Harmonize, Nandy kutumbuiza Mapinduzi Cup

Wasanii wa muziki wa kizazi kipya Nandy na Harmonize wanatarajia kutoa burudani kwenye fainaliza za Kombe la Mapinduzi zinazotarajia kufanyika Januari 13 mwaka huu.
Fainali hizo zitafanyika kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja, Zanzibar.
Mashindano hayo kwasasa yapo hatua ya makundi ambapo zimebaki mechi mbili pekee kukamilisha hatua hiyo ili kuingia hatua ya nusu fainali.
Yanga ambayo ipo kundi A imetinga hatua ya nusu fainali inasubiri mshindi wa Kundi C ambalo mechi ya kuamua itachezwa kesho Jumapili kati ya Azam FC na Malindi.
Timu hizo mbili zimecheza mechi moja kila moja huku zikiwa na pointi moja moja kutokana na sare walizopata mechi zao za awali wakati Mlandenge yenyewe ina pointi mbili na imemaliza mechi zake zote.
Kundi B linahitimishwa usiku wa leo Jumamosi kwa kuzikutanisha Simba na Mtibwa Sugar timu zote zina pointi tatu kila moja kwani zilishinda mechi zao za awali.
Mechi hiyo ndiyo itakayoamua mchezo wa nusu fainali ambapo mshindi wa kundi hilo atacheza na best looser.
Best looser inategemea na mchezo huo kwa uwingi wa mabao kwani mpaka sasa Simba ana mabao matatu, Mtibwa ana bao moja huku Namungo wao wana bao mbili walizozipata kwenye mechi yao ya mwisho dhidi ya Jamhuri ambayo imetolewa mashindanoni.
Hivyo basi, kama Mtibwa Sugar atapoteza mechi hiyo nusu fainali itakuwa dhidi ya Simba na Namungo huku Yanga huenda wakacheza kati ya Azam FC au Malindi ambazo zinacheza kesho na zote zina pointi moja kila timu.