MUSIC FACTS: Albamu ya Ferooz 'Safari' iliuza nakala 200,000 kwa wiki moja tu!

ALIFANYA vizuri tangu akiwa na kundi la Daz Nundaz hadi aliposimama pekee yake, mtindo wake wa kipekee katika uimbaji ulipelekea Ferooz kupendwa na wengi na ni miongoni mwa wasanii walioonja mafaniko ya kiuchumi kutokana na kazi zao.

Ferooz ameweza kutoa ngoma kubwa na bora katika Bongofleva kwa muda wote, ngoma zake zinasifika kwa kuigusa jamii vilivyo upande wa elimu na hata kuburudisha. Huyu ndiye Ferooz;


1.Wakati anaaza muziki alikuwa anajiita Kamanda, ila walipokuja kutoa wimbo 'Kamanda' wa kundi la Daz Nundaz akaamua kutumia jina lake halisi, Ferooz. Hiyo ni kutokana na aina ya maudhui ya wimbo huo (kifo), hivyo akaona kama atakuwa amejiimbia yeye, ndipo akarudi kwenye jina la Ferooz ambalo lilikuwa maarufu shule.


2. Wimbo wa Ferooz 'Bosi' aliuandika akiwa kidato cha sita shule ya Makongo, wimbo huo uliotayarishwa na P Funk Majani ndani ya Bongo Records, pia Bizman amehusika kwa kiasi kikubwa kuweka vionjo vile kama vya asili vinavyosikika.


3. Starehe ndio wimbo wa kwanza wa Ferooz kushutiwa video, kabla ya Starehe nyimbo ambazo Ferooz alitoa hapo awali kama Bosi na Jirushe hakufanya video zake licha ya kufanya vizuri kila sehemu.


4. Ferooz anaamini Daz Nundaz ndio waliotambulisha muziki wa kuimba kwenye Bongofleva na sio Dully Sykes kupitia wimbo wake, Salome kama ambavyo inatajwa. Hoja ni kwamba wakati Salome inatoka, tayari Daz Nundaz walikuwa washatoa ngoma kama Kamanda na Barua.


5. Video ya wimbo wa Ferooz, Starehe iliyotoka mwaka 2004 iligharimu Sh1 milioni, fedha ambayo ilikuwa kubwa kwa msanii kufanya video kwa wakati huo. Video ilifanyika na Benchmark Production, kampuni yake Madam Rita ambayo ilikuwa inafanya vizuri sana wakati huo.


6. Bifu la Daz Nundaz na Solid Ground Family liliibuka baada ya Solid Ground kurudia wimbo wa Ferooz uliokuwa bado haujatoka wala kurekodiwa rasmi ambao ulikuwa kwenye kanda aliyoipoteza akiwa shule.

Ikumbukwe Ferooz alikuwa anarekodiwa katika kanda na DJ Ibraah ambaye alikuwa anamtafutia nafasi, sasa moja ya kanda ndio ilipotea na Solid Ground wakaamua kupita nayo.


7. Ferooz alitumia muda wa miezi sita kuandika wimbo, Starehe hadi ukakamilika, alimshauri P Funk Majani kutengeneza mdundo wa kuchezeka kutokana watu wanaweza wasiupende wimbo huo kutokana na ujumbe wake. Hata hivyo, ulivyotoka bado ulipendwa sana na ni miongoni mwa nyimbo bora za Bongofleva kwa muda wote.


8. Prodyuza P Funk Majani ndiye alimchagua Ferooz kuimba 'chorus' ya wimbo wa Mangwair, Mikasi, hata hivyo, tayari Mangwair  alikuwa amesharekodi sehemu hiyo, hivyo Ferooz alikuja kurudia kama ilivyokuwa.

Ferooz ambaye alikuwa ndiye msanii wa mwisho kurekodi sehemu yake katika wimbo huo, alimuomba Majani akarekodi 'chorus' hiyo nyumbani ila akakataliwa.


9. Albamu ya kwanza ya Ferooz, Safari (2005) ni miongoni mwa albamu za Bongofleva zilizouza sana, albamu ya Safari iliuza nakala (kanda) 200,000 katika wiki yake ya kwanza sokoni, hivyo akarudi kwa Msambazaji kugonga muhuri wa nakala nyingine tena. Inakadiriwa albamu yote alipokea zaidi ya Sh150 milioni.


10. Baada ya kupewa mkataba wa kufanya albamu chini ya Bongo Records, wimbo wa kwanza kurekodi Ferooz  ulikuwa ni Jirushe, na ulipomalizika P Funk Majani aliuchukua na kuupeleka vituo vya Radio bila hata Ferooz kujua.

Na siku moja Ferooz akiwa shule akapigiwa simu na Majani na kumuita studio, alipofika ndipo akakutana na remix ya ngoma hiyo ambapo Jay Moe alishirikishwa, Majani ndiye aliyemchagua Jay Moe na hadi anarekodi Ferooz  alikuwa hajui chochote.