Chapa la Zuchu kwenye mlima wa fedha kuvuta soko

Chapa la Zuchu kwenye mlima wa fedha kuvuta soko

IKIWA ni miaka miwili tangu atoke kimuziki, Zuchu kwa ushirikiano na WCB anazidi kuijenga chapa yake kwenye mlima wa fedha na kujijengea taswira ya kuwa msanii wa kike ghali zaidi Afrika Mashariki kwa sasa.

Zuchu aliyetambulishwa WCB Wasafi Aprili 2020 na kuwa msanii wa pili wa kike wa lebo hiyo baada ya Queen Darleen, ana Diploma ya Business and Commerce aliyoipata nchini India.

Tayari ametoa Extended Playlist (EP) moja, I Am Zuchu, ameshinda tuzo mbili; African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2020 na East Africa Entertainment Awards (EAEA) 2022.

Ameweza kushirikiana na wasanii wa kimataifa kama Bontle Smith (Afrika Kusini), Joeboy (Nigeria), Tyler ICU (Afrika Kusini), Olakira (Nigeria), Spice Diana (Uganda) na wengineo.

Zuchu ndiye msanii pekee wa kike Tanzania na Afrika Mashariki ambaye video zake zimetazamwa zaidi kwenye mtandao wa YouTube zikifikisha kutazamwa zaidi ya mara milioni 350.

Mwaka 2021 video ya wimbo wake, Sukari iliweka rekodi Afrika kwa kutazamwa zaidi ya mara milioni 60 na kuivunja rekodi aliyoiweka Diamond Platnumz mwaka 2020 kupitia video ya wimbo wake, Jeje iliyotazamwa zaidi ya mara milioni 40.

Lakini ni kwa namna gani Zuchu ameweza kuijenga chapa yake kifedha? Makala haya yanaenda kuangazia hilo kwa kuanzia bei za shoo zake, viingilio vya shoo zake, dili zake za ubalozi na makazi yake.

Kwa sasa Zuchu anatoza Sh46.3 milioni kwa shoo za nje ya nchi, huku za ndani zikiwa ni Sh34.8 milioni, huyu ndiye msanii pekee wa kike Bongo kuweka wazi malipo anayohitaji kuendana na ukubwa wa chapa yake.

Bei hiyo ilitangazwa na Meneja wa WCB, Sallam SK ikiwa ni ongozeko la Sh26.3 milioni kutoka bei ya awali ya Sh20 milioni ambayo ilikuwa imetangazwa Julai 29, 2020 kwa shoo za kimataifa.

Na Agosti 13 mwaka huu Zuchu alifanya shoo yake ya kwanza barani Ulaya ambapo alitumbuiza nchini Uingereza katika jukwaa la African Nite.

Shoo yake Siku ya Wapendanano, Februari 14 mwaka huu Mlimani City, Dar es Salaam, vingilio vilikuwa ni Sh50,000, Sh100,000, Sh2 milioni, Sh3 milioni na Sh5 milioni. Kwa mujibu Zuchu, tiketi zote zilimalizika.

Hii ilikuwa mara ya pili kwa Zuchu kufanya shoo katika ukumbi huo na kuuza tiketi zote, mara ya kwanza ilikuwa Julai 18, 2020 ambapoo viingilio havikupishana sana na hivyo vya mwaka huu ingawa shoo hii tiketi zilimalizika saa saba kabla ya tukio lenyewe.

Hapo Julai 2020 Zuchu alitangaza kuwa anatoza kati ya Sh80 hadi 100 milioni iwapo kuna kampuni, taasisi au shirika linahitaji kumtumia kama Balozi kwa lengo la kutangaza bidhaa au huduma zao.

Hadi sasa Zuchu ameweza kufanya kazi za Ubalozi na kampuni kama Darling Hair Tanzania, Zantel, Wasafi BET, Spotify na Infinix.

Utakumbuka Diamond tayari alishaweka wazi kuwa kwa mwezi anapokea Sh200 milioni kwa dili zake za Ubalozi ambazo anafanya kazi na kampuni za kuuza vinywaji baridi, simu za mkononi, sabuni, rangi za nyumba n.k.

Kwa mujibu wa Zuchu mwenyewe, nyumba anayoishi amekuwa akilipa kodi Sh3.7 milioni kwa mwezi ambazo ni sawa na Sh44.4 milioni kwa mwaka mmoja.

Anasema anaweza kuishi nyumba ya kawaida yenye bei nafuu ila haina faida kwa chapa yake, anasistiza bei ya msanii katika soko inavutwa na mtindo wake wa maisha, hivyo ukitaka dili la Sh200 milioni lazima mtindo wako wa maisha uonyeshe kweli unastahili kiasi hicho.

Ndani ya miaka miwili Zuchu amefanikiwa kumiliki magari matano ambapo matatu anayotumia yeye mwenyewe likiwemo Toyota Vanguard, huku mawili akiyatoa zawadi ambapo mama yake mzazi, Khadija Kopa alipata aina ya Toyota Alphard, huku meneja wake, Dorice Mziray alipata aina ya BMW.

Je, wasanii kuweka wazi gharama za muziki wao na mambo yanayowazunguka kuna maana gani hasa kwa ukuaji wa chapa yao? Msanii wa Bongofleva, Malaika na Meneja wa Wasanii na pia Branding and Communication Expert, Dokta Ulimwengu wanaliangazia hilo.

Akizungumza na gazeti hili, Malaika amesema ingawa kufanya hivyo ni jambo la kibinafsi zaidi, ila hakuna ubaya kwa msanii kuweka wazi gharama za shoo kwani kutengeneza muziki ni gharama pia.

“Gharama za shoo lazima ziwepo maana msanii hatengenezi wimbo bure, video kwa sasa ni gharama sana, imefika milioni 10 na kuendelea ndio ufanye video nzuri ambayo inaeleweka. Audio kurekodi ni milioni 1.5 hadi 2, hivyo msanii lazima atangaze bei ya shoo ili arudishe fedha yake,” amesema Malaika.

Kwa upande wake Dokta Ulimwengu anayesimamia chapa za wasanii kama Hamisa Mobetto, Idris Sultan, Jaymond na Jux, amesema wasanii kufanya hivyo ni kwa ajili ya kutengeneza thamani yao mbele ya soko.

“Lazima ujue kuwa anatumia gharama kubwa kusimamia chapa yake, kwa sababu asipokuelezea wewe utakuja na ofa yako ambayo kwa maisha yako utaona inafaa,” amesema.

Lakini iwapo msanii anafanya vizuri katika sanaa yake kuna ulazima wowote wa kufanya hivyo? Dokta Ulimwengu anasema: “Chapa inapotafuta Balozi inaangalia mtu mwenye ushawishi tu.“