Hawa hapa wakali Bongo kwa kuimba na michano
MUZIKI ni sanaa yenye kuhitaji ufundi na ubunifu wa hali ya juu katika uwasilishaji wake, tena katika kipindi hiki ambacho muziki wa Bongofleva umekuwa na wasanii ni wengi, lazima kuzingatia vitu hivyo kama unahitaji kuendena soko lake.
Wapo baadhi ya wasanii ambao wamelitambua hilo na kuamua kulifanyia kazi na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kufahamu nini mashabiki wao wanahitaji, hapa uwezo binafsi unahitajika na sio kila mmoja anaweza.
Makala haya yanakuletea wasanii watano kutoka kwenyeBongofleva wenye uwezo mzuri wa kuimba na kurap kitu kinachopelekea kuendelea kushikilia mashabiki wa pande zote mbili;
G NAKO
Warawara, The Kankara, The Finest of AR, anafanya vizuri tangu akiwa na kundi la Nako 2 Nako Soldiers hadi sasa Weusi, kipindi yupo Nako 2 Nako alisikika sana akirap ukilinganisha na sasa ambapo amebadilika kidogo.
Kuna baadhi ya ngoma zake aliwashirikisha wasanii wa kuimba na yeye akisimama kama msanii wa Rap, ngoma hizo ni kama; Right Here,Oh Oh akiwa na Baby J, Bado Ngware akiwa na Peter Msechu, Mama Yeyoo akiwa na Ben Pol n.k.
Kuna ngoma alizorap na kuimba kwa wakati mmoja, nazo ni Chizika remix ya FBG (Fly But Ghetto), Bado Muda Kidogo akiwa na Chindo Man na JCB, Gere ya Weusi, Tumewaka na Godzilla, Show Love ya Nako 2 Nako, Wapoloo ya Weusi n.k.
Achilia mbali kazi alizofanya na Weusi, kwa sasa mara nyingi anasikika akiimba na amekuwa akishirikishwa na wasanii wengi ili akawaimbie 'chorus' amefanya hiyo kwenye ngoma ya Mfalme ya Mwana FA, Mtaa kwa Mtaa ya Country Boy, Shem Lake ya Izzo Bizness, Sana ya Stereo n.k. Na pia kuna ngoma alizoshirikishwa ili arap tu, nazo ni Make Up ya Rama D, Tudumishe ya Damian Sol n.k.
QUICK ROCKA
Hakuna asiyejua uwezo wake wa kurap, tena ile miondoka ya 'tantwista' ambayo ndio ilimtoa kimuziki, ingawa alionekana kuwa ana uwezo wa kuimba ili hilo kwa wakati huo hakulipa nafasi kubwa kama sasa.
Wakati yupo chini ya usimamizi wa MJ Records ngoma zake nyingi aliwashirikisha wasanii wa kuimba, ngoma kama vile Bullet alifanya na Makamua, My Life akampa shavu Marco Chali, 255 akimshirikisha Belle 9 na Tutoke aliyofanya na Shaa.
Sasa amebadisha kabisa muziki wake, anajita 'Switcher Baba', amejikita sana kwenye muziki wa kuimba, ameshafanya 'chorus' ya nyimbo kadhaa na nazikafanya vizuri, utaikumbuka Ball Player ya Izzo Bizness, Jana Na Leo ya Young Killer na Stamina n.k.
Pia ameshawahi kushirikishwa na wasanii wa kuimba ili aingize michano katika ngoma zao, utakumbuka ngoma kama Kisa Pombe ya Mwasiti na Nipe Love ya Ray C.
Nyimbo zake binafsi za kuimba ambazo zimefanya vizuri ni kama vile Teamo, My Baby,You My, Nakupenda, Tosamaganga, pia ana uwezo kurudia nyimbo (cover) za wasanii wenzake na kuzitendea haki, ameshafanya hivyo kwenye ngoma kama Sophia ya Ben Pol na Love Yourself ya Justin Bieber.
MR. BLUE
Wakati anatoka kimuziki alisikika sana akiimba ukilinganisha na sasa ambapo amejichimbia kwenye Rap, mwenyewe anaeleza Rap ndio mchezo anaupenda zaidi kwa sasa.
Blue wa ngoma ya Mapozi ni tofauti na yule wa ngoma ya Blue Blue, na hata sasa anafanya hivyo, Mr Blue wa ngoma ya Tilalila hafanani na yule wa ngoma ya Pesa au Pombe na Muziki.
Amekuwa na uwezo mkubwa sana wa kuchanganya ladha katika muziki wake, na hii ni toka kitambo anafanya hivyo, leo anaimba kesho anarap, kwenye nyimbo zake binafsi hilo kinaonekana kwa sana.
Ameshawahi kushirikishwa na wasanii wa kuimba ili aingize michano kwenye ngoma zao, ameshafanya kazi na Lady Jaydee - Wangu, K Lynn - Nipe Mkono, Belle 9 - Wewe Ni Wangu, Diamond Platnumz - Nakupa Moyo Wangu, Hemed Phd-Someday n.k.
Kwa sasa anatamba na sauti moja ya kibabe sana ambayo amekuwa akiitumia kwenye ngoma zake na kundi lake la B.O.B kitu ambacho kimefanya kuwa mpya na kupata kushirikishwa na wasanii wengi.
Hilo utaliona kwenye baadhi ya ngoma alizoshirikishwa na wasanii wa kurap, tazama ngoma kama Mlete ya Stosh, Panga Pangua ya Stamina, Kumekucha ya Young Killer, Naogopa ya Lulu Diva au wimbo wake, Mautundu.
A.Y
Toka kitambo anafanya vizuri, siri kubwa ya mafanikio yake anasema ni kubadilika kadri muziki unavyobadilika, ana uwezo wa kuimba na kurap toka anaanza muziki, ukisikiliza ngoma yake kama Nipe Nikupe aliyofanya na Prezzo na Leo utagundua hilo.
Ukiskiliza ngoma zake kama Mikono Juu, El Capo, Jipe Shavu, Money, Good Look na nyinginezo utatambua uwezo wake mkubwa wa kurap.
Pia ana uwezo wa kuchanganya vyote kwa wakati mmoja, sikiliza nyimbo zake kama Party Zone, Dakika Moja, Zigo, Dan'Hela na Freez aliyofanya na P Square, utabaini hilo.
Ikumbukwe A.Y ni mmoja kati ya wasanii wa mwanzo kuanza kuutangaza muziki wa Bongofleva nje ya mipaka ya Tanzania kwa kufanya kazi na wasanii wa Kenya kama vile Prezzo, Amani, Jagwa, Avil na Sauti Sol na pia wa Uganda kama vile Maurice Kirya.
Wasanii wengine wenye uwezo huo ni Marehemu Ngwea, sikiliza nyimbo zake kama Mikasi na She Got A Gwan utaona kulikuwa na watu wawili ndani yake. Pia Marehemu Godzilla aliweza hilo, sikiliza ngoma kama Thanks God na Nataka, utabaini kulikuwa na vitu viwili ndani yake pia.