Shakira amtoa Messi pangoni
Muktasari:
- Shakira, kwa kushirikiana na msanii maarufu wa Nigeria, Burna Boy, walipewa jukumu la kutengeneza wimbo rasmi wa mashindano hayo uitwao “Dai Dai”, ambao tayari umesambaa kwa kasi mitandaoni, hasa kutokana na tukio la kushangaza lililomhusisha Lionel Messi.
MIAMI, MAREKANI: Dunia ya muziki na soka zimeungana tena kuandaa mazingira ya Kombe la Dunia Fifa 2026 litakayofanyika Marekani, Mexico na Canada kuanzia Juni 11 hadi Julai 19.
Shakira, kwa kushirikiana na msanii maarufu wa Nigeria, Burna Boy, walipewa jukumu la kutengeneza wimbo rasmi wa mashindano hayo uitwao “Dai Dai”, ambao tayari umesambaa kwa kasi mitandaoni, hasa kutokana na tukio la kushangaza lililomhusisha Lionel Messi.
SHAKIRA AMEFANIKISHA LISILOWEZEKANA KWA MESSI
Msanii huyo wa Colombia ameandika historia tena baada ya mafanikio ya nyimbo zake za Kombe la Dunia kama “La La La” ya mwaka 2014 nchini Brazil na “Waka Waka (This Time for Africa)” ya mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
Mnamo Mei 23, Shakira aliachia rasmi video ya wimbo wa 2026, na mashabiki walijaa mtandaoni kuizungumzia.
Kilichovutia zaidi ni tukio lisilotarajiwa mwanzoni mwa video: Messi akizungumza kwa Kiingereza.
Video inaanza na Kylian Mbappé akisema “Shakira, we are ready,” akifuatiwa na mastaa wengine kama:
Harry Kane, Luis Díaz, Christian Pulisic, Santiago Giménez,
Alphonso Davies,Vinícius Júnior,Takefusa Kubo, Jamal Musiala,Rodri na Erling Haaland. Wote wakisema: “We are ready.”
Lakini kilichowashangaza wengi zaidi ni pale nahodha wa Argentina, Messi, naye alipotamka maneno hayo kwa Kiingereza.
Hii iliwashangaza mashabiki wake kwa sababu katika maisha yake yote ya soka, Messi amekuwa akiepuka kuzungumza hadharani kwa lugha nyingine isipokuwa Kihispania.
MITANDAO YA KIJAMII YALIPUKA
Hii si mara ya kwanza Messi kuonekana kwenye kazi ya Shakira; aliwahi kushiriki pia katika video za “La La La” na “Waka Waka.”
Lakini safari hii, mashabiki walifurika mitandaoni kwa utani na mshangao, wakisema: “Shakira ndiye mtu wa kwanza katika historia kumfanya Messi azungumze Kiingereza. Ni icon wa kweli.”
“Messi kuongea Kiingereza kabla ya Grand Theft Auto VI kutoka!”
Wengi wameona tukio hilo kama moja ya nyakati za kushangaza zaidi kuelekea Kombe la Dunia la 2026.