Ali Kiba, Diamond uso kwa uso na Konde Boy

Muktasari:

  • Hii ni albamu ya tano kwa Harmornize baada ya awali kuachia 'Visit Bongo' ya mwaka jana yenye ngoma 14 zilizotanguliwa na Afro East ya 2020, High School ya 2021 na Made For Us ya 2022.

MAFAHARI watatu wa muziki wa kizazi kipya nchini, Diamond, Alikiba na Harmonize leo usiku wanatarajiwa kukutana kwa mara ya kwanza katika shoo ya muziki ya uzinduzi wa albamu, kitu ambacho hakijawahi kutokea kwa miaka ya karibuni.

Ipo hivi. Mondi hajawahi kuhudhuria shoo au uzinduzi wowote wa Harmonize tangu alipojiengua WCB Wasafi mwaka 2019, lakini huenda leo akawa mmoja ya mastaa watakaonogesha shoo ya Konde Boy inayofanyika Mlimani City, jijini Dar es Salaam, huku Alikiba naye akitajwa atakuwepo kuongeza utamu.

Harmonize anafanya uzinduzi wa albamu mpya iitwayo ‘Muziki wa Samia’ utakaofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City kuanzia saa mbili usiku, huku nyota kibao wakitarajiwa kuhudhuria shoo hiyo.

Hii ni albamu ya tano kwa Harmornize baada ya awali kuachia 'Visit Bongo' mwaka jana yenye ngoma 14 iliyotanguliwa na Afro East ya 2020, High School ya 2021 na Made For Us ya 2022.

Iwapo Mondi atafika kama ilivyotangazwa katika bango la wasanii wageni waalikwa, basi hilo litakuwa ni tukio la kwanza la burudani kuwakutanisha kwenye uzinduzi wa albamu hiyo ya Harmonize anayetajwa kama mmoja wa mahasimu wake katika miondoko hiyo nchini.

Hivi karibuni, mastaa hao walitupiana maneno katika mitandao ya kijamii kupitia akaunti za instagram ambapo ishu ilianzia Aprili 27, 2024, Diamond alikuwa na shoo kwenye viwanja vya Posta-Kijitonyama, Dar es Salaam, iliyohudhuriwa na wasanii wengine walipanda jukwaani kutumbuiza.

Lakini ilipofika zamu yake alitumbuiza nyimbo zake kadhaa na katikati alisimamisha shoo na kusema daima Harmonize na Rayvanny watasalia kuwa wanawe na atazidi kujivunia mafanikio yao kimuziki.

Alifafanua kuwa bila yeye pengine wasanii hao wasingejulikana kimuziki.

Itakumbukwa Harmonize alikuwa msanii wa kwanza kabisa kusainiwa katika Lebo ya WCB Wasafi ilipozinduliwa 2015 kisha akaja Rayvanny na wengine kama Lava Lava, Queen Darleen na baadaye Mbosso na Zuchu, na mwaka jana akamalizia na D Voice. 

Baada ya Diamond kusema hivyo, kauli hiyo ilionekana kutomfurahisha Harmonize ambaye alisema kauli za kusema kila mara kwamba alisaidiwa kimuziki zinamchosha na kumkera.

Harmonize alikwenda mbali zaidi na kujibu akidai kwamba kwa Diamond kumwambia hivyo anakaribia kujuta kukubali msaada wake kimuziki, lakini pia akasema ni bora bosi wake huyo a zamani akaacha kujivunia mafanikio yake kwani alishamlipa fedha za kuvunja mkataba.

Kwa kumjibu, Diamond baada ya majibu hayo ya Harmonize alionekana kukubaliana naye akisema hakuwa anajua kuwa alikuwa amejitayarisha kwa malumbano, na kwamba ameshinda katika vita hiyo ya maneno huku yeye akijitaja kuwa mnyonge ambaye hawezi tena kuendelea kubishana.

Katika uzinduzi wa albamu wa leo kutakuwa na wasanii wengi walioalikwa akiwemo Ali Kiba, Nandy, Zuchu, Aslay, Dully Sykes, Billnas, Macvoice, Ibra, Weusi, Dogo Janja, Mrisho Mpoto, AY, Jux na Gigy Money. 

Wengine ni Man Fongo, Maua Sama, Miso Misondo, Tunda Man na wengine wengineo. 

Kwa upande wa wasanii wa filamu walioalikwa ni pamoja na Irene Uwoya, Wolper, Lulu, Wema Sepetu, Hamisa Mobetto, Aunt Ezekiel, Steve Nyerere, MC Gara na Mpoki, ilhali upande wa watayarishaji muziki ni Man Walter, S2zzy, Abbah, Master J na wengineo. Vilevile wanatarajiwa kuwapo viongozi mbalimbali wa kiserikali.