Prime
Dada: Dulla Makabila kwa Simba, Yanga ukweli ndo huu!

Muktasari:
- Sasa utata huu ambao wengi wanatamani kufahamu hasa mashabiki zake, umewekwa hadharani na dada yake, Amina vikoba na kitendo cha kuhamahama timu ni kwa sababu anazozijua Makabila mwenyewe.
KUMEKUWA na utata juu ya msanii wa Singeli, Dulla Makabila ni shabiki wa timu gani hapa Bongo. Hii imetokana na kila wakati kubadilika na leo ni Simba na kesho Yanga.
Sasa utata huu ambao wengi wanatamani kufahamu hasa mashabiki zake, umewekwa hadharani na dada yake, Amina vikoba na kitendo cha kuhamahama timu ni kwa sababu anazozijua Makabila mwenyewe.
Hata hivyo, Amina Vikoba ambaye ni msanii maarufu wa maigizo nchini na kipenzi cha wengi kupitia tamthilia mbalimbali, alisema kabla ya baba yao hajafariki dunia, Dulla alikuwa shabiki wa Yanga, lakini kwa sasa amekuwa hatabiriki kwani anaweza kuamka leo Simba usiku akawa Yanga.
"Yule mdogo wangu Dulla Makabila kichwa chake anakijua mwenyewe, maana wakati baba yuko hai sisi wote tulikuwa tunashabikia Yanga, ila kwa sasa mtu huwezi kumpangia, kwanza yule Dulla kwenye mpira hayuko kivile yaani sio shabiki sio mpenzi sana, yeye zake ni kukaa atunge nyimbo zake maisha yaende," alisema Amina.
Kwa upande wake, Amina alisema yeye ni shabiki wa Yanga na ametabiri mwaka huu itachukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
"Mimi kama mimi ni shabiki wa Yanga, ukiachana na kusema hatuchezi ubingwa lazima, Simba wajitahidi sana wasipoteze mechi zao zijazo," alisema Amina Vikoba.
Aidha Amina amezungumzia kuhusu tabia ya Dulla Makabila kupenda kutunga nyimbo za vijembe pale anapoona adui yake amepata majanga, kama ilivyoonekana kwa aliyewahi kuwa mkewe Zaylissa alivyoachana naye akatunga wimbo unaoendana na mambo aliyokuwa akiishi ndani ya nyumba, pia hata alipoolewa na Haji Manara akaachika ametunga wimbo.
"Mie naona sana tu kwani Dulla anaenda na upepo ulivyo, maana kama jambo linatokea halafu anakuwa chapu kuingia studio hicho ni kipaji alichokuwa nacho," alisema Amina.