Extra bongo kurudi kivingine, baada ya kupotea miaka  tisa

Muktasari:

  • "Unajua bendi huwa hazifi ila zinaenda kupumzika na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa  Extra Bongo, ilienda mapumzikoni na sasa imerejea sio next level bali 'Extra Bongo baba Lao’,” amesema Ally Choki

Dar es Salaam. Bendi ya muziki wa dansi, Exra Bongo inatarajia kurudi mjini rasmi baada ya kupotea miaka tisa katika uga wa muziki huo.

Mwenyekiti wa Bendio hiyo, Ally Choki ameyasema hayo leo Jumanne, Oktoba 21,2023 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa bendi hiyo ambapo itazinduliwa rasmi Desemba 2, jijini hapa.

Choki ambaye ndio mwanzilishi wa bendi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2003, amesema ameamua kuirudisha ili kuendelea kuwapa watu burudani.

"Unajua bendi huwa hazifi ila zinaenda kupumzika na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa  Extra Bongo, ilienda mapumzikoni na sasa imerejea sio next level bali 'Extra Bongo baba Lao’,”amesema mwanamuziki huyo.

Akizungumzia namna itakavyofanya kazi, Choki  amesema wamejipanga kuja kivingine ikiwemo kucheza na mitandao ya kijamii kwa kuwa ndio mahali wanapigwa bao na wasanii wa muziki wa Bongofleva.

Pia lengo  kubwa ni kurudisha muziki huo kwenye heshima yake kwa maonyesho yake kufanywa kwa viingilio badala ya vinywaji.

"Katika kuhakikisha hili linafanyika kwenye uzinduzi wa kuirudisha bendi yetu mjini hiyo Desemba, tutakuwa na viingilio vya VIP ambavyo ni Sh200,000 huku kiingilio mlangoni kikiwa ni Sh10,000,"amesema Choki.

Meneja wa bendi hiyo  , Kalumbi Juma maarufu Kaylou, amesema kiwanja cha nyumbani cha  bendi hiyo wamekubaliana kitakuwa katika klabu ya Andrew's Lounge, iliyopo Sinza Kijiweni na tayari maandalizi yapo vizuri.

Hata hivyo amesema dalili za kuwa bendi hiyo watu walikuwa na hamu nayo, kabla ya uzinduzi wake tayari imeshapata shoo katika maeneo mbalimbali ya nchi Desemba baada ya uzinduzi.

Amesema bendi hiyo itakuwa na wasanii 15 na tayari imeshatunga nyimbo 10 kati ya hizo mbili zitatambulishwa rasmi siku ya uzinduzi moja ikiitwa ‘Kinyago changu’ na ‘Penati ya mwisho’.

Ali Choki amewahi kutamba na vibao kama ‘Majirani na Regina aliwahi kuhudumu kwa muda mrefu kwenye bendi ya Twanga Pepeta.