MKOJANI-3: Huyo Tin White mbona freshi tu!

KATIKA toleo lililopita Mkojani alielezea maisha yake kwa undani tangu kuwa staa. Alielezea mambo ya maendeleo aliyoyafanya, pia aliweka wazi kuhusu namna watu wanavyomchukilia na yeye alivyo.

Katika toleo hili anaongelea mambo muhimu kuhusu sanaa yake ikiwemo tetesi za kuwepo kwa ugomvi kati yake na wachekeshaji wenzake Tin White na Ringo. Shuka nayo


UGOMVI NA TIN WHITE

Kwa namna moja ama nyingine unaweza kusema wachekeshaji Tin White na Ringo ndiyo waliompa umaarufu Mkojani wakati alipoanza kuigiza kwa jina la Kipupwe.

Kipindi hiko alikuwa akiigiza kwenye filamu za swahiba zake hao ambao walikuwa maarufu zaidi yake, na hata alipoanza kupata umaarufu bado alienda kuigiza nao bega kwa bega.

Hata hivyo, siku hizi amepunguza kabisa au unaweza kusema anaigiza peke yake bila kina Ringo na Tin White huku kukiwa na tetesi kwamba maswahiba hao wameshazinguana, hapa kipupwe anaelezea ishu nzima ilivyo.

“Tin White na Ringo ni ndugu zangu na wala hatuna tatizo lolote. Tumeacha kuigiza pamoja kwa sababu watu walikuwa wanasema tunabebana, yaani kwa mfano walikuwa wanasema mimi sijui kuigiza, nabebwa na kina Tin White. Kwahiyo tukasema tuache kuigiza pamoja kwanza ili tuwaonyeshe watanzania uwezo wetu na ndicho tunachofanya.” anasema.

Anaongeza kuwa yeye na Tin White wana filamu zaidi ya 11 ambazo bado hawajazitoa. Na zaidi anasema ni watu wanaowasiliana karibu kila siku iendayo pamoja.


NDOA YA WAKE WENGI

Mkojani anathibitisha kwa sasa ana mwanamke anayeishi naye ambaye ni mchumba wake. Anasema ameshafanya taratibu zote na kilichobaki ni harusi na kuufinya ubwabwa tu.

Lakini mwandishi alimpotupia swali la kizushi la kwamba je ana mpango wa kuoa mke zaidi ya mmoja, Mkojani alikataa na kudai kuwa yeye hawezi kupenda wanawake wawili kwa wakati mmoja.

“Dini inaruhusu lakini mimi moyo wangu hauwezi. Namudu mwanamke mmoja tu kwahiyo sitarajii kuoa mke zaidi ya mmoja.” anasema.

Kabla ya kuwa na mwanamke huyu Mkojani aliwahi kufunga ndoa na mwanamke mwingine ambaye walizaa mtoto mmoja anayeitwa Masoud, ambaye ni wa pili kwa Mkojani lakini waliachana. Pia, mtoto wa kwanza wa staa huyo anaitwa Nasri ambaye anasema alimpata alipokuwa kijana mdogo, enzi za damu kuchemka.


ISHU ZA KALUMANZILA

Moja ya mambo yaliyowahi kuvuma kwenye mitandao ya kijamii ni kwamba eti baba mzazi wa Mkojani ni mganga wa kienyeji, na waswahili wakasema eti mzee wake anampigia manyanga ndiyo maana anatrendi.

Akijibu kuhusu hilo, Mkojani kwanza anakanusha taarifa za kwamba baba yake ni mganga wa kienyeji lakini pili anasema anaamini kuhusu kuwepo kwa matumizi ya nguvu za giza ila hajawahi kuzitumia.

“Mambo ya ushirikina na waganga yapo, Mtanzania anayesema haamini anaongopa, wote hapa tulivalishwa vitambaa vyeusi tulipokuwa watoto, ni ushirikina huo. Lakini mimi binafsi sijawahi kuutumia kwenye kazi zangu na wala siamini kama unaweza kunisaidia.” anasema Mkojani.

Anaongeza kuwa kama kweli waganga wangekuwa wanasaidia, basi kila Mtanzania angekuwa anatrendi kwa sababu karibu kila familia ya Kitanzania ina mganga.


KUMUIGA MAJUTO

Ikumbukwe kuwa kabla ya kuanza kujiita Mkojani, staa huyo alikuwa akijiita Kipupwe. Lakini tangu amebadilika kuwa Mkojani pia amekuwa akishambuliwa na watu mitandaon kwamba eti anagandamizia swaga za marehemu mzee Majuto kwenye uchekeshaji wake.

Mkojani anapangua tuhuma hizo kwa kudai kuwa sio kwamba yeye anamuiga Majuto, isipokuwa watu wanamfananisha kutokana na muonekano.

“Simuigi, watu wananifananisha naye kwa sababu kupitia uhusika wangu wa mkojani navaa msuli, balaghashehe na hata naigiza kama mtu mtata vitu ambayo marehemu alikuwa anavifanya, nadhani ndiyo maana watu wananifanisha naye.” anasema.

Alipoulizwa anajisikia kufananishwa na Majuto Mkojani anasema ni utamu tu kwa sababu anafananishwa na mtu anayempenda.

“Mi naona utamu, unapofananishwa na mfalme maana yake una dalili ya kuwa mfalme pia.” anasema.


AZIPOTEZEA TAMTHILIA

Aidha wasanii wote maarufu kwa sasa wamepata madili ya kurusha kazi zako kupitia chaneli kubwa kama vile za Sinema Zetu ya Azam TV na Maisha Magic Bongo ya DSTv; msanii kama Tin White, Mboto ni mifano halisi. Lakini kwanini yeye hayuko huko, hapa Mkojani anafichua siri.

“Hayo makampuni yalinitafuta mimi lakini nilikataa kwa sababu pesa ilikuwa ndogo kwa sababu naamini hilo linatakiwa liwe Tobo langu. Sioni sababu ya kupeleka kazi zangu kwenye chaneli ya TV kwa mkataba wa milioni moja, wakati kuna wengine wanapata mpaka milioni 150 kwa mwezi. Nataka zaidi ndo maana sijafanya nao kazi.” anasema.


MCHONGO UNAOMLIPA ZAIDI

Mkojani anaeleza kuwa kazi zake anauza kwa namna kuu mbili, kupitia mitandao ya kijamii kama vile Youtube pamoja na mtindo wa zamani uliozoeleka wa kuuza DVD. Alipoulizwa kuhusu pesa zaidi anaingiza kupitia wapi Mkojani hakusita kuweka wazi kuwa ni kwenye mitandao ya kijamii.

“Pesa zaidi napata kwenye mitandao. Tena mpaka najilaumu kwanini nilichelewa kuweka kazi zangu huko kwa sababu wasanii wa filamu tumechelewa sana, tulikuwa tunadhani Youtube ni kwa ajili ya wanamuziki tu.” anasema.

Mkojani aliwahi kumwaga chozi ndani ya ndege, je unajua ilitokana na kitu gani na anamzungumziaje Joti? Malizana naye kesho.

Itaendelea