Jennifer Lopez: ‘Single mother’ wa viwango
Muktasari:
- Jennifer Lopez, mkali wa kibao cha On The Floor (2011), na filamu kama Kiss of the Spider Woman (2025), kwa miaka mingi amewalea watoto wake akiwa kama single mother baada ya kuachana na baba yao tangu mwaka 2014.
MBALI na shughuli zake katika muziki na filamu, tukija upande wa familia Jennifer Lopez (J.Lo), 56, ni mama wa watoto pacha, Max na Oskar, zamani Emme, ambao kupitia wao tunapata kuona upande wa pili wa staa huyo.
Jennifer Lopez, mkali wa kibao cha On The Floor (2011), na filamu kama Kiss of the Spider Woman (2025), kwa miaka mingi amewalea watoto wake akiwa kama single mother baada ya kuachana na baba yao tangu mwaka 2014.
Ijumaa iliyopita, Lopez alijikuta akibubujikwa na machozi wakati wa mahafali ya mtoto wake, Max, 18, ambaye amehitimu masomo yake ya sekondari. Mwimbaji huyo alionekana akifuta machozi katika picha zilizochapishwa na Page Six.
Katika hafla hiyo, Lopez aliambatana na wazazi wake Guadalupe Rodriguez na David Lopez, meneja wake Benny Medina, pamoja na pacha wa Max, Emme ambaye anaripotiwa kubadili jina na sasa anafahamika kama Oskar.
Ikumbukwe Lopez alijaliwa pacha hao hapo Februari 22, 2008, wakati huo bado alikuwa katika ndoa na mwanamuziki mwenzake, Marc Anthony ambaye uhusiano wao ulianza mwishoni mwa miaka ya 1990.
Mastaa hao walifunga ndoa Juni 5, 2004, na kutangaza kutengana Aprili 9, 2012 ingawa shauri la talaka yao lilikamilishwa Juni 16, 2014, huku Lopez akihifadhi haki ya msingi ya kuwalea watoto, kwa mujibu wa mahakama. Hata hivyo, Marc Anthony hakuhudhuria mahafali hayo ya kijana wake Max na hata yale ya Oskar yaliyofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita.
Katika mahafali ya Oskar, Lopez alihudhuria akiwa ameongozana na mama yake mzazi, Guadalupe Rodriguez, Max na Samuel Affleck ambaye ni mtoto wa mume wake wa zamani Ben Affleck. Utakumbuka Lopez na Ben Affleck ambaye walifunga ndoa mwaka 2022, licha ya kuachana kwao mnano 2024, wameendelea kuwa na uhusiano mzuri kama familia hasa upande wa watoto wao.
Affleck ana watoto watatu ambao ni Violet, 19, Seraphina, 16, na Samuel, 12, aliowapata katika ndoa na mkewe wa zamani, Jennifer Garner.
Lopez na Affleck ambao waliocheza pamoja filamu kama Gigli (2003) na Jersey Girl (2004), awali walikuwa na uhusiano kati ya mwaka 2002 hadi 2004, walipoachana na ndipo Lopez akaenda kufunga ndoa na Marc Anthony kisha kupata mapacha hao.
Akizungumza katika kipindi cha Jimmy Kimmel Live! siku mmoja kabla ya mahafali ya Oskar, Lopez alisema lengo lake kubwa kwa sasa ni kuwaona watoto wake wakiwa na furaha na kufuata njia wanazotaka wao maishani.
“Kikubwa nataka wawe na furaha, waende wanapotaka kwenda na wafanye wanachotaka kufanya,” alisema.
Kabla watoto hao hawajaondoka kwenda kuanza maisha yao mapya chuoni, Lopez katika kipindi cha Watch What Happens Live with Andy Cohen alieleza jinsi alivyowalea bila kuwaharibu kwa kuwapa kila kitu.
“Kwa kweli, watoto hufanya wanachokuona ukifanya, si suala la kuwaambia mambo kila wakati. Ingawa kwa sasa ninajaribu kuwapa kila somo na kila funzo nililojifunza maishani kabla hawajaondoka kwenda chuo mwezi Agosti,” alisema.
Katika mahojiano hayo yaliyorushwa Juni 8, Lopez alisema kuwa watoto wake hawataki kuwa kama yeye, bali wanataka kujijengea njia yao wenyewe katika maisha kwa kufuata kile wanachopenda.
“Wanaona hadhi ya umaarufu wangu kama kitu cha tofauti kabisa, lakini pia ninawaona wakichukua baadhi ya sifa na maadili mazuri kutoka kwangu, hata kama hawaniigi moja kwa moja,” alisema.
Katika hatua nyingine alizungumzia jinsi watoto wake wanavyojiandaa kwenda chuo, jambo ambalo limemfanya kuwa na mawazo kiasi akifiria kuanza maisha mapya ya nyumbani bila kuwa na watoto. “Watu wamekuwa wakija na kuondoka katika maisha yangu, lakini sisi watatu kila wakati tumekuwa tukibaki pamoja. Wao wamekuwa hapo kwa muda wote, na mimi pia nimekuwa hapo kwa ajili yao kila wakati,” alieleza.
Hata hivyo, alisema anawashukuru watu waliomzunguka kwa msaada ambao ulimwezesha kutimiza majukumu yake ya malezi pamoja na kazi zake za sanaa. Kwa sasa Lopez anachukuliwa kuwa mmoja wa wasanii wenye ushawishi mkubwa na waliochangia kukuza muziki wa Latin Pop, na pia alisaidia kuvunja vikwazo vilivyowakabili Wamarekani wenye asili ya Kihispania katika soko la Hollywood.
Ikumbukwe baada ya kupata umaarufu kupitia filamu kadhaa ikiwemo Anaconda (1997), ndipo Jennifer Lopez akageukia muziki akitoa albamu, On the 6 (1999) iliyokuwa na wimbo (If You Had My Love) ulioshika nafasi ya kwanza chati ya Billboard Hot 100.