Ferre Gola atua Bongo, amtaja Diamond Platnumz

Thursday December 23 2021
fere pic
By Nasra Abdallah

Mwanamuziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo, Ferre Gola ametua nchini Tanzania kwa ajili ya kupamba mashindano ya kumsaka mrembo wa East Africa.
Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika Desemba 24, 2021 katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam ambapo washiriki kutoka nchi 14 watapanda jukwaani kushiriki.
Ferre Gola ametua leo Alhamisi Desemba 23, 2021 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere na kupokewa na wenyeji wake kampuni ya Rena  International ambao ndio waandaji wa mashindano hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari waliokuwepo uwanjani hapo, Ferre Gola aliyetingisha na vibao mbalimbali ikiwemo 100 kg, Pyromane, Vita Imana, Maboko Pamba, Kinshasa na nyingine nyingi, aliahidi kushusha show ya kufa mtu na kuwataka watu kutokubali kuikosa.
“Nimejiandaa vilivyo kuwapa watu wangu burudani, hivyo watu wanatakiwa wasikose siku hiyo ya Jumamosi kwa kuwa nitawaambia nyimbo zao pendwa zikiwemo mpya ambazo hazijawahi kusikika kokote,” amesema mwanamuziki huyo.
Akizungumzia kuhusu wasanii wa Tanzania anaowapenda, alisema wapo wengi akiwemo Diamond Platnumz, lakini kwa ujumla wengi alisema wanafanya vizuri na kubainisha kuwa yupo tayari kufanya nao kazi watakapomuhitaji.
Katika mashindano hayo mbali na Ferre Gola, mwingine atakayetumbuiza ni msanii wa Bongo Fleva nchini Tanzania, Yusufu Mbwana  maarufu kwa jina la 'Mbosso'.
Warembo hao kutoka nchi 14 watakaochuana usiku huoni  kutoka nchi ya Moritius, Sudani ya Kusini,Djbout, Elitrea, Shelisheli,Comoro, na Uganda. Nchi nyingine ni Kenya,Uganda,Malawi,Somalia,Ethiopia,Burundi,Ruanda,Malawi na wenyeji Tanzania.

Mshindi katika mashindano hayo anatarajiwa kuondoka na gari aina ya Nissan Xtrail  na mshahara wa mwezi mmoja wa dola 1500, wakati mshindi wa  pili ataondoka na na kitita cha  dola 5000 huku mshindi wa tatu atapata dola 2000.

Advertisement