Chid Benz awaka baada ya kuzushiwa kifo

Muktasari:
- Wiki iliyopita katika mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram na baadhi ya media za online kulikuwa na taarifa iliyosambaa ya msanii huyo ameaga dunia ghafla na kuzua taharuki na mshtuko kwa watu wengi.
BAADA ya taarifa za uzushi za kifo kuibuka na kuleta mshtuko kwa watu, msanii wa Hip Hop, Chid Benz ameiomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuvichukulia hatua baadhi ya vyombo vya habari vya mitandaoni "Online Media" na wenye akaunti feki wenye tabia hiyo ili waache mara moja.
Wiki iliyopita katika mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram na baadhi ya media za online kulikuwa na taarifa iliyosambaa ya msanii huyo ameaga dunia ghafla na kuzua taharuki na mshtuko kwa watu wengi.
Mwanaspoti lilimtafuta Chid Benz na alionyesha kusikitishwa kwa kuzushiwa kifo na baadhi ya watu na alisema kufa ni lazima na hakuna atakayebaki lakini siyo vizuri kumzushia kifo mtu.
Chid Benz alisema inasikitisha na kushangaza sana mtu anawezaje kumzushia mwanadamu mwenzake kifo na mabaya mengi, wanaofanya hivi ni Watanzania wa kawaida kama wao ambao walitamani watoe habari na burudani na wao wapate riziki, lakini wako bize kutupotosha.
"Mimi nilipopata taarifa za mimi nimefariki nilistushwa sana, yaani ulishawahi kuona marehemu anajiona akiwa hai? Hili sasa naona limezidi, kila kukicha watu kuzushiana vifo tu. Mimi nawaomba sana TCRA wasiache kuzichukulia hatua online Tv, makanjanja wengine na peji feki za mitandao ya kijamii wanaopotosha umma, tuna imani nao TCRA na Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine, watu kama hawa wakiachwa, wanachafua taswira nzuri ya vyombo vingine vinavyofanya kazi kwa weledi, wachukuliwe hatua na kutokomezwa kabisa," alisema Chid Benz na kuongeza.
"Jaman kifo kipo na hakuna atakayekwepa, ni lazima tutakufa na hakuna atakayebakia ila si vyema kunizushia, siku yangu itafika tu na wote mtajuwa lakini siyo jambo la busara kunizushia," alisema Chid Benz.