Gadner afariki dunia, wasanii wamlilia

Muktasari:

  • Kufuatia taarifa ya kifo cha mtangazaji huyo watu mbalimbali wakiwemo wasanii na watu wanaomfahamu wametuma salamu za rambirambi kwa familia kupitia mitandao ya kijamii.

MTANGAZAJI maarufu wa kituo cha Clouds FM, Gadner G. Habash amefariki dunia leo saa 11:00 asubuhi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Taarifa za kifo cha mtangazaji huyo zilianza kusambaa asubuhi hii, kabla ya kuthibitishwa na kituo hicho cha redio.
“Ni kweli kwa taarifa za awali amefariki (dunia), lakini nitatoa taarifa zaidi baadaye,” amesema Emilian Malya, msemaji wa Clouds Media Group.

Kufuatia taarifa ya kifo cha mtangazaji huyo watu mbalimbali wakiwemo wasanii na watu wanaomfahamu wametuma salamu za rambirambi kwa familia kupitia mitandao ya kijamii.

Aliyewahi kuwa mfanyakazi mwenzake Zamaradi Mketema kupitia mtandao wake wa Instagram ameandika: “Aaah Gadna jamani!!! Inalillahi waina ilaihi rajiun!!! MUNGU akupumzishe kwa amani kaka, Dah!!! Gadna, pumzika kwa amani kaka!!! Kazi ya MUNGU haina makossa.”

Naye msanii wa Bongofleva, Peter Msechu kupitia Instagram amendika: “Daaaah aiseee😭😭😭😭💔💔💔💔 Pumzika Brother Gadner.”

Mwingine ni mwingizaji wa Bongo Movie, Steve Nyerere ambaye naye kupitia mtandao huo wa Instagram ameandika: "Mstafuuuuu. HAPA Duniani tunapita na barabara tunayo pita ni wote tutapita hiyo hiyo bahati nzuri njia tunayopita kila mmoja ana muda wake wa kupita lakini atapita tu.

“Katika ukurasa huo ameendelea kuandika kuwa maskini atapita aajiri atapita mh atapita chizi atapita, lakini tumepishana saa tu."

Steve ameandika kuwa Mungu kaweka siri kubwa kwenye kifo na ndiyo maana mpaka leo tumekuwa watu wa kusema Mungu nisaidie kifo chema.

“Kaka lala, tutaonana baadaye. Ni ngumu kuamini, lakini kwa mapenzi ya Mungu kila jambo linawezekana...” amehitimisha andiko lake.

Msanii Dulla Makabila kupitia Instagram yake aliandika “REST IN PEACE BROTHER GADNER 😭😭😭😭😭😭😭. Mungu aitie nguvu familia ndugu jamaa na mrafiki kwenye kipindi hiki kigumu."

Naye Kijekitile Ngombare maarufu Kinje mtoto wa Hayati Kingunge Ngombare Mwiru, kupitia mtandao wake wa Instagram ameandika: "Rest in peace mdogo wangu juzi nimekuja kukuona nikakuambia nitakuja kukuona tena, daah pumzika kwa amani mdogo wangu.”

Wakati wa uhai wake, mtangazaji huyo aliwahi kuwa katika uhusiano wa muda mrefu na mwanamuziki Judith Wambura 'Lady JD' ambapo pia muda mwingi walikuwa pamoja katika shughuli zake za muziki na ndiye alifahamika kama meneja wake.

Hata hivyo, miaka michache iliyopita waliachana na kila mmoja kuendelea na maisha yake, huku mara moja moja Gadner katika siku za karibuni akionekana kuwa karibu na binti yake Karen ambaye pia ni mwanamuziki wa Bongofleva. 

Gadner alijipatia umaarufu kupitia kipindi cha Jahazi cha Clouds FM katikati ya miaka ya 2000 wakati huo akishirikiana na Ephraim Kibonde ambaye pia sasa ni marehemu na Paul James maarufu PJ ambapo kipindi hicho kilikuwa kikirushwa hewani kuanzia saa 10 jioni hadi saa 12 jioni.