Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nedy Music na rekodi katika muziki Zanzibar

PETER AKARO


MWIMBAJI wa Bongofleva, Said Seif Ally ‘Nedy Music’ ni miongoni mwa wanamuziki wachache kutokea visiwani Zanzibar ambao wamekuwa na mwendelezo mzuri kisanaa katika kipindi cha takribani miaka minane iliyopita na kuandika rekodi yake.

Nedy Music amejipachika a.k.a ya ‘Mpemba Mmoja’ ili kujivunia na kuwakilisha kule anapotokea kama ilivyo kwa G Nako (The Finest of AR), Fid Q (Ngosha The Swagger Don), Joh Makini (Mwamba wa Kaskazini), Mike Tee (Mnyalu), Mimi Mars (Chuga Queen) n.k.

Wakati tunaadhimisha miaka mitatu ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi madarakani kwa kutazama yale mazuri aliyotekeleza kwa kipindi chake, upande wa burudani tunamuangazia Nedy Music anayewakilisha vizuri visiwa hivyo vya marashi ya karafuu.

Nedy Music, 28, alianza taaluma yake kama dansa ambapo pamoja na kundi lake waliibuka washindi wa shindano la Dance La Fiesta 2010 chini ya Clouds Media, baadaye alishiriki mashindano ya Dance Mia Mia 2012 chini ya EATV lakini hawakufanya vizuri.

2013 baada ya kuhitimu sekondari, Nedy Music alijiunga na Tanzania House of Talent (THT) ili kujifunza zaidi muziki kwa muda mfupi kama ilivyokuwa kwa Ben Pol, Lava Lava na Marioo kwa sababu hawa nao hakutoka kimuziki chini ya chapa hiyo.

Utakumbuka THT imezalisha majina makubwa na maarufu kwenye Bongofleva kama Mwasiti, Barnaba, Linah, Amin, Ruby, Ditto, Ibrah Nation, Recho Kizunguzungu, Jolie, Ally Nipishe, Nandy, Jay Melody n.k. 

Miaka mitatu baadaye Nedy alisainiwa na Poz kwa Poz (PKP) Entertainment, Rekodi Lebo yake Ommy Dimpoz na kuachia wimbo wake, Usiende Mbali (2016) ambao alimshirikisha pia Dimpoz ambaye wakati huo alikuwa katika kilele cha mafanikio ya kazi yake. 

Wimbo huo ulifanya vizuri ndani na kimataifa kwa kukamata chati za vituo vikubwa vya televisheni kama MTVbase, Sound City, Trace Urban n.k, na hadi sasa ndio wimbo pekee wa Nedy uliotazamwa zaidi katika mtandao wa YouTube ukiwa na ‘views’ zaidi ya 1.7 milioni.

Ni wimbo uliopata mapokezi makubwa ndani ya muda mfupi, ilichukua siku 13 tu kwa video yake kufikisha ‘views’ 1 milioni YouTube, 2016 kupata namba hizo zilikuwa ni mafanikio kutokana watumiaji wa mtandao huo hawakuwa wengi kama sasa.

Kwa sasa Nedy Music ameikuza chapa yake kwa kuachia ngoma nyingine kali kama Rudi ft. Christian Bella, Nishalewa ft. Mr. Blue, Dozee, Zungusha, Kinomanoma ft. Jux, Carino ft. Singah, Pinda, Haula ft. Dayoo na Nigee unaofanya vizuri kwa sasa.

Ndoa yake na PKP ilitamatika baada ya Ommy Dimpoz kusainiwa RockStar Africa (2017) na baadaye Sony Music Entertainment Africa, na tangu wakati huo Nedy Music akawa anafanya kazi kama solo na ndipo alipopata mafanikio zaidi kimuziki.

Tetesi za kuachana na PKP zilianza alipoachia wimbo, One and Only (2018) akimshirikisha Ruby, video yake ilitoka bila nembo (logo) ya PKP ndipo maneno yakaanza ila mwaka mmoja kabla Dimpoz kuiiambia XXL ya Clouds FM kuwa amemtafutia Nedy menejimenti.

Hata hivyo, wimbo huo uliotengenezwa na Prodyuza Yogo Beats ndio ulimfanya Nedy Music kuandika rekodi katika muziki wa Zanzibar na hadi sasa inaishi na kitu ambacho amekuwa akijivunia kwa miaka yote.

Nedy Music ndiye msanii wa kwanza kutoka Zanzibar kushinda Tuzo ya All Africa Music Award (AFRIMA), usiku wa kuamkia Novemba 25, 2018 alishinda tuzo hiyo Ghana katika kipengele cha African Fans Favourite.

Ni kupitia wimbo ‘One and Only’ ft. Ruby, aliwazidi kete washindani wake kama Phyno - Nigeria (N.W.A) ft. Wale, Kojo Funds Ghana (Stallin), Aminux Morocco (Ghanhibo), Ommy Dimpoz- Tanzania (Yanje) ft. Seyi Shay, Not3s - Nigeria (My Lover) n.k.

“Kuwa mshindi kwenye tuzo kubwa kama hizi ambazo zimeunganisha mataifa 54 ni kubwa sana kwangu na nchi yangu Tanzania na wote wapenda burudani ambao hamkuchoka kupiga kura,” anasema Nedy Music.

Kufuatia ushindi huo Nedy Music uliungana na wasanii wengine wa Bongofleva kama Diamond Platnumz, Vanessa Mdee, Alikiba, Nandy n.k ambao hapo awali walishinda tuzo za AFRIMA kwa nyakati tofauti. 

Tuzo za AFRIMA zilianza Desemba 2014 kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU) na kwa mara ya kwanza zilifanyika Nigeria kisha Ghana zikiwa na lengo la kuutangaza na kuupa thamani muziki wa bara hilo. Tuzo hizi ambazo mshindi hupatikana kwa kura za mashabiki (public votes) na wataalamu wengine kutoka tasnia ya burudani, zina jumla ya vipengele 37 vinavyojumuisha kanda tano za Afrika ambazo ni Afrika Mashariki, Afrika ya Kati, Magharibi, Kaskazini na Kusini mwa Afrika.