Diamond avuna Sh233 milioni kwa dakika 10

Nairobi. Moja kati ya kivutio kikubwa katika ufungaji wa kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja, Raila Odinga ni kupanda jukwaani kwa msanii Naseeb Abdul (Diamond Platnumz).
Diamond alipanda jukwaani Agosti 6, 2022 katika uwanja wa Moi Kasarani ambapo Diamond Platnumz aliitwa kutumbuiza na kuzusha shangwe kubwa na baada ya kutumbuiza alimuita Odinga ambaye alipata wakati mgumu wa kuwatuliza watu waliokuwa wakimshangilia msanii huyo.
Mara tu baada ya mshehereshaji kumuita Diamond kwenye jukwaa, uwanja unalipuka kwa shangwe na kelele huku wafuasi wa muungano wa Azimio kwanza wakilisogelea jukwaa kutaka kumuona vizuri na kwa ukaribu.
Kitendo cha kuingia jukwaani kimemfanya avune Sh233 kwa dakika chache alizopanda jukwaani kutumbuiza na baadaye kurejea nchini Afrika Kusini kushiriki sherehe za siku ya kuzaliwa kwa binti yake Latifa
Diamond Platnumz alifanya onyesho la dakika 10 la kusisimua lililogawanywa kwenye sehemu mbili kabla na baada ya hotuba ya mgombea wa Azimio la Umoja Raila Odinga.
Alianza kwa kutumbuiza wimbo wake wa 2019 wa ‘Baba Lao’ akibadilisha mashairi kidogo ya kumsifu Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua kisha alitoa hotuba fupi ya kumuunga mkono hadharani kiongozi wa Azimio.

Diamond alirudi tena jukwaani kwa mara ya pili baada ya hotuba ya Odinga na kuimba pamoja na wagombea na viongozi wa Azimio La Umoja.
Baada ya tukio hilo mijadala mbalimbalia iliibuka huku mchekeshaji Erick Omond akiwatupia lawama wasanii wa Kenya kwa kuwa wavivu kwenye kazi zao.
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari zinaeleza kuwa wanasiasa wa Kenya walitenga fedha nyingi kuhakikisha kampeni zao zinafanyika kikamilifu ikiwemo kukodi helikopta 41 na wasanii mbalimbali akiwemo Mbilia Bell
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Gavana wa Mombasa, anayemaliza muda wake Ali Hassan Joho kuwa na mchango mkubwa kwenye kufanikisha dili hilo
"Samahani hii haijarekodiwa, lakini mazungumzo ya Diamond kutumbuiza kwenye mkutano wa Raila yalikuwa yanatarajiwa kwa wiki tatu. Utendaji huo kwa kweli ulifadhiliwa na tajiri mmoja nchini Tanzania, sina uhakika kama tajiri huyo ni mfanyabiashara au mwanasiasa lakini inaonekana wazi ni mtu anayefahamika sana na viongozi wa Azimio. Hata hivyo, uhakika nilionao ni kuwa Diamond alilipwa $100,000 (Sh233.1 milioni) kwa onyesho la Kasarani,” chanzo cha habari kuhusu mipango hiyo kiliiambia Mwananchi.
Hata hivyo haijabainika iwapo tajiri huyo pia alilipa bili ya ndege binafsi iliyotumiwa na Diamond nchini humo na kurejea Afrika Kusini.
Hadi Julai 2021, Diamond alikuwa anatoza $70,000 kwa onyesho la nje ya Tanzania na $50,000 kwa show za ndani maelezo hayo yalitolewa na meneja wake Sallam SK wakati wa mahojiano na Wasafi TV.
Sallam pia alisema mbali na fedha ya onyesho lakini muandaaji anatakiwa kumlipia Diamond ndege binafsi, hoteli ya nyota tano pamoja na chakula.