Katisha Mondi na rekodi ya kugawa magari

Katisha Mondi na rekodi ya kugawa magari

HAKUNA ubishi kuwa Diamond Platnumz ndiye msanii anayeongoza Bongo kwa kutoa zawadi ya magari kwa wasanii wa lebo yake, WCB Wasafi na watu wake wa karibu katika kazi yake.

Huu umekuwa ni utamaduni wa mwimbaji huyo wa kutoa zawadi ya magari kwa wasanii wenzie, wapenzi wake, wafanyakazi wake na watu wake wa karibu katika tasnia. Hii ni orodha ya watu wachache waliokumbana na bahati hiyo.


Muhidin Gurumo -Fun Cargo

Agosti 2013, Diamond alimpa zawadi ya gari aina ya Fun Cargo msanii mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Muhidin Gurumo (sasa marehemu), aliamua kufanya kutokana na kutambua mchango wake baada ya kustaafu muziki.

Gurumo aliyekuwa mwanamuziki wa bendi ya Msondo Ngoma alikabidhiwa gari hilo kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, wiki moja baada ya kutangaza kustaafu muziki akiwa na umri wa miaka 73, baada ya kuwa kwenye tasnia hiyo kwa miaka 53.


Wema Sepetu -Nissan

Wakati penzi lao limepamba moto, Septemba 2014 katika Birthday ya Wema Sepetu, Diamond aliamua kumnunulia bibie gari aina ya Nissan kuuonyesha ulimwengu ni kwa kiasi gani anampenda.

Diamond ambaye wakati huo alikuwa anatamba na wimbo, My Number One alisema alitamani kumpa Wema vingi kuonyesha ni jinsi gani anampenda lakini hana uwezo huo.

Aliongeza kama kumpenda Wema hadi kumpa zawadi ya gari ni wendawazimu, basi ni heri asalie na uchizi wake kuliko kupata ufahamu.


Harmonize & Rayvanny (Rav4, Mark X)

Kwa nyakati tofauti mwaka 2016 Diamond kupitia WCB alitoa zawadi ya magari kwa Rayvanny na Harmonize ambao kwa sasa wameachana na lebo hiyo kwa sababu mbalimbali.

Katika birthday ya Rayvanny alikabidhiwa gari aina ya Rav4 yenye rangi nyeusi katika sherehe ndogo iliyofanyika nyumbani kwa kina Diamond Madale, Dar es Salaam.

Hatua hiyo ilikuwa ni baada ya uongozi huo kumkabidhi Harmonize gari aina ya Mark X yenye rangi nyeusi huku Diamond akitembelea gari aina ya BMW X6 kwa wakati huo.


Lava Lava & Mbosso -TOYOTA Harrier

Mara baada ya kuachia tu wimbo wao unaokwenda kwa jina la Jibebe hapo Agosti 2018, Diamond aliamua kuwakabidhi kila mmoja gari lake aina ya Toyota Harrier wasanii hawa waliopo chini ya lebo yake, WCB.

Ikumbukwe wasanii hawa wawili wamepishana kipindi kifupi kujiunga kwao na WCB, Lava Lava akitambulishwa Mei 2017 huku Mbosso kwa upande wake akitangazwa rasmi Januari 2018 mara baada ya kuachana na kundi la Yamoto Band.


Lukamba - Altezza

Huyo alikuwa ndiye mpigapicha rasmi wa Diamond ambaye alikuwa akizunguka na Diamond duniani kote kwa ajili ya kuchukua matukio yote muhimu ya mwimbaji huyu.

Oktoba 2018, Diamond alimkabidhi Lukamba gari aina ya Altezza kama kuthamini mchango wa kazi yake kitu kilichomtoa machozi kijana huyo ambaye ilikuwa ni mara ya kwanza kumiliki gari.


Tanasha -Land Cruiser V8

Julai 2019 Diamond aliwazawadia magari ya kifahari mama yake mzazi (Mama Dangote) pamoja na aliyekuwa mpenzi wake, Tanasha Donna ambao kwa pamoja walikuwa wakisherekea siku zao za kuzaliwa.

Tukio hilo lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam, Diamond alikabidhi funguo za magari mawili mapya aina ya Toyota Land Cruiser V8 kwa wawili hao. Hata hivyo, Aprili mwaka 2020, Tanasha akizungumza na True Love Magazine East Africa nchini Kenya alisema aliliacha Tanzania gari hilo alilozawadiwa na Diamond.


Zuchu - Vanguard

Julai 2020, Diamond alimzawadi Zuchu gari jipya aina ya Toyota Vanguard katika hafla iliyorushwa mubashara kupitia shoo ya Big Sunday Live ya Wasafi TV. Zawada hiyo ilikuja baada ya saa 24 tangu Zuchu kufanya uzinduzi wa Extended Playlist (EP) yake iitwayo ‘I Am Zuchu’ kwenye Ukumbi wa Mlimani City.

Ikumbukwe Zuchu alipewa zawadi hiyo ikiwa ni miezi mitatu tu tangu ajiunge kwenye lebo ya WCB Wasafi akiungana na mwenzake kama Rayvanny, Lava Lava, Mbosso na Queen Darleen kwa wakati huo.


Baba Levo - Harrier

Januari 2021, msanii wa muziki Bongo, Baba Levo alionyesha gari ambalo amenunuliwa na Diamond Platnumz, kwa mujibu wa msanii huyo, Diamond alitoa fedha kiasi cha Sh26.5 milioni kununua gari hilo aina ya Toyota Harrier.

Inawezekana Diamond aliamua kumnunua Baba Levo gari hilo kutokana na kuwa miongoni mwa wafanyakazi kwenye kituo chake cha redio, Wasafi FM, huku baadaye wakija kutoa wimbo wa pamoja unaokwenda kwa jina la Shusha.


Coy Mzungu - Mark X

Katika jukwaa la Cheka Tu pande za Mlimani City, Februari 2021 Diamond aliibuka na kutangaza kumpatia gari aina ya Toyota Mark X Mchekeshaji Coy Mzungu ambaye ni mshirika wake kibiashara.

“Nina maagizo kutoka taasisi ya Wasafi, nimeambiwa nimletee gari Coy, hakuwa anajua ikabidi nije kumfanyia ‘suprise’, lakini anafanya kazi nzuri sana na anaipa thamani comedy, na sisi kama vijana ni jukumu letu kumuunga mkono,” anasema Diamond.


Bajuni ‘Dancer’ - Toyota Crown

Kufika Desemba 2021, Diamond alimzawadia dansa wake, Bajuni gari jipya aina ya Toyota Crown, Bajuni amekuwa akifanya vizuri kazi yake hadi kushinda tuzo kutoka African Entertainment Awards USA (AEAUSA) 2018.

“Asante Mwenyezi Mungu kwa hatua hii, asante Big Bro Diamond Platnumz kwa zawadi hii kwangu, Mwenyenzi Mungu apajaze pale ulipopunguza,” anasema Bajuni baada ya kupekea gari hilo.

Ikumbukwe Diamond ambaye anakadiriwa kuwa na utajiri wa Dola 10 milioni wastani wa Sh 23.3 bilioni anamiliki gari la kifahari aina ya Rolls-Royce Cullinan ambalo alisema alinununua kwa bei ya Sh 2.3 bilioni.

Pia ana magari mengine ya kifahari kama Toyota Land Cruiser V8 na Cadillac Escalade Sky Captain.