Mastaa wa Bongo waliopigiwa Saluti na Mastaa wa Mamtoni

Friday November 27 2020
mastaa pic

KARIBU kila mwanamuziki Bongo ana ndoto ya kufanya kazi na msanii mkubwa wa mamtoni. Rapa Rosaree amewahi kukiri kuwa anatamani kufanya kazi na Jay Z ile mbaya, Diamond yeye alishazungumza sana jinsi ndoto yake ya kufanya kolabo na Usher Raymond inavyomkosesha usingizi, wakati upande wa Chid Benz yeye humwambii kitu kuhusu 2pac Shakur mpaka kuna siku alitania kuwa wameshafanya ngoma na supastaa huyo wa Marekani aliyeuawa kwa risasi mwaka 1996 - watu wakaona kama amedata.

Lakini kwanini ndoto hizi zinabaki kuwa ndoto kwa muda mrefu? Ni kwa sababu wasanii wakubwa wa mamtoni ni wagumu kuwapata. Yaani mpaka msanii wa Bongo afanikiwe kumshawishi msanii wa mbele akubali kufanya naye ngoma au hata kumsikiliza ni lazima awe amepitia mageti mengi ya vizuizi.

Hata hivyo, licha ya ugumu uliopo, kuna wasanii wa Bongo, tena madogo janja tu, wamevunja tamaduni kwa kuwafanya wasanii wa mamtoni wawapigie saluti kwa kipaji na uwezo wao wa kutisha kwenye muziki. Nimekuwekea listi ya wasanii hao na walichofanya hapa chini.

PITBULL & RAYVANNY

Vanny Boy alipotoa wimbo wa Tetema milango kibao ilifunguka. Ngoma ilikuwa hit kiasi kwamba wasanii wengi kutoka nje walitaka kuifanyia remix na ndio maana wimbo huo una remix mbili mpaka sasa.

Moja ya wasanii waliokiri kumkubali staa huyo mwenye asili ya Mbeya City alikuwa ni mkali wa mangoma ya club kutoka Marekani, Armando Perez maarufu Pitbull na kwa mujibu wa Rayvanny ni kwamba jamaa huyo alipoisikia ngoma tu akaipigia saluti na kutaka kuifanyia jambo hivyo akamtafuta na wakafanya remix ya wimbo huo.

Advertisement

Hata hivyo, Vanny Boy na uongozi wake waliona itapendeza zaidi kama wataongeza wasanii wengine wenye asili ya kilatini kwenye ngoma hiyo, ndipo Rayvanny akafanya mpango wa kumuongeza Mohombi na msanii mwingine wa kuitwa Jeon na kufanya remix hiyo iwe na jumla ya wasanii watano ndani; Pitbull, Mohombi, Jeon, Diamond Platnumz na Rayvanny mwenyewe.

Ukubwa wa Pitbull unaweza kuupima kwa mafanikio yake ya kimuziki, kwani anamiliki tuzo tatu za Billboard na moja ya Grammy.

FAT JOE & CONBOI

Mtoto wa Kinondoni, mkali wa michano, alipotoa ngoma yake ya Till I Die ilimfikia rapa kibonge kutoka Marekani Fat Joe. Mshikaji aliikubali michano ya dogo kiasi kwamba alishindwa kujizuia kumtumia meseji DM instagram ambapo aliandika “King, see U grinding”

Stori ilikuwa hivi, ConBoi ambaye zamani alikuwa memba wa kundi la OMG, alipotoa ngoma yake alikuwa anawatumia link wadau wengi wa Hip Hop, moja ya wadau hao alikuwa ni Fat Joe, na hapo sio kwamba alikuwa wanafahamiana, hapana, yeye alikuwa anatumatuma tu.

Lakini kumbe ngoma ilipomfikia jamaa aliisikiliza na akarudi kumpa mrejesho wa kwamba ngoma ilikuwa ni ya moto na jamaa ni mbadi sana kwenye kuchana.

“Nilituma lakini sikuwa na matarajio kwamba atanijibu. Hanijui, wala hajawahi kunisikia, ana followers zaidi ya milioni 3, atakuwa ana pokea DM nyingi, kwahiyo isingewezekana akanijibu, hicho ndo nilichokuwa nikiamini, lakini kila kitu kilienda tofauti,” anasema Conboi.

Conboi alishea screenshot za chat zake na Fat Joe na pia kuwahakikishia mashabiki zake kwamba huenda yeye na Fat Joe wakafanya jambo siku za usoni.

Fat Joe amehit na ngoma kama vile All The Way Up, Make It Rain aliyomshirikisha Lil Wayne, lakini pia kwa kipindi chote cha muziki wake amewahi kushinda tuzo kubwa za muziki kama vile Grammy, BET, Billboards na nyinginezo.

SWIZZ BEATZ & MEJA KUNTA, LAVALAVA

Prodyuza mkubwa wa Marekani, Swizz Beatz alipoisikia ngoma ya singeli ya Wanga (Wabaya) iliyoimbwa na Meja Kunta ft Lavalava alidata ile mbaya na akashindwa kujizuia kuomba atumiwe chap kwa haraka. Na alipotumiwa tu akashea video inayomuonesha mke wake, mwanamuziki Alicia Keys akicheza wimbo huo.

Mchezo uko hivi, wimbo huo ulipotoka Diamond aliupost kwenye akaunti yake ya Instagram, Swizz alipouna ali-comment kuomba atumiwe wimbo huo na Diamond alimtumia. Baadaye jamaa alishea kwenye akaunti yake lakini pia alimtag Lavalava.

Kama hiyo haitoshi, baada ya wiki kadhaa kupita Swizz Beatz alishea mdundo wa wimbo wa Wanga lakini safari hii ukiwa umetiwa vionjo vya kimamtoni kana kwamba alikuwa anataka kufanya aina mpya ya muziki.

ALICIA KEYS & DIAMOND

Licha ya kwamba Diamond Platnumz ameshafanya kazi na wasanii wengi wa Mamtoni, lakini Alicia Keys anaonekana kumkubali mkali huyu wa Bongofleva zaidi ya kawaida. Kwanini?

Kwanza ni yeye ndiye aliyemuita Diamond kwa ajili ya kumshirikisha kwenye wimbo wake wa Wasted Energy uliotoka mwezi Septemba mwaka huu. Lakini pili, wimbo huo ulikuwa ndani ya Albamu ya Alicia Keys, katika albamu hiyo kulikuwa na ngoma nyingine ambazo ameshirikisha wasanii wa kiwango cha kushabihiana na Diamond, lakinia huwezi kuamini, mara nyingi Alicia anapokuwa kwenye intavyuu amekuwa akimtaja Mondi zaidi ya wasanii wengine aliowashirikisha kwenye albamu hiyo.

Kama hiyo haitoshi, hata kupitia kwenye akaunti zake za Instagram, na Twitter amekuwa akiweka wazi jinsi gani anamtazama Diamond kama msanii mkali sana lakini pia mwenye mashabiki wenye upendo.

CASSIDY & MEX CORTEZ

Kwa wanaopenda Hip Hop ngumu wanamfahamu Cassidy, rapa kutoka New York, Marekani ambaye pia anatajwa kuwa moja ya hazina ya wana Hip Hop wanaojua kufanya Free Style ile mbaya.

Mwanzoni mwaka huu Cassidy aliona video ya rapa wa Bongo anayefahamika kwa jina la Mex Cortez.

Akamkubali kinoma kiasi kwamba alimuendea DM na kumtaka ikiwezekana amshirikishe kwenye albamu zake zijazo.

Advertisement