Kate, mrembo aliyeibeba huzuni ya Rio Ferdinand
Muktasari:
- Umaarufu wa Kate ulianza alipohusishwa kimapenzi na Dan Edgar, mmoja wa washiriki wa TOWIE, kabla ya yeye mwenyewe kujiunga na kipindi hicho mwaka 2015.
JINA la Kate Wright lilijulikana kupitia kipindi cha televisheni cha The Only Way Is Essex (TOWIE), lakini maisha yake yalibadilika kabisa alipokutana na aliyekuwa mchezaji wa England na Manchester United, Rio Ferdinand.
Umaarufu wa Kate ulianza alipohusishwa kimapenzi na Dan Edgar, mmoja wa washiriki wa TOWIE, kabla ya yeye mwenyewe kujiunga na kipindi hicho mwaka 2015.
Hata hivyo, Kate hakutarajia siku moja angejikuta katika jukumu kubwa la kuwa mama wa kambo wa watoto watatu waliokuwa wamepitia maumivu makubwa ya kumpoteza mama yao mzazi.
Hadithi inaanza pale Kate na Rio walipokutana Dubai mnamo 2017, wakati huo Rio alikuwa bado akijaribu kujenga upya maisha yake baada ya kumpoteza mke wake wa kwanza, Rebecca Ellison, aliyefariki mwaka 2015 kutokana na saratani ya matiti akiwa na umri wa miaka 34.
Rebecca na Rio walikuwa wanandoa waliokuwa wamejenga familia yao kwa upendo na walijaliwa kupata watoto watatu: Lorenz (2006), Tate (2008) na Tia (2011).
Kifo cha Rebecca kilimwacha Rio akiwa baba mlezi, akiwalea watoto hao huku akiwa bado na majukumu yake ya uwanjani.
Mwaka 2017, Rio kupitia BBC alitoa documentary iliyozungumzia maisha yake kama baba anayelea watoto peke yake kufuatia kifo cha mkewe.
Inaelezwa ilitazamwa na zaidi ya watu milioni 7 na kugusa hisia za wengi.
“Nilikuwa nimevunjika moyo kabisa. Nilihisi kama nisingeweza kutoka katika hali ile ngumu. Kisha nikakutana na Kate na kila kitu kikabadilika,” alieleza Rio.
Kwa upande wake, Kate alisema alipoanza uhusiano na Rio alikuwa na umri wa miaka 27 tu, hivyo hakujua ukubwa wa changamoto iliyomsubiri ya kuwa mama wa kambo.
“Mama yangu alidhani nimechanganyikiwa,” alisema Kate akielezea jinsi familia yake ilivyoshangazwa na uamuzi wake wa kuingia kwenye uhusiano na mwanamume aliyekuwa na watoto watatu na mkubwa kwake kwa miaka 12.
“Nilipoingia katika familia hii nilifikiri mambo yangekuwa rahisi, lakini ukweli ni yanahitaji kazi kubwa sana,” alisema na kuongeza:
“Nilikuwa nimezoea kujijali mwenyewe tu, sikuwa napika mara zote, mara nyingi nilikula migahawani au nyumbani kwa mama yangu. Ghafla nikawa nawalea watoto watatu waliokuwa na mahitaji yao mbele ya yangu. Hilo lilikuwa jambo jipya kabisa kwangu,” alisema Kate.
Licha ya upendo huo, baadhi ya mashabiki walimchukulia Kate kama mtu ambaye hakustahili kuwa na Rio kutokana na historia yake katika TOWIE, huku wengine wakimkosoa Rio kwa madai ya kuharakisha kuingia kwenye uhusiano mpya baada ya kifo cha mkewe.
“Unapoona watu wakisema, ‘amesonga mbele haraka sana,’ unafikiria, sawa, lakini natumaini hawatapitia hali kama hii maishani mwao,” alisema Rio akielezea jinsi alivyoguswa na maoni hayo.
Hata hivyo, Kate alikuwa na mtazamo tofauti, akisema alielewa kwa nini baadhi ya watu walikuwa na mashaka kuhusu uhusiano wao.
“Watu walikuwa na haki ya kunihukumu. Unapoona mtu mgeni anaingia katika familia kama hii, ni kawaida kujiuliza kama atakuwa mfano mzuri kwa watoto,” alisema.
Wakati yote yakiendelea, Kate alibaki na mtazamo chanya; badala ya kujibu wakosoaji kwa maneno, aliamua kuthibitisha kwa vitendo kwa kujenga uhusiano wa karibu na watoto wa Rio.
Hatimaye, wawili hao walifunga ndoa nchini Uturuki Septemba 27, 2019, huku watoto wa Rio wakiwa sehemu ya sherehe hiyo na binti yake Tia alipewa jukumu maalum la kuongoza msafara wa maharusi.
Mwaka 2020, wanandoa hao walitangaza wanatarajia mtoto wao wa kwanza pamoja. Hadi sasa Kate na Rio wamepata watoto wawili: Cree (2020) na Shae (2023), hivyo kumfanya Rio kuwa na jumla ya watoto watano.
Tangu aingie katika maisha ya ndoa na familia, Kate amepunguza kuonekana kwenye vyombo vya habari na kujikita zaidi katika kazi ya ushawishi wa chapa kupitia mitandao ya kijamii (influencer).
“Nilikuwa na machaguo mawili; niendelee kuishi katika ulimwengu uliojaa drama au maisha ya sasa. Nilipokutana na Rio na watoto wake nilijua kwamba watoto hawa waliompoteza mama yao walihitaji mtu wa kuwa karibu nao nyumbani, si mtu anayekuwa nje muda wote,” alisema.
Hadi sasa Kate ana wafuasi zaidi ya milioni 1.4 kwenye Instagram, ambapo mara nyingi hushare matukio ya familia yake.
Ingawa Kate aliingia katika maisha ambayo hakuyatarajia akiwa na umri wa miaka 27, ni wazi ameweza kujenga familia imara, huku safari yake ikionyesha kwamba familia yenye mzazi wa kambo inaweza kufanikiwa licha ya changamoto zinazoweza kujitokeza.