Prime
Adam Kibaro na maajabu ya fikra katika Tamthilia ya 'Noma'
KWA sasa tasnia ya Bongo Movie imetawaliwa na tamthilia. Kila kukicha zinaibuka tamthilia mbalimbali zinazoteka hisia za mashabiki kutokana na kufuatiliwa kwa wingi na kuwafanya watayarishaji kuumiza vichwa kuona wanaendeleaje kuwapa mashabiki burudai inayokata kiu yao.
Moja ya Tamthilia zinazokimbiza kwa sasa ni 'Noma' iliyoandaliwa na Adam Kibaro ambaye pia ni mwandaaji wa 'Koneksheni' iliyofanya vizuri.
Kibaro pia amewahi kusimamia matukio makubwa nje ya sanaa, yakiwamo ya michezo na simulizi zake zimekuwa zikigusa hisia za wengi.
Kibaro anaendesha shughuli zake katika ofisi yake ya uzalishaji iliyopo Sinza, mtaa wa Matatiele (karibu na Layani Hotel), na ofisi ya masoko iliyopo Makumbusho.
Kutokana na fikra zake za kibiashara na ujasiri wa kuwekeza kwenye ubora, anathibitisha ukiwa na maono na uvumilivu, unaweza kubadilisha tasnia yoyote unayoguza.
Safari yake kutoka kwenye helikopta ya Diamond uwanjani hadi kwenye skrini za sebuleni kupitia 'Noma' ni ushahidi tosha kuwa huyu ni "Genius" anayejua nini anafanya katika ulimwengu wa burudani na biashara Tanzania.
Falsafa ya miaka 50 ndani ya watu wa miaka 35
Licha ya Adam Kibaro kuwa na umri wa miaka 35, anajinasibu kuwa na uzoefu wa maisha wa mtu mwenye miaka 50. Anasema kuwa 'exposure' uzoefu wa mazingira aliyoipata katika maisha imemsaidia kuona vitu mbali zaidi ya umri wake, hii ndiyo siri inayomfanya aweze kutunga simulizi zenye mashiko kwa muda mfupi, ana uwezo wa kujenga wazo la stori na kulikamilisha ndani ya saa moja au mbili tu.
Kibaro haichukulii sanaa kama burudani pekee, bali kama pendekezo la kibiashara 'proposal'.
"Naiangalia stori yangu au wazo langu kama proposal, lazima iwe imeshiba kuweza kumshawishi mteja," anasema akielezea jinsi anavyotumia taaluma yake ya masoko kwenye filamu.
Ayabeba matamasha ya michezo, amtaja Diamond
Mbali na filamu, Kibalo ndiye injini ya kampuni ya AMOK Marketing Limited, ambayo imefanya mapinduzi makubwa ya kimasoko katika michezo nchini.
Anasema, “Kwenye upande wa sports branding and activation sisi ndiyo kampuni namba moja. Sisi tumetransform namna gani matukio ya mpira nje ya mpira yanatakiwa kufanywa, yaani nje ya dakika 90. Tuliikuta Simba Day ikiwa haina uwekezaji wowote wa branding, tukaingia na kufanya Simba Day ya kwanza ya mwaka 2020 ile ambayo Diamond Platnumz anaingia na helikopta uwanjani; sisi ndio ambao tulifanya.
"Tumefanya kazi na Simba kwa miaka sita au saba sasa, tumebadilisha namna trophy handover ceremonies zinatakiwa kufanyika kuanzia Ruangwa mpaka michuano ya kimataifa kama African Football League. Ile steji ambayo Ali Kiba anapanda pale na kombe linatoka hivi, ile tumetengeneza sisi wenyewe. Hakuna tukio kubwa la kimpira nchi hii ambalo limefanyika halijawahi kupita katika mikono yetu tangu 2019, zipo kama Azam Sports Federation Cup, NBC Premier League na hata African Football League.”
Machungu ya tamthilia ya Koneksheni
Ingawa sasa anafurahia mafanikio ya 'Noma', safari yake haikuwa rahisi, Kibaro anakiri tamthilia ya Koneksheni ilimpa changamoto kiasi cha kutaka kuacha sanaa kabisa.
"Ilifikia wakati una pesa alafu haikusaidii, vitu vilikuwa vizito," anasema.
Katika mradi huo, Kibaro alipata hasara kubwa na ndani ya siku tano alitumia zaidi ya Sh10 milioni, lakini kazi iliyofanyika ilikuwa na thamani ya chini ya Sh2 milioni, changamoto kubwa ilikuwa ni ukosefu wa nidhamu na kujitolea kwa wasanii na wengine walikuwa wanachelewa masaa mengi na kusababisha hasara ya gharama za kila siku, kama chakula, 'location' na 'crew'.
