Kaka aeleza kilichosababisha kifo cha Waziri Sonyo

Wednesday February 24 2021
sonyo pic
By Nasra Abdallah

Sanit Sonyo ambaye ni kaka wa mwanamuziki Waziri Sonyo, ameeleza kilichosababisha kifo cha msanii huyo kuwa ni ugonjwa wa moyo na shinikizo la damu.
Sonyo aliyewahi kufanya kazi katika bendi mbalimbali ikiwemo Tanzania One Theatre, Tamtam na Chuchu Sound, alifariki jana Jumatano Februari 23,2021 huko kwao Kibaha, mkoani Pwani.
Akizungumza chanzo cha kifo cha Sonyo, kaka yake huyo alisema kimetokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu na moyo kwa muda mrefu ambapo alikuwa akiishi kwa kutumia dawa.
“Ndugu yetu amefikwa na umauti kutokana na ugonjwa wa shinikizo la damu na moyo , magonjwa yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda sasa ambapo jana baada ya kutoka kutazama mpira wa simba na Al Ahly kupitia runinga maeneo ya jirani na nyumba ndio akafikwa na mauti majira ya saa 2:30 usiku wakati anataka kuingia ndani.
“Sonyo alitoka kuangalia mpira na nilizungumza naye kipindi cha mapumziko cha mechi hiyo, lakini alipofika tu mlango wa nyumbani alijisikia vibaya na kuanguka chini.
“Baada ya tukio hilo aliwaomba wadogo zangu wampatie dawa zake, na wakati dada yetu mmoja anaenda kumchukulia alivyorudi ndio akamkuta kalala moja kwa moja na kutonyanyuka tena,” alisema Sanit.
Alisema baadaye waliamua kuuepeleka mwili wa msanii huyo kwenda kuihifadhi hospitali ya Tumbi na anatarajiwa kuzikwa jioni hii katika makaburi ya Air Msae wilayani humo Kibaha.
Waziri sonyo atakumbukwa kwa namna alivyoweza kuchezea sauti yake na moja ya kibao ambacho aliwahi kukitunga na kuwika ni ‘Masimango’ akiwa TOT na mpaka anafariki alikuwa akifanya kazi na bendi ya Kiteshe yenye makazi yake Kibaha Maili moja.

Advertisement