Harmonize hatoi tena kiki kwa Diamond
Muktasari:
- Baada ya kufanya kazi pamoja kwa takribani miaka mitano kwa mafanikio makubwa, ghafla ukaribu wao uligeuka kuwa uwanja wa lawama na fedheha katika mchakato wa Harmonize kuondoka WCB Wasafi.
NI kama Harmonize hataki tena, au amechoka kumuimba bosi wake wa zamani, Diamond Platnumz, katika nyimbo zake baada ya kufanya hivyo mara kadhaa kufuatia mgogoro mkubwa wa kibiashara ulioibuka mwaka 2019.
Baada ya kufanya kazi pamoja kwa takribani miaka mitano kwa mafanikio makubwa, ghafla ukaribu wao uligeuka kuwa uwanja wa lawama na fedheha katika mchakato wa Harmonize kuondoka WCB Wasafi.
Diamond ndiye aliyemtoa kimuziki Harmonize mwaka 2015 baada ya kumsaini katika lebo hiyo ya muziki, huku akiwa mwanamuziki wa kwanza kutambulishwa.
Chini ya WCB Wasafi, Harmonize alipata umaarufu kupitia nyimbo zake, hasa zile alizomshirikisha Diamond ambazo ni Bado (2016) na Kwangwaru (2018), ambao ndiyo wimbo wake pekee uliotazamwa zaidi ya mara milioni 100 kwenye YouTube.
Hata hivyo, katika mchakato wa kuachana na WCB Wasafi, uliibuka mgogoro mkubwa kati yake na Diamond ambao ulikuwa gumzo kubwa katika kiwanda cha muziki wa Bongo kwa wakati huo.
Baada ya kufanikiwa kuondoka WCB Wasafi, Harmonize alitoa nyimbo kadhaa akirusha vijembe kwa Diamond, lakini sasa ni kama ameamua kuachana na jambo hilo kwani mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa mwaka 2021.
Mojawapo wa sababu zinazoweza kuwa zimemfanya aache kufanya hivyo ni changamoto zilizokabili lebo yake ya Konde Music Worldwide, huku baadhi ya wasanii wakimlalamikia kwa mambo yanayofanana na yale aliyokuwa akimlalamikia Diamond.
Lakini ni lini na kwa namna gani Harmonize alirusha vijembe kwa Diamond kupitia nyimbo zake? Zifuatazo ni baadhi ya nyimbo zake ambazo alifanya hivyo kati ya mwaka 2019 na 2021.
Uno (2019)
Ulikuwa wimbo wake wa kwanza kuutoa tangu aachane na WCB Wasafi. Ulifanya vizuri sana, huku Harmonize akiwarusha vijembe Diamond pamoja na mzazi mwenziye, Zari The Boss Lady kutoka Uganda.
"Uno la Chibu Chibu linamkondesha Zari," aliimba Harmonize katika wimbo huo, licha ya wawili hao kuwa tayari walikuwa wameachana. Wakati huo, Diamond alikuwa katika uhusiano na Tanasha Donna kutoka Kenya.
Kushoto Kulia (2019)
Kupitia wimbo huu, Harmonize anamshukuru Diamond kama mmoja wa watu waliomleta mjini na kumpa nafasi, huku akitaka masuala ya ugomvi yasiingizwe katika muziki wao.
"Peace kwa walionileta mjini, Mondi wa Tandale. Maneno, majungu tupa chini, muziki utawale," aliimba Harmonize, ambaye katika video ya wimbo huo anaonekana kama mtumwa aliyevunja minyororo na kuondoka zake.
Ushamba (2020)
Ukiachana na wimbo wenyewe, pia video yake iliibua gumzo kufuatia Harmonize kumtumia kijana mwenye mwonekano unaofanana kwa kiasi kikubwa na Diamond.
"Halina meno hilo Simba Zee, likila demu lazima litangaze." Inajulikana kuwa Diamond amekuwa akitumia jina la Simba katika muziki wake. Ukiachana na kijana anayefanana naye katika video hiyo, ilitoa picha kamili kwamba kijembe hicho kilikuwa kikielekezwa kwake.
Usia (2021)
Ni ngoma inayopatikana kwenye albamu yake ya pili, High School, iliyotoka ikiwa na nyimbo 20. Humo pia alimrushia vijembe Diamond. Ikumbukwe kuwa nyimbo mbili zilizotangulia zipo kwenye albamu yake ya Afro East (2020).
"Simba na ukali wake wote, ila akimuona Tembo anachimba, ila hiyo haimfanyi Tembo kuvimba," anaimba Harmonize, ambaye amekuwa akitumia jina la Tembo katika muziki wake, huku akiwa amejichora tattoo ya mnyama huyo anayejulikana kwa nguvu zake kubwa.