Ghetto Kids, Shakira wanajambo lao
Muktasari:
- Kundi hilo ambalo lilianza kwa kucheza dansi wakiwa peku kwenye vumbi Kampala nchini Uganda ni miongoni mwa vijana wachache wanaoenda kuandika historia kwenye Uwanja wa MetLife, New Jersey nchini Marekani.
NDOTO imekuwa kweli. Hayo ni maneno ya baadhi ya watoto kutoka katika kundi la dansi la Ghetto Kids lililopo Uganda ambapo siku chache zilizopita mwanamuziki maarufu Shakira alitangaza kucheza nao kwenye Halftime shoo ya Fainali za Kombe la Dunia Marekani.
Kundi hilo ambalo lilianza kwa kucheza dansi wakiwa peku kwenye vumbi Kampala nchini Uganda ni miongoni mwa vijana wachache wanaoenda kuandika historia kwenye Uwanja wa MetLife, New Jersey nchini Marekani.
Kutoka maisha ya umaskini katika mitaa ya Kampala hadi kutumbuiza na Shakira mmoja wa wanamuziki wenye ushawishi mkubwa duniani.
Habari hizo zimetikisa mitandao ya kijamii na Afrika kujivunia mafanikio ya watoto hao ambao wamepitia kwenye maisha magumu tangu wakiwa wadogo.
SAFARI YAO
Safari ya Ghetto Kids ilianza mwaka 2014 katika mitaa ya Kampala, mji mkuu wa Uganda. Wakiwa watoto wadogo waliotoka kwenye mazingira ya umaskini mkubwa, walitumia dansi kama njia ya kujiburudisha na kujikimu kimaisha.
Baadhi ya watoto wanaounda kundi hilo ni yatima au waliotoka kwenye familia maskini. Baadhi yao walikuwa hawaendi shule, hawakuwa na chakula cha kutosha wala mahitaji ya msingi ya maisha.
Meneja wa kundi hilo, Dauda Kavuma, ndiye aliyeanzisha taasisi hiyo inayowasaidia watoto hao kupata malezi, elimu na nafasi ya kukuza vipaji vyao.
Kavuma anasema lengo la taasisi hiyo lilikuwa kutumia sanaa kubadilisha maisha ya watoto wa mitaani na kuwapa matumaini mapya.
“Tunatumia muziki, dansi na maigizo kufanya maisha ya watoto hawa kuwa bora na kweli kupitia muziki na dansi, maisha yao yalianza kubadilika polepole,” amesema Kavuma.
Kundi hilo lilianza kupata umaarufu baada ya kufanya chalenji ya wimbo wa mwanamuziki wa Uganda, Eddy Kenzo 'Sistya Loss' ngoma iliyoachiawa miaka 11 iliyopita.
Watoto hao walifanya chalenji ya dansi na kuirejesha tena ngoma hiyo kwenye trend, wimbo huo ulisambaa kwa kasi kupitia Youtube na mitandao mingine ya kijamii.
Katika video hiyo, watoto hao walionekana wakifanya miondoko ya ajabu kwa furaha kubwa licha ya maisha magumu waliokuwa wanaishi. Dunia ilivutiwa na vipaji vyao, nguvu zao na tabasamu waliloonyesha.
Tangu wakati huo, Ghetto Kids waliendelea kukua na kuwa moja ya makundi maarufu zaidi ya dansi barani Afrika.
SHAKIRA AWAPA NGUVU
Wiki iliyopita mwanamuziki, Shakira, alitangaza kuwa Ghetto Kids wataungana naye katika onyesho la halftime Show ya fainali ya Kombe la Dunia.
Shakira amesema alitaka halftime hiyo iwe ya kipekee na isiyosahaulika, ndiyo maana akaamua kuwaalika watoto hao wenye vipaji vikubwa kutoka Afrika.
Watoto hao tayari wameonekana katika video ya wimbo wa 'Dai Dai' ambao ni wimbo rasmi wa mashindano ya Kombe la Dunia 2026.
“Tulifurahi sana tuliposikia habari hizo. Tuliruka juu na chini tukisherehekea,” amesema Ssegirinya Madwanah King mwenye umri wa miaka 15.
"Onyesho hilo lina maana kubwa kwa kundi letu, ambalo sasa ni kama familia moja kubwa iliyotoka pembezoni mwa jamii ya Uganda.
Kabla ya kujiunga na kundi, hatukuwa tunaenda shule, hatukusafiri, na hatukupata mahitaji ya msingi,” amesema Ssegirinya.
“Kama nisingekuwa sehemu ya kundi hili, sijui ningekuwa wapi leo.”
Tiyoma Keysha mwenye umri wa miaka 11 amesema:“Tuna furaha sana. Siwezi kusubiri kuuonyesha ulimwengu kile tunachoweza kufanya.”
KUTOKA UGANDA HADI MAREKANI
Ghetto Kids sasa wanajiandaa kusafiri kwenda Marekani kwa ajili ya maandalizi ya onyesho hilo kubwa litakalotazamwa na maelfu ya watu duniani.
Kundi hilo lina watoto zaidi ya 60 wenye umri kati ya miaka 4 hadi 16.Mbali na kucheza na Shakira, watoto hao pia watapata nafasi ya kuonyesha utamaduni, vipaji na nguvu ya vijana wa Afrika.
MUENDELEZO
Huu ni muendelezo tu wa kile walichowahi kukifanya kwenye mashindano ya America Got Talent mwaka 2024 wakionyesha vipaji mbalimbali vya kucheza.
Kundi hilo ambalo lilifika hadi fainali ingawa halikuchukua taji lilivutia majaji na watazamaji duniani kutokana na dansi zao wenye nguvu, ubunifu na burudani kabambe waliyoionyesha.
Mbali na sindano hilo kubwa watoto hao waliwahi kushiriki mashindano ya Britain Got Talent mwaka 2023 wakaishia hatua ya nusu fainali.
Pia waliwahi kuonekana kwenye video ya rapa wa Marekani, French Montana 'Unforgettable' mwaka 2017.
Kupitia mitandao ya kijamii, video zao zimeendelea kuvutia mamilioni ya watazamaji duniani kutokana na ubunifu wao na dansi zenye furaha.
CHANGAMOTO YA EBOLA
Hata hivyo, safari yao kuelekea Marekani bado inakabiliwa na changamoto kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Uganda na nchi jirani ya Congo.
Mamlaka za Uganda tayari zimeanza kuchukua tahadhari kali za kiafya ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Licha ya hali hiyo, meneja wa kundi hilo amesema wana matumaini kuwa kila kitu kitakuwa sawa na watafanikiwa kusafiri kwenda Marekani kwa ajili ya onyesho hilo kubwa.
“Tunaamini kila kitu kitakuwa sawa. Kwa neema ya Mungu hakuna lisilowezekana,” amesema Kavuma.
Kwa watoto waliotoka maisha ya mitaani, safari yao ni ushahidi kwamba vipaji vinaweza kubadilisha maisha.
Kutoka kucheza peku kwenye vumbi la Kampala hadi kucheza jukwaa moja na Shakira katika fainali ya Kombe la Dunia, Ghetto Kids sasa wamekuwa mfano wa matumaini kwa baadhi ya watoto wa Afrika.
Mafanikio yao yanaonyesha kuwa kupitia kazi ngumu, nidhamu na msaada, hata watoto waliotoka mazingira magumu wanaweza kufikia ndoto kubwa duniani.