Bruce Melodie adondosha “Niki Minaji” X Blaq Diamond
Muktasari:
- Wimbo huo haumzungumzii moja kwa moja Nicki Minaj kama binadamu bali unaelezea namna alivyo mrembo na mwenye kujiamini mbele ya jamii.
MSANII wa muziki kutoka Rwanda, Bruce Melodie, ameachia singo yake mpya iitwayo “Niki Minaji” akiwa amemshirikisha msanii wa Afrika Kusini, Blaq Diamond.
Ni kibao chenye mikong'osio ya Amapiano na Afropop ambapo wawili hao wamefanya vurugu za aina yake ndani ya ngoma hiyo.
Wimbo huo haumzungumzii moja kwa moja Nicki Minaj kama binadamu bali unaelezea namna alivyo mrembo na mwenye kujiamini mbele ya jamii.
Ujumbe wa wimbo huo unaelezea namna mtu anapokuwa katika mapenzi na binti mrembo aliye maarufu pia kwenye jamii yake jambo linalompotezea kujiamini.
"Nilitaka kuonyesha kwamba unapokuwa katika mapenzi ya dhati, hata kama huyo mtu ni mrembo kiasi gani, mtanashati au jasiri, anaweza kulinganishwa na msichana huyu ninayempenda," Bruce Melodie alizungumzia video hiyo iliyorekodiwa jijini Kigali, Rwanda, ikiongozwa na Jean Chretien Munezero.
Wakati huohuo, Bruce Melodie alitangaza kujiandaa kutoa kwa albamu mpya ya nne iitwayo 'Colorful Generation', atakayoiachia mapema mwakani (2025).
Ni albamu iliyowashirikisha mastaa kibao wakiwemo, Joe Boy katika traki “Not A Lie” , Mkenya Bien kwenye wimbo “Iyo Foto” na staa wa kimataifa wa Reggae /dancehall, Shaggy kwenye wimbo “When She’s Around (Funga Macho)”.