Basata yatoa muongozo kudhibiti corona

Friday July 30 2021
basata pic

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Matiko Mniko

By Nasra Abdallah

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limetoa masharti  tisa uendeshaji wa shughuli za sanaa katika kudhibiti ugonjwa wa corona 19 ikiwemo kusafishwa vema kwa vitakasa vifaa wanavyotumia kupiga muziki.
Vifaa hivyo ni pamoja na magitaa, vipaza sauti, tumba, vinanda vinavyotimika wakati wa burudani ambapo vitatakiwa kutakaswa kabla na baada ya kutumika.
Maagizo hayo yametolewa leo Ijumaa Julai 30, 2021 na Kaimu Katibu Mtendaji wa baraza hilo Matiko Mniko ambayo yapo katika mwongozo wa uendeshaji wa shughuli hizo katika mapambano dhidi  ya ugonjwa wa corona.
Akizungumza na Mwanaspoti, Matiko amesema Mei 2 mwaka  jana Baraza  kwa kushirikiana na wasanii na wadau mbalimbali wa Sanaa  na burudani uliandaliwa mwongozo ambao ulilenga kuweka mazingira wezeshi na  salama katika kuendelea na shughuli za Sanaa na burudani ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo na maazimio yake yakotoka na mwongozo huo.
Amesema kipengele ‘E’ cha muongozo huo kimeeleza shughuli za matamasha ya muziki na matukio mengineyo yanapaswa kuzingatia masharti bayana mara baada ya kupata kibali kutoka Basata.
Ameyataja masharti hayo kua ni pamoja kushirikina na mamlaka nyinginezo za serikali za Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa wakiwemo Halmashauri husika na Maofisa Utamaduni kusimamia na kukagua uzingatiaji wa masharti ya afya  dhidi ya maambukizo ya corona.
“Hii itakuwa ni  katika viwanja au maeneo ya wazi  na maeneo maalum ikiwemo kumbi za harusi,sherehe na burudani.
 “Pia Wasanii na waandaji wa matukio wanawajibika kuwakumbusha waalikwa na watazamaji mara kwa mara namna ya kujikinga na maambukizi kwa kuzitaja njia sahihi zilizoelekezwa na Wizara ya afya,” ameagiza Katibu huyo.
Njia zilzioelekezwa na Wizara hiyo ni pamoja na kupima joto la mwili, matumizi ya vitakasa mikono na maji tiririka, uvaaji barakoa na kuzingatia umbali wa  mita moja wakati wa ukaaji au usimamaji kati ya mtu mmoja na mwingine,” amesema Katibu huyo
Masharti mengine,Matiko amesema  ni wamiliki wa kumbi  za starehe, sherehe na burudani, waandaji wa matukio wa wasimamizi wa viwanja vinavyotumika kwa matamasha kuhakikisha  miundombinu yao inafanya kazi  na kuwawezesha waalikwa au wateja wao kujikinga na maamubuki.
Pia amesema  suala la kuzingatia idadi ya watu katika kumbi kwa kulingana na madaraja na   ukubwa kwa maeneo  au kumbi  lizingatiwe kwa kupunguza idadi  ya wateja au wadau.
Aidha Matiko amesema milango yote ya kuingiza watu kwenye matamashainapaswa ifunguliwe mapema na itumike kwa kuzingatia umbali wa mita moja wakati wa kuingia ili kuepusha misongamano.
Kuwasiamia vyema watoa huduma  mbalimbali  wakiwemo washehereshaji, DJ na watoo huduma wa vyakula  katika kuendesha  ratiba na matukio wanapokuwa ndani  ya ukumbi wa sherehe au burudani.
Wakati kwa wasanii kutoka nje, amesema wana wajibu wa kutoa uthibitisho kuwa hawana maambukizi ya corona.

Advertisement