Aziz Ki alipa mahari ya ngo'mbe 30 kumuoa Hamisa Mobetto

Muktasari:
- Mahari hiyo imekabidhiwa na Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said kwa niaba ya familia ya Aziz Ki katika zoezi lililofanyika Viwanja vya Gofu, Mikocheni jijini Dar.
HATIMAYE! Taarifa ikufikie kwamba, mwanamitindo Hamisa Mobetto leo Februari 15, 2025, amelipiwa mahari ya ng'ombe 30 na mume wake mtarajiwa, Stephanie Aziz Ki ambaye ni kiungo mshambuliaji wa Yanga SC raia wa Burkina Faso huku mipango kabambe ya ndoa ikiendelea.
Mahari hiyo imekabidhiwa na Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said kwa niaba ya familia ya Aziz Ki katika zoezi lililofanyika Viwanja vya Gofu, Mikocheni jijini Dar.
Katika zoezi la utoaji wa mahari hiyo, Aziz Ki ameongozana na baadhi ya wachezaji wa Yanga akiwemo Pacome Zouzoua, Bakari Mwamnyeto, Yao Kouassi na Ofisaa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe.
Kwa upande wa Hamisa Mobetto, aliingia eneo la tukio akiwa na meneja wake, Paul Mangoma huku warembo 15 wakitangulia wakiwa wamevaa sare.
Hamisa Mobetto ameliambia Mwanaspoti kuwa, anamshukuru Mungu kumpata mtu anayeona ndiye anamfaa katika maisha yake na tayari sasa ni mchumba rasmi wa mtu, tena kijana anayempenda kwa dhati.
“Sasa hapa ndiyo nimefika kwa kuwa nimekutana na mtu mwenye mapenzi ya kweli kwangu. Pia nafsi zetu zimeendana, hapa namuomba Mungu anyooshe mambo yaende kama vile tulivyopanga,” amesema Hamisa Mobetto.
Kwa upande wa Aziz Ki, amesema anaamini safari yake ya muda mrefu imefika kwa kuwa amempata mwanamke anayempenda kutoka ndani ya uvungu wa moyo wake.
Aziz Ki aliongeza kuwa, kwa upande wake taratibu zote za uchumba amemaliza, kilichobaki anasubiri ndoa tu iliyopangwa kufungwa kesho Jumapili Februari 16, 2025 huku sherehe rasmi ikitarajiwa kufanyika Februari 19 mwaka huu kwenye ukumbi wa The SuperDome uliopo Masaki jijini Dar es Salaam.