu itoke rasmi hapo Aprili 9, 2021.

Wizkid alipata umaarufu baada ya kuachia wimbo wake ‘Holla at Your Boy’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Superstar (2011) iliyotoka miaka miwili baada ya kusainiwa na Banky W’s Empire Mates Entertainment (E.M.E).


9. Baby On Fire - Die Antwoord 

Die Antwoord ni kundi la muziki wa Hip Hop Afrika Kusini lililoanzishwa mjini Cape Town mwaka 2008 na Marapa wawili, Ninja na Yolandi Visse, mwaka 2009 walitoa albamu yao ya kwanza, $O$ bila malipo mtandaoni na kuwatangaza vilivyo.

Kufika Juni 2, 2012 waliachia video ya wimbo wao ‘Baby On Fire’ ikiongozwa na Ninja na Terence Neale, hadi sasa huko YouTube imefikisha ‘views’ zaidi ya milioni 277.

Mwaka 2011 Die Antwoord walianzisha lebo yao wenyewe, Zef Recordz na kufuatia mfululizo wa albamu zao kali kama Ten$Ion (2012), Donker Mag (“Dark Power”; 2014) na Mount Ninji and da Nice Time Kid (2016).


10. Yope Remix - Innoss’B & Diamond Platnumz

Hadi sasa Staa wa Bongofleva kutoka WCB Wasafi, Diamond Platnumz ameshiriki katika video nane zilizofikisha ‘views’ zaidi ya milioni 100 YouTube, video hizo ni Yope Remix, Inama, Waah!, Time To Party, Kwangwaru, Jeje, Nana na Enjoy.

Video ya Yope Remix ambayo Diamond kashirikiana na Innoss’B kutokea DR Congo ilitoka Septemba 7, 2019 na hadi sasa ina ‘views’ zaidi milioni 238 YouTube na ndio video inayoongoza Afrika Mashariki.

Ikumbukwe Diamond ambaye ametoa albamu tatu, EP moja, huku akishinda tuzo zaidi 40, ndiye msanii pekee Tanzania na Afrika Mashariki ambaye video zake zote zimefanikisha kufikisha jumla ya ‘views’ zaidi ya bilioni 2.7 YouTube.