Hapatoshi, huku Diamond, kule Harmonize

Friday November 27 2020
DIAMOND PIC

WASHINDANI wa muziki wa Bongo Fleva, Harmonize na Diamond Platnumz kesho wanatarajia kuwashushia burudani mashabiki zao.
Hii ni baada ya Wasafi kuwa na tamasha lao la ’Tunawasha’ wilayani Kahama mkoani Shinyanga, huku Harmonize akifanya tamasha lake la Ushamba mkoani Mtwara.

Tamasha la Ushamba awali lilikuwa lifanyike mkoani Dar es Salaam, lakini kutokana na sababu ambazo hazikuwekwa wazi na Harmonize liliahirishwa na kupelekwa mkoani Mtwara.

Kutokana na ratiba hiyo, Diamond atasindikiwa na wasanii mbalimbali Shinyanga na wakati huohuo mkoani Mtwara Harmonize atawapa raha mashabiki zake akisindikizwa na wasanii wa lebo yake ya Konde Gang.
Hili linajirudia kwa wasanii hao kutumbuiza siku moja kama ilivyotokea Desemba 31, ambapo Diamond alikuwa na tamasha la miaka kumi tangu alipoanza muziki lililofanyika mkoani Kigoma.

Katika tukio moja la kuvutia ilikuwa msanii huyo, wasanii wengine pamoja na ndugu jamaa na marafiki kusafiri kwenda na kurudi mkoani humo kwa kutumia usafiri wa treni.

Kwa upande wa Harmonize moja ya tukio lililovutia ilikuwa ni kushuka na winchi stejini.
Macho na masikio mwaka huu ni wasanii hao wataingia na staili gani katika kutumbuiza katika matamasha. Endelea kufuatilia hapa.

Advertisement