Hadithi
HADITHI: Zindiko (sehemu ya 4)

Muktasari:
- Huu ni mwendelezo wa hadithi ya kusisimua kutoka kwa mtunzi mahiri wa riwaya, SULTAN TAMBA. Twende naye....
Sikuvuka hata hatua mbili, kitu cha kushangaza kilitokea.
Joka kubwa na la ajabu lilitoka kwenye ule mtungi na kunijia kwa kasi. Kabla sijaweza kuamua chochote, lile joka likanizingira na kuniweka katikati. Halafu nilipoinua uso, ghafla – mbele yangu akasimama mtu anayefanana na mimi kwa kila kitu, ananitazama.
Yaani hilo jambo lilifanyika haraka sana kabla hata akili yangu haijakaa sawa, likawa tayari limeniweka kati. Maana kama lingekuwa ni joka la kujivutavuta hata kidogo tu, ningeweza kukimbia.
Lakini nikajikuta nimesimama, nikisikilizia ni nini kinachotaka kutokea nikiwa katika hali ya hofu na wasiwasi.
Kutoka kwenye mtungi, moshi mwingi mithili ya bomba ulitoka, kisha ukaja mbele yangu na kutoweka ghafla na kumwacha mtu amenisimamia.
Huyu mtu aliniduwaza. Si kwa ujio wake wa kuletwa na moshi, bali kwa wajihi wake. Alifanana na mimi kwa kila kitu.
Kwa lugha nyingine niseme huyu ni mimi niliyepigwa photocopy. Alinisimamia huku akiwa na tabasamu maalum. Tabasamu la kazi, tabasamu la kuonyesha kwamba, licha ya kwamba yeye ni photocopy yangu, lakini ni mtu mwingine! Ila, alivaa tofauti na mimi na alikuwa ameshika mkongojo. Alivaa maushanga kiunoni na kichwani.
Alinitisha.
Alikuwa amesimama mikono nyuma, akasimama kwa nidhamu mbele yangu. Joka likabadili mwelekeo na kutuzingira wote. Tukawa tupo katikati.
Ni wakati alipoanza kuzungumza, ndipo tabasamu lake lilipofutika.
Mtu huyu akatoa mkono wake mmoja kutoka nyuma, akanioneshea.
Kilikuwa ni aina ya tufe au kito kikubwa jekundu. Ukubwa wake ni kama yai la kuku (ila yale mayai ya kuku makubwa makubwa ya kizamani, sio haya ya kuku wenu wa siku hizi!). Akanyoosha mkono wake juu juu huku akifumba macho kwa hisia.
“Naapa kwa jiwe jekundu, lenye nguvu katika uhai na mali kwamba - Zindiko limekamilika.”
Akarudisha mikono nyuma, akanitazama.
Nami nikatulia kumtazama, nikitegemea kauli kutoka kwake.
Lakini nilichokihofia zaidi ni hukumu. Nilihisi kwa kufika pale, pengine nilikuwa nimevunja sheria maalum na ndiyo maana yote hayo yanaelekea kunifika. Sikuwa na ujanja wa aina yoyote pale. Hakukuwa na njia ya kutoroka wala kufanya lolote. Ndio kusema, milango ya kujinusuru ilikuwa imefungwa.
“Bwana Zimataa!” aliniita kwa jina langu. “Hongera kwa kuwa mtu wa kwanza kuja hapa. Umebahatika. Lakini pia inaweza kuwa kinyume chake.
Itategemea na utakavyokuwa mtiifu. Hiyo miguu yako kukanyaga hapa imekamilisha zindiko la kinga ya nyumba hii.
Nilimeza funda la mate kwa wasiwasi, nikamtazama msemaji huyu. Lakini hakuendelea. Ni kama aliacha tobo la mimi kujibu kitu. Nikajitafuta, ulimi wangu ukafanikiwa kuinuka kumjibu, “Mimi ni mtiifu. Ila... Naomba tu uniambie.. wewe ni nani... Manake naona tunafanana sana. Na kwa nini umekuja. Kama nimekosea niruhusu niondoke na sitakuja tena.”
Yule mtu akatabasamu.
“Hebu angalia hapo chini yako…”
Nikaangalia chini… Sikujua anamaanisha nini, maana sikuona chochote.” “Huna kivuli.. si ndio.”
Akanishtua.
Sasa nikaangalia tena chini – ni kweli, sikuona kivuli chochote. Nikainua sura na kumkubalia kwa kichwa.
“Mimi ndiye kivuli chako.” Nikakubali tena kwa kichwa.
“Sasa sikiliza kwa makini. Zindiko kubwa la siku tatu lililofanywa kwenye nyumba hii, lilikuwa linamsubiri mtu wa kwanza kufika hapa ili akabidhiwe majukumu yake. Mtu mwenyewe ni wewe. Kama hujui basi ndio nakwambia. Wewe ndiye mtu wa kwanza kukanyaga kwenye viunga hivi.”
