Lulu Diva, Marioo wamjibu Babu Tale

Tuesday June 07 2022
marioo pic
By Nasra Abdallah

SIKU moja baada ya Mbunge wa Morogoro Kusini  Mashariki, Hamis Taletale maarufu kwa jina la Babu Tale kuwatolea mifano wasanii Lulu Diva na Marioo, wenyewe wamjibu.
Akiwa anachangia jana Jumatatu Juni 6, 2022 bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo katika vikao vya bunge vinavyoendelea jijini Dodoma, Mbunge huyo aligusia suala la mirabaha na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).
Tale ambaye pia ni meneja wa lebo ya WCB, alidai taasisi ya Haki Miliki Tanzania (Cosota) imekuwa haitendi haki katika ugawaji mirabaha na kueleza kuwa  kama siku wakipelekewa Takukuru watafungwa wote.
Katika hilo alitolea mfano ugawaji wa mirabaha uliofanyika Januari mwaka huu, kuwa haukuwa wa haki na kueleza kuwa haiwezekana msanii Lulu Diva katika ugawaji huo akapata Sh550,000 huku msanii wake Kassim Mganga, akipata Sh50,000.
“Mi natoa mfano, nina msanii wangu anaitwa Kassim Mganga anatokea Tanga, hakuna asiyeimba nyimbo zake kwenye msimu wa harusi.
“Mheshimiwa Naibu Spika, Kassim Mganga unamuita unaenda kumpa Sh50,000 ,halafu unaenda kumuita Lulu Diva unampa Sh550,000.
“Umetumia vigezo gani, kuna utaratibu gani ambao unatumika Cosota kugawa mirabaha,"
Aliongeza kuwa wasanii wengi wamekuwa wakipewa  pesa  kutokana na ukubwa wao kwenye mitandao ya kijamii ya Instagram na makelele tu.
Akijibu hilo kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram, Lulu ameandika ”Mheshimiwa angeweza kutetea maslahi ya wasanii wake pasina kunitaja, angekua amesaidia sana tasnia leo,”.
 
Akiizungumzia Basata, Taletale  amesema ni chombo cha kuwasaidia wasanii, lakini bahati mbaya imekuwa Polisi wa wasanii na kubainisha kuwa hawana utaratibu wa kuwapa elimu na semina wasanii na badala yake wana utaratibu wa kufungia nyimbo zao.
Katika kukazia hoja yake hiyo, aliomba kuimba kibwagizo cha ’Mama Aminaa’  kinachopatikana kwenye wimbo wa Marioo unaoitwa ‘Mama Amina aliouimba kwa kumshirikisha Sho Madjozi na Bontle Smith, na kueleza kuwa hana uhakika kama kuna Mbunge ataitikia.
Akilizungumzia hilo, alipohojiwa na kituo cha redio Clouds, Marioo, amesema sio nia yake kumjibu Babu Tale kwa kuwa anamuheshimu sana kwenye tasnia ya muziki.
Badala yake alieleza kuwa alichomaanisha kwenye wimbo huo ni Mamaa Amina ambaye alikuwa akimlalamikia namna anavyomuumiza moyo kwenye mahusiano yao na kueleza maana nyingine zinazosemwa ni za watu wenyewe lakini yeye ndicho alichomaanisha kwa kumuita mama huyo.

Advertisement