Hata hivyo, aliamua kubaki na mtazamo chanya, akiamini hiyo ndiyo gharama ya kulipia ugeni wake kwenye tasnia.
Uchaguzi wa Riyama Ally na maono ya Chioma
Katika tamthilia ya 'Noma', Kibaro alionyesha ujasiri mkubwa katika kuchagua wasanii. Anasema katika nafasi ya Riyama Ally, hakuona mwingine yeyote ambaye angeweza kuivaa kama yeye.
"Kama ningemkosa Riyama, mimi mwenyewe ningesikitika," anasema na kubainisha mapokeo ya watu kwa Riyama kwenye tamthilia hiyo ndiyo yalikuwa lengo lake.
Vilevile, Kibaro ana jicho la kipekee la kuona vipaji, alimtabiria msanii Chioma atakuwa msanii wa kike namba moja nchini na sasa utabiri huo unatimia kutokana na kazi nzuri anayoifanya kwenye Tamthilia ya Noma.
Awatolea uvivu watayarishaji
Anasema baadhi ya watayarishaji ambao wanawazuia wasanii wao kufanya kazi na watu wengine, akikiita kitendo hicho ni uoga na kutokujiamini. Kwake, sanaa ni maono, na msanii anapaswa kuwa huru kugawanyika kwa watayarishaji tofauti ili kukuza tasnia.
Ushindani wa Noma, Kombolela
Akizungumzia ushindani wa tamthilia mtaani, Kibaro anasema hana hofu na kazi nyingine, bali anafurahia kuona mashabiki wakigawana mbao kati ya 'Noma' na 'Kombolela'.
Anasema, “Kwenye upande wa hofu sina hofu kabisa, lakini nakubali uwepo wa tamthilia zinazofanya vizuri kama Kombolela. Ni tamthilia ambayo inaishi na imetengeneza magwiji kama Mzee Kikala na Biti Msumi ambao watu wanaishi nao nje katika maisha ya uhalisia. Huko mtaani mashabiki kugawanyika kati ya Noma na Kombolela ni sawa na Simba na Yanga; ni kwa sababu hizi ni kazi mbili bora nchini kwa sasa na zinafuatana. Mtu anayeangalia Noma ndiye huyo huyo anayeangalia Kombolela na tunapenda kuona watu wanavyobishana kwa sababu hiyo inaonyesha kazi zetu zimefanikiwa kuwafikia watu moja kwa moja.
Ni Mnyama lialia, awakubali Rushine, Kagoma
“Mimi ni Simba kwa vitu vingi sana. Simba ni moja ya walezi wangu. Kwa sasa tunapitia kipindi kigumu ndiyo maana tunatoa sare, kila timu inapitia vipindi hivi.
"Mchezaji ninaowapenda Simba ni wawili; Rushine De Reuck na Yusuf Kagoma, hawa ni wachezaji wanaocheza kwa moyo, yaani ile kwao sio kazi bali yale kwao ni maisha.
"Ukiangalia namna Rushine anavyopambana hadi mwisho unaona kabisa huyu mtu inabidi hata aongezewe mshahara, ukiangalia Kagoma anacheza mpaka unatamani tumpumzishe sasa huyu tofauti na wachezaji wengine. Ingekuwa tunapata ile hari ambayo wachezaji hawa wawili wanayo kwa kikosi kizima, basi tungekuwa tunafanya vizuri sana na kuwa na mwendelezo nzuri ya matokeo, na kwenye suala la ubingwa msimu huu sijakata tamaa tunaweza kubeba kombe."
Diamond v Ali Kiba
Kibaro anamtaja Diamond Platnumz kama mwanamuziki aliyebadilisha thamani ya sanaa Tanzania.
“Namkubali Diamond Platnumz kwa sababu ameweza kuishape 'industry' na kuipa thamani muziki. Diamond ndio msanii wa kwanza mimi kwa akili zangu timamu niliyemsikia miaka ya nyuma akisema hafanyi show chini ya milioni 10, wakati kipindi hicho wasanii wenzake walikuwa bado wanafanya show kwa laki au milioni moja.
"Leo hii unaona namna gani amewanyanyua vijana na ana ushawishi mkubwa ndani na nje ya kazi yake. Ni mtu pekee anayetuwakilisha sisi kimataifa na muziki wake kupenya nje ya mipaka kuliko mwingine yeyote. Diamond ametufanyia makubwa sana kama nchi na kwangu mimi yule ni balaa.”