Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chameleone msanii wa kwanza Afrika Mashariki kutumbuiza Bongo Flava Honors

Muktasari:

  • Bongo Flava Honors inalenga kuwaheshimu siyo tu wasanii wa Tanzania, bali pia watu wote waliotoa mchango mkubwa katika kukuza na kueneza muziki huo ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Mwanamuziki mkongwe kutoka Uganda, Jose Chameleone, ameandika historia kwa kuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kutumbuiza katika jukwaa la Bongo Flava Honors, hatua inayotambuliwa kama heshima kwa mchango wake mkubwa katika ukuaji na maendeleo ya muziki wa Bongo Flava Afrika Mashariki.

Chameleone atatumbuiza Julai 31, 2026 kwenye ukumbi wa The Super Dome, Masaki katika shoo ya pili ya msimu wa nne wa tamasha la Bongo Flava Honors linaloandaliwa na Deiwaka World.

Akizungumza wakati wa utambulisho wake leo Juni 14, 2026 Chameleone amesema anajivunia kupata nafasi ya kushiriki katika tamasha hilo na kuahidi kutoa burudani ya kiwango cha juu kwa mashabiki wa ndani na nje ya nchi watakaohudhuria siku hiyo.

"Napenda kuishukuru Tanzania, Afrika Mashariki na Watanzania wote, najivunia kuwa sehemu ya Bongo Flava Honors, watu wengi wameniona kwenye televisheni lakini hawajawahi kuniona live.

"Tumeanza mapema kujiandaa na nina uhakika itakuwa zaidi ya shoo," amesema Chameleone.

Msanii huyo aliyetikisa anga la muziki kwa nyimbo kama Jamila na Tubonge amesema muziki wake umependwa Tanzania kwa sababu unaelezea maisha halisi ya watu huku akitumia lugha ya Kiswahili inayowaunganisha watu wengi zaidi Afrika Mashariki.

"Watu wengi Uganda hujiuliza kwa nini ninaimba Kiswahili badala ya Kiganda, lakini Kiswahili ni lugha ya kimataifa, ninaimba maisha halisi ambayo watu wengi wanaweza kuyaelewa na kujihusisha nayo," amesema.

Katika shoo hiyo Chameleone ataimba na bendi yake kamili kutoka Uganda na amebainisha kuwaalika wanamuziki mbalimbali aliofanya nao kazi kwa nyakati tofauti akisisitiza lengo ni kuhakikisha mashabiki wanapata burudani bora, huku akibainisha kuwa maandalizi na mazoezi makubwa yatafanyika nchini Uganda na baadae Tanzania kabla ya shoo.

Mratibu wa tamasha hilo, mwanamuziki na  Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, amesema Chameleone amestahili heshima hiyo kutokana na mchango wake mkubwa katika muziki wa Bongo Flava na ushirikiano wake wa muda mrefu na wasanii wa Tanzania.

"Mchango wake katika muziki wa Bongo Flava ni mkubwa. Ni mmoja wa wasanii wa nje walioweza kufanya ziara katika mikoa mingi ya Tanzania kuliko hata baadhi ya wasanii wa hapa nchini.

"Ana mchango mkubwa katika muziki wa Afrika Mashariki, ndiyo maana amekuwa wa kwanza kupata nafasi hii, na naamini hatakuwa wa mwisho," amesema Sugu.

Naye meneja masoko wa The Super Dome, Isack Baha amesema ukumbi huo umejijengea sifa ya kuandaa matamasha makubwa yenye viwango vya kimataifa ikiwamo la Chameleone.

"Tunafahamika kwa ubora wa shoo tunazoandaa, tuna timu imara inayofanya kazi kwa karibu na wasanii na wadau mbalimbali kuhakikisha kila tamasha linafanyika kwa mafanikio na Julai 31, Chameleone atahakikisha kila atakayefika anaondoka akiwa na furaha," amesema Baha.

Bongo Flava Honors inalenga kuwaheshimu siyo tu wasanii wa Tanzania, bali pia watu wote waliotoa mchango mkubwa katika kukuza na kueneza muziki huo ndani na nje ya mipaka ya nchi, Professa Jay ndiye alikuwa mwanamuziki wa kwanza kufungua msimu wa nne akifuatiwa na Chameleone  huku msimu wa tatu ukifungwa na mkongwe, Seleman Msindi (Afande Sele).