Dabi hii kumfuta chozi Kiba ama Mondi

MWIMBAJI wa Bongo Fleva kutoka Kings Music, Alikiba wikiendi hii ana kibarua cha kujiuliza kama Dabi ya Kariakoo itamfuta machozi kama ilivyofanya kwa mshindani wake kimuziki Diamond Platnumz.

Waimbaji hao ambao kila mmoja katoa albamu tatu na kushinda tuzo kubwa kama MTV, wote walikaribishwa na vipigo katika dabi ya kwanza ya ligi pindi tu walipobadilisha ushabiki wao katika timu hizo za Kariakoo.

Jumapili hii Yanga na Simba zinazounda Dabi ya Kariakoo inayotajwa kuwa miongoni mwa dabi tano bora barani Afrika, zitashuka Uwanja wa Mkapa katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara 2023/24.

Hii ni dabi ya pili kwa Alikiba akiwa shabiki wa Simba baada ya Agosti 2023 kuhamia akitokea Yanga, mabingwa wa kihistoria ambao sasa wanasaka taji la ligi la tatu mfululizo. Dabi ya kwanza iliyopigwa Novemba 5, 2023, akiwa shabiki wa Simba, Alikiba alishuhudia kipigo cha mabao 5-1 kilichosababisha Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kufukuzwa.
Utakumbuka alipojiunga na Simba, Alikiba alitumbuiza katika ufunguzi wa mashindano ya African Football League (AFL) uliofanyika Tanzania na kukaribisha pambano kati ya Simba dhidi ya Al Alhy ya Misri.  

Alikiba alikuwa ndiye msanii pekee wa Bongo Fleva aliyechaguliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutumbuiza katika mashindano hayo ambayo yalikuwa ya kwanza kufanyika na kushirikisha klabu nane za Afrika.

Ikiwa Simba itaibuka na ushindi katika dabi wikiendi hii, basi itakuwa imemfuta Alikiba machozi ya kipigo cha awali. Ni kitu ambacho kilitokea kwa Diamond baada ya kuhamia Yanga akitokea Simba. Diamond alijiunga na Yanga mnamo Januari 2023 na kupokewa na Rais wa timu hiyo, Hersi Said na aliyekuwa msemaji, Haji Manara katika hafla iliyofanyika Mlimani City.

Akiwa shabiki wa Yanga, dabi ya kwanza iliyopigwa Aprili 16, 2023, Diamond alishuhudia timu yake ikipasuka mabao 2-0 kutoka Simba ambayo ina kiu kubwa na ubingwa baada ya kuukosa kwa misimu miwili mfululizo.

Hata hivyo, dabi ya pili ilimfuta machozi baada ya Yanga kushinda mabao 5-1. Je, dabi ya wikiendi hii itamfuta Alikiba machozi, yaani Simba kuibuka na ushindi mnono? Uzuri ni Alikiba ana tabia ya kusawazisha matokeo lipokuja suala la ushindani na Diamond, mathalani hadi mwaka 2015 Diamond alikuwa ameshindda tuzo 17 za muziki Tanzania (TMA), mwaka 2022 Alikiba akasawazisha na kufikisha tuzo 17.

Diamond alifikisha albamu tatu mwaka 2018, Alikiba akaja kusawazisha 2021. Albamu za Diamond ni Kamwambie (2010), Lala Salama (2012) na A Boy From Tandale (2018), za Alikiba ni Cinderella (2007), Ali K 4Real (2009) na Only One King (2021)
Ikumbukwe iwapo Diamond angehamia Yanga kama mchezaji, basi angecheza eneo la ushambuliaji na kuvaa jezi namba 7 sawa na Cristiano Ronaldo, mshambuliaji wa Al Nassr FC ya Saudi Arabia na timu ya taifa ya Ureno.
Ronaldo ambaye ni mchezaji wa kwanza kushinda mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA), hakuna ubishi ndiye mchezaji anayependwa zaidi na Diamond hadi kutamtaja katika nyimbo zake mbili, Nana (2015) na Waah! (2021).

Hata hivyo, Diamond katika wimbo wake, Fire (2017) akiwa na Tiwa Savage wa Nigeria ameeleza kutambua uwepo wa mshindani wa Ronaldo, Lionel Messi, mshindi mara nane wa Ballon d’Or. Pia anatambua ushindani ya dabi ya Kariakoo.

“Ye ndo Messi uwanjani, msiniibie Simba, Yanga.” Anaimba Diamond katika ngoma hiyo inayopatikana katika albamu yake ya tatu, A Boy From Tandale (2018) iliyotoka chini ya Universal Music Group (UMG).
Alikiba ambaye pia ni shabiki wa majogoo wa Anfield, Liverpool FC, angeweza pia kuhamia Simba kama mchezaji maana ana uwezo na tayari alishacheza Ligi Kuu Bara 2020/21 akiwa na Coastal Union.

Diamond na Alikiba kuwa timu tofauti katika Dabi ya Kariakoo kuna maana kubwa katika ushindani wa muziki wao na ndio sababu hawataki kuwa chama moja; Diamond alipohamia Yanga akitokea Simba, naye Alikiba akahamia Simba akitokea Yanga.
Mwaka 2015 Alikiba alianza kujiita Tembo baada ya kuchaguliwa na shirika la kimataifa la WildAid kuwa balozi wa kukomesha ujangilili wa Tembo. Ghafla Diamond naye akaingia katika ulimwengu wa wanyama na kujiita Simba, akichukua jina hilo kwa Mr. Blue.

Alikiba alipoona hivyo, akaacha kujiita Tembo, katika mahojiano na Podcast ya Swahili Radio by Audiomack, Kiba alisema yeye ni Mfalme anafuga wanyama wote, hivyo haifai tena kutumia jina la mnyama.

Katika wimbo wa Fid Q, Fresh Remix (2017) ambao Diamond alishirikishwa, anajitambulisha kama Simba kutoka mbuga ya Tandale, huku akimchana Alikiba kwa madai amemuachia kitanda na kiti cha Ufalme alichokitaka.

Alikiba akaja kumjibu katika wimbo  wake, Mediocre (2020) na katika video anaonekana akivua kofia yake ya Ufalme na kumvisha Mbuzi, kwake ina maana Mbuzi ni mkali kuliko Simba.

Na kumbuka katika Bongo Fleva anayetumia jina la Mbuzi ni Young Lunya.