Joti ajitabiria ushindi Zikomo Africa

Joti ajitabiria ushindi Zikomo Africa

Msanii wa vichekesho, Lucas Mhavile 'Joti' amejitabiria ushindi wa mapema katika tuzo za Zikomo Afrika.
Tuzo hizo zinazotarajiwa kutolewa Oktoba 15, 2022 jijini Lusaka nchini Zambia zimelenga kutambua watu mbalimbali walio katika kazi za  sanaa, masuaa ya haki za binadamu na ujasiriamali.
Joti ameyazungumza hayo katika mkutano ulioandaliwa na Bodi ya filamu kwa ajili ya kuwapongeza wasanii  walioteuliwa katika tuzo hizo.
Joti amesema katika kinyang'anyiro hicho anashindanishwa katika kipengele cha mchekeshaji bora nchi za Afrika Mashariki na Kusini na anaona hakuna mpinzani wake.
"Mpaka sasa najiona ni mshindi katika tuzo hizo, kikubwa watu waendelee kupiga kura ili nirudi na ushindi wa kishindo," amesema Joti mwenye kipaji cha kuvaa uhusika wa babu,mtoto,kijana na mdada.
Emmanuel Ndumukwa, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Filamu kutoka bodi ya filamu alisema kitendo cha wasanii zaidi ya 23 wa filamu kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho ni wazi kuwa tasnia ya filamu nchini inakuwa na inafutiliwa na nchi mbalimbali.
Kutokana na hatua hiyo aliomba Watanzania  kuwapigia kura wasanii hao kwa kuwa wakishinda ni nchi nzima itakuwa imeshinda na pia ni moja ya njia ya kukuza sanaa hiyo.
Akielezea hali ilivyo katika mchuano huo, alisema ushindani unaonekana mkubwa katika nchi ya Namibia, Afrika Kusini na Tanzania.
Balozi wa tuzo za Zikomo, Kulwa Mkwandule aliiomba serikali kuangalia namna ya kuwawezesha wasanii kwenda Zambia kushiriki fainali za utoaji tuzo hizo kwa kuwa kuna gharama mbalimbali ikiwemo nauli na malazi.
Wasanii wengine wa filamu waliotajwa kwenye tuzo hizo ni Lulu Diva, Romy Jones, Mariam Robert, Masai Nyota, Hakika Reuben, Katarina wa Karatu na wengine.