TUONGEE KISHKAJI: Saluti kwao Cheka Tu kuanzisha chaneli ya TV

Muktasari:

  • Walianza kwa kuanzisha kundi la wachekeshaji miaka zaidi ya sita nyuma. Wakafanya vizuri, lakini kwa bahati mbaya kundi lilivurugika na baadhi ya wachekeshaji wakaondoka na kwenda kuanzisha kundi lingine linaloitwa Watubaki.

KWENYE intavyuu za kazi kuna maswali ambayo lazima ukutane nayo. Swali kama unajiona wapi miaka mitano ijayo? Hili lilishazoeleka kiasi kwamba hata kama hutaulizwa lakini ni vyema ukaenda ukiwa na jibu lake.

Na ili kuthibitisha kwamba ni swali maarufu ukizunguka mitandaoni utakutana na mamilioni ya makala na video zinafundisha jinsi ya kujibu swali hilo.

Kimsingi hilo ni swali gumu kwa wengi wetu na ni kwa kwa sababu linahusisha mambo ya mipango. Wabongo si unatujua mambo ya kujipanga sio yetu kabisa. Mtu hata plani za kesho hana unamuuliza mambo ya kujiona wapi miaka mitano ijayo.

Lakini nina uhakika swali hilo wangeulizwa waanzilishi wa Cheka Tu mbona aliyeuliza angekoma. Kwanini? Kwa sababu ni kama vile jamaa walikuwa wamejipanga sana. Juzi Ijumaa, mwanzilishi wa Cheka Tu, Coy Mzungu na timu yake walizindua chaneli ya kwanza ya TV Tanzania na pengine Afrika Mashariki kwa ajili ya vichekesho. Kwa kuanzia chaneli hiyo itakuwa inapatikana kupitia kisumbuzi cha Azam namba 414. Lakini ukirudi nyuma na kutazama kila hatua waliyopitia Cheka Tu utagundua kwamba walijipanga na pengine Mungu yupo upande wao na anabariki kila wanachopanga.

Walianza kwa kuanzisha kundi la wachekeshaji miaka zaidi ya sita nyuma. Wakafanya vizuri, lakini kwa bahati mbaya kundi lilivurugika na baadhi ya wachekeshaji wakaondoka na kwenda kuanzisha kundi lingine linaloitwa Watubaki.

Muda mwingine nahisi hiyo kutengana ulikuwa ni mpango wao kwani baada ya pale kulitokea ushindani mkubwa wa kuzalisha maudhui kati ya Cheka Tu na Watubaki. Ni kama ambavyo kwenye muziki unaona timu zinavyofanya muziki uchangamke.

Baadaye Cheka Tu wakaungana na Wasafi na wakalitumia jina la Diamond vizuri sana kujikuza. Hata hivyo, ni kama vile wachekeshaji wengi wakali walikuwa wamekwenda Watubaki. Hivyo Cheka Tu ilikuwa ni aidha ife au itafute namna ya kuja na wachekeshaji wapya wazuri.

Kuonyesha kwamba jamaa walikuwa wamejipanga mara walianzisha Cheka Tu Comedy Search ambayo lengo ilikuwa ni kuzunguka mikoa mikubwa ya Tanzania na kufanya usaili wa wachekeshaji. Na mwisho wa siku wakachukua ile TOP FIVE na kui-brand na mpaka leo ndiyo wachekeshaji wakubwa wa majukwaani Tanzania kiasi kwamba wanawazidi hata baadhi ya wachekeshaji wa Watubaki kwa umaarufu.

Mtu kama Eliud Samweli ni zao la Cheka Tu comedy Search. Leonardo, Said Said, Asma, Ndaro Mjeshi na zaidi.

Majuzi walizindua application ya simu inayoitwa Cheka Plus kwa ajili ya watu kutazama maudhui yao huko na sasa hivi wanazindua TV ya vichekesho ambayo binafsi naitabiria mazuri. Kukiwa na TV ambayo kazi yake ni kuonyesha vichekesho tu mwanzo mwisho unadhani nani hatataka kuitazama kupunguza stresi.

Kusema ukweli nashindwa kujizuia kuwatabairia makubwa Cheka Tu. Kwa kutazama mienendo na nyendo zao naona kabisa washikaji wanakwenda kuwa bonge moja la jukwaa na wataokoa Watanzania wengi sana wenye vipaji vya kuvunja mbavu.