MOI yathibitisha kifo cha Director Khalfani

Muktasari:

  • Siku 146 zikiwa zimepita tangu kifo cha mwongozaji wa muziki Nisher Davie kikiwa hakijapoa, Tanzania imepoteza mwongozaji mwingine maarufu ‘Director Khalfani Khalmandro’ aliyefariki akipatiwa matibabu Taasisi ya Mifupa MOI.

 Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) imethibitisha kifo cha muongozaji wa video za muziki nchini Tanzania, maarufu ‘Director Khalfani Khalmandro’.


Kwa mujibu wa MOI, Khalmandro amefariki wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika taasisi hiyo usiku wa kumkia leo.


Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Mei 5, 2024, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano MOI, Patriki Mvungi amesema, “Ni kweli amefariki saa sita usiku wakati akiendelea na matibabu, Director Khalfani aliletwa hapa kwetu MOI akitokea Hospitali ya Taifa Muhimbili.”

Kifo hicho kimekuja wiki kadhaa tangu taarifa zake za kuomba msaada wa matibabu zisambae huku baadhi ya watu wake wa karibu wakieleza namna fedha nyingi za matibabu yake zinavyohitajika ili kulipia gharama hospitali.

Hata hivyo, taarifa za awali zilieleza kuwa Khalmandro alifikishwa hospitalini hapo akiwa na tatizo la damu kuvilia kwenye ubongo, lililosababisha changamoto ya kupooza upande wa kulia wa mwili wake.

Mwongozaji huyo amefariki ikiwa ni miezi michache tangu kifo cha mwongozaji mwingine maarufu nchini Nisher Davie hakijapoa miongoni mwa wapenzi wa burudani nchini, aliyefariki Desemba 12, 2023.

Wakati wa uhai wake Khalfani, alijipatia umaarufu kwa kuongoza video za wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya akiwemo Linah, Shilole, Aslay, NavyKenzo, Christian Bella, Baby Madaha Chinbees na wengine wengi.

Kufahamu zaidi kuhusu taarifa ya kifo cha Khalmandro endelea kufuatilia mitandao yetu ya kijamii na website ya Mwananchi.