Nay wa Mitego awafurusha Harmonize na Ibra

Wednesday September 01 2021
ney pic
By Nasra Abdallah

Ikiwa ni siku ya pili tangu aachie wimbo wake wa Rais wa Kitaa, msanii Nay wa Mitego ameweza kuwafurusha Harmonize na Ibra kwa kukamata namba moja YouTube.
Kabla nyimbo hiyo haijatoka,  wimbo wa Teacher wa Harmonize ndio ulikuwa unakamata namba moja ukifuatiwa na wimbo  wa Jipinde wa Ibra, wasanii ambao wote hawa wanatoka lebo ya Kondegang.
Hata hivyo leo Jumatano Septemba Mosi, 2021 Nay ambaye jina lake halisi ni Elibariki Minja, amewapita wasanii hao kwa kasi ya 4G kwa kukamata namba moja,ikiwa ndio kwanza nyimbo yake ina siku ya pili.
Hii inafanyika ikiwa walioitazama nyimbo yake hiyo hawajafika hata 600,000, wakati Teacher ikiwa imetazamwa mara milioni 2.5  na Jipinde iliyotoka wiki moja iliyopita ikiwa imetazamwa mara milioni 2.7.
Wachambuzi wa masuala ya biashara huko YouTube wanasema kuna namna nyingi inaangaliwa ili nyimbo itrend namba moja ikiwemo watu waliopenda, watu walioitazama kwa muda mrefu na pia walioweka maoni yao.
Kwa namna hii inavyoonekana kwa haraka huenda Nay kabebwa na mashairi ya wimbo wake ambayo yameongelea mambo mbalimbali yanayoendelea nchini ikiwemo suala zima la tozo ambalo siku za karibuni liliibua mjadala.

Advertisement