Nilitumbua macho, nikisubiri kusikia anachotaka kusema
“Majukumu yako ni kutunza mazingira ya hapa. Inatakiwa uwe unakuja hapa kufanya usafi angalau kila wiki. Hiyo ni kwa sababu jengo hili litakuwa pweke kwa muda mrefu usiojulikana.”
Nikashangaa. Hofu ikapungua baada ya kuona kumbe sikuwa kwenye hatari. Nikawa na shauku ya kuuliza – lakini nilijizuia. Ni kama alikuwa anajua nilichotaka kumuuliza, akaendelea.
“Jengo hili halipangishwi, wala halitaishi mtu. Limejengwa hapa na watu maalum, kwa sababu maalum. Zindiko lililowekwa hapa litailinda nyumba hii kwa muda wowote utakaohitajika. Wewe ndio mtu pekee ambaye si mwana-familia ambaye amepata kibali cha kuingia hapa. Hakuna mtu mwingine ambaye zindiko litamwacha salama. Waonye wasije kusogea hapa. Watakufa.
“Haya. Nimeongea kwa niaba ya Joka la Zindiko, sasa zamu yako. Unaruhusiwa kuomba chochote iwe ndio malipo yako kutokana na jukumu ulilopewa.”
Akanionyesha tena jiwe jekundu.
“Jiwe jekundu litakupatia unachotaka.”
Nikalitumbulia macho jiwe hilo lenye wekundu wa ajabu unaometameta.
Akarudisha mikono nyuma. Akasubiri kunisikiliza.
Nikawa kwenye wasiwasi mwingi. Joka lilikuwa limetuzingira! Mtu huyu wa ajabu amenisimamia. Vipi nikitaka kusema kitu ambacho hatakikubali?
“Nasubiri useme. Ila usiwaze kukataa. Kwa sababu ukikataa hutatoka hapa salama, utamezwa na Joka la Zindiko. Mlinzi mtiifu unayemuona ametuzunguka. Kisha tutamsubiri mwingine aje apewe jukumu ulilokataa wewe.”
Nikageukageuka kuliangalia joka, lenyewe halikuwa likituangalia, liligeuzia kichwa chake upande mwingine. Kisha nikarudi kumtazama yeye.
“Mimi siwezi kukataa mheshimiwa. Na kama unanambia niseme kitu, basi nitasema - ila usinielewe vibaya. Mimi ni mtu masikini. Ninachokiomba kwenu, naomba niwezeshwe niwe napata kipato cha kulisha familia yangu kwa uhakika kila siku. Kwa sasa mimi ni mkulima, ila niwezesheni nipate kazi nyingine ya kuniongezea kipato. Hiyo itaniwezesha kutimiza jukumu mlilonipa kwa urahisi zaidi wakati wowote. Ni hilo tu.”
Baada ya kusema maneno hayo, nikatulia kusikiliza.
Yule mtu wakati nasema yote hayo alikuwa ameinamisha kichwa chini akinisikiliza kwa mtindo wa kunitii na mikono yake ikiwa nyuma muda wote.
Nilipomaliza akainua kichwa kuniangalia.
Halafu akatoa mikono yake nyuma. Mkono mmoja ulikuwa umeshika mtungi mdogo!
Aliuchukua wapi, sijui!
Amekuja kimiujiza, kwa hiyo kila anachokifanya kinaendana na jinsi alivyokuja. Ni mwendo wa miujiza!
Akanikabidhi.
Nikaupokea.
“Ombi lako limekubaliwa. Hicho kibuyu ni karama ya uganga. Kuanzia sasa utatibia watu kwa ugonjwa na shida zozote zile.”
Nikaendelea kumsikiliza na yeye akaendelea.
“Zindiko litakuletea wateja kutoka kila pembe. Kila mtu akija kufuata tiba, hata kama hujui dawa yake, msikilize na Zindiko litakujulisha dawa kupitia ndoto. Pia kupitia ndoto za usiku au ndoto fupi za mchana unaposinzia, zindiko litakuonyesha kila mtu atayekuja, ugonjwa wake na dawa pia.
“Lakini dawa utakayooteshwa haitafanya kazi dawa hiyo hadi uilete kwenye mtungi ule pale wa joka la zindiko ili zithibitishwe kwamba ndiyo zenyewe. Mlinzi wa zindiko atatoka na kukupa baraka zake. Usipofanya hivyo, dawa hizo hazitafanya kazi kwa sababu utakuwa umefanya kosa.
Nilitabasamu!
Hizi zilikuwa ni habari njema sana kwangu.
Kazi ya uganga nilikuwa naipenda japo nilikuwa sijui hata dawa moja. Huko nyuma, niliwahi kufanya kazi kwa Mzee Baingu, mganga maarufu kwenye mji wetu nilikokuwa naishi.
Kilichonipeleka kufanya kazi kwa Mzee Baingu, ilikuwa ni majukumu, nilipomuoa huyu mke niliyenaye na kupata mtoto wetu wa kwanza, maisha yalikuwa magumu sana. Nilikuwa naishi bila hata senti kwa hata wiki zaidi ya kuchuma mboga na kuomba chakula kwa wanandugu.
Itaendelea...