Lady Jaydee msikilize Mimi Mars

MWANADADA anayefanya vizuri kwenye tamthilia ya Juakali, Marianne Mdee ‘Mimi Mars’ amemtaja Judith Wambura ‘Lady Jaydee ama Jide’ kuwa ni msanii anayetamani kukutana naye kwani ana maswali mengi ya kumuuliza huku akitaja wimbo wa Yahaya kuwa ndio wimbo wake pendwa kati ya nyimbo zilizoimbwa na mkongwe huyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mimi Mars alisema tangu ameanza kufanya muziki kwa asilimia kubwa amepata bahati ya kukaa na mastaa kibao lakini hajabahatika kukutana na kukaa pamoja na Lady Jaydee ambaye anakiri kuwa anatamani kumuona.

“Siwezi kukwambia ni nini nataka kumwambia ila nina maswali mengi juu yake kuhusiana na maisha ya sanaa pia kwenye nyimbo zake nyingi alizoimba navutiwa nazo zote ila Yahaya ni moja ya wimbo bora kwangu kwa sababu kafikisha ujumbe,” alisema na kuongeza;

“Mayahaya wapo wengi mjini na nimekutana nao hivyo ujumbe huo utakuwa umewafikia na unaendelea kuwafikia unajua wanaume wana maisha mengi sana, mtu anataka kuonekana ana kila kitu wakati maisha yake ni ya kawaida wanapenda mambo makubwa na hawana lolote,” alisema.

Katika hatua nyingine alizungumzia tamthilia ya Juakali ilipofikia sasa kuwa amekuwa akipitia wakati mgumu kutoka kwa mashabiki wanaofuatilia kutokana na tukio alilomfanyia Luka ambaye ndiye alikuwa mpenzi wake.

“Nilifanya vile ili kulinda penzi langu na ni maigizo lakini Watanzania wanalichukulia kiuhalisia sina tabia hizo naigiza tu na hayo mambo yapo kwenye jamii tunazoishi nimecheza kufundisha na sio kuumiza watazamaji,” alisema.