‘Baby shower’ ya Paula ilivyoacha maswali kwa Wema, Kajala

Muktasari:

  • Wema ni mmoja wa wasanii maarufu nchini tangu alipotwaa taji la Miss Tanzania mwaka 2006 na kuingia machoni na masikioni mwa Watanzania.

ILIKUWA lazima iwe hivyo. Na kama ingepita tu, basi umaarufu wa msanii Wema Sepetu ungekuwa shakani, labda tungejiuliza umekufa? Hafuatiliwi? Au ndo watu wameamua kupotezea matukio yake.

Wema ni mmoja wa wasanii maarufu nchini tangu alipotwaa taji la Miss Tanzania mwaka 2006 na kuingia machoni na masikioni mwa Watanzania.

Hata hivyo, umaarufu una mambo yake. Kuna kusifiwa, kusemwa vibaya na kupewa michongo na madili makubwa.

Ili mradi tu una jina hapa Bongo, tambua mashabiki watakufuatilia kokote unakokwenda, unachofanya, uhusiano wako, umekuwa, hujala, una bifu na nani, una patana sana na nani na mengine mengi.

Kwa Wema si jambo la kuuliza, tangu amekuwa maarufu na kuitwa Tanzania Sweethart, hajashuka na kila tukio anafuatiliwa.

Moja na tukio lililowashangaza wengi na kujiuliza maswali ni kwa Wema kutokuonekana kwenye sherehe ya Baby Shower ya Paula mtoto wa msanii wa Bongo Movie, Kajala Masanja.

Macho yote Jumatano ya Aprili 17 yaliangazia Wema ameketi wapi. Hata hivyo hakuonekana na ndio hapo maswali yakaanza kuibuka kwa wadau.

Katika sherehe hiyo iliyofanyika Wherehouse, Masaki, jijini Dar es Salaam baada tu ya hafla hiyo kilichoendelea mitandaoni ni ‘Wema na Kajala wana bifu’.


Kikubwa ni Wema kutokushiriki katika tukio hilo muhimu kwa Kajala (bibi mtarajiwa) licha ya wawili hao kutoka mbali na mambo mengi wamekuwa wakisaidiana ikiwamo Wema kumtoa Kajala mahabusu miaka ya nyuma.

Baada ya sintofahamu hiyo, Mwanaspoti lilimsaka Wema ili kujua kiundani stori hiyo na kufunguka mengi na zaidi ni majukumu ndio sababu ya kutokuhudhuria sherehe hiyo na hana ugomvi na Kajala.

“Unajua watu ni wa ajabu sana, sasa mimi kutoonekana kwenye hiyo ‘Baby Shower’ ndio tuna ugomvi na Kajala? Tumeshakuwa watu wazima, tuna akili na kujielewa. Habari za kugombana na mtu ndio usiende kwenye msiba au sherehe ya mwenzio, sijaona haya mambo muda mrefu sana na kwanza hata kama ndio nina ugomvi na Kajala vipi Marioo je nina ugomvi naye au Paula? Watu waache kukuza mambo mimi nilibanwa na majukumu yangu ya Familia,† anasema Wema.

Kuonyesha hana bifu na rafiki yake huyo waliyetoka mbali, Wema anasema licha ya mara nyingi wawili hao kugombana lakini walipatana na kwa sasa wanaelewana vizuri na alipanga kuhudhuria sherehe hiyo.

“Mimi na Kajala tumeshagombana sana na kupatana  zaidi ya mara tatu kipindi tupo karibu sana, yaani tulikuwa marafiki sana na mwishowe tuliamua kuacha utoto huo na kuendelea kuelewana hadi sasa, japo maelewano yetu sio kama yale ya zamani lakimi tunaongea.”

TUJIKUMBUSHE

Kajala na aliyewahi kuwa mumewe, Faraja Chambo waliwahi kukabiliwa na makosa matatu ambayo ni pamoja na kula njama na wote kwa pamoja walitenda kosa kwa kuhamisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi Salasala, jijini Dar es Salaam.

Shtaka la pili Aprili 14 mwaka 2010 walihamisha isivyo halali umiliki wa nyumba hiyo kinyume na kifungu cha 34 (2)A(3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007. Shtaka la tatu ni la kutakatisha fedha na walilitenda Aprili 14 mwaka 2010, huku wakijua ni kinyume cha sheria

Hukumu ikasomwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam na katika hukumu hiyo Kajala akahukumiwa kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya Sh13 milioni na mumewe kwenda jela miaka saba au kulipa faini ya Sh200 milioni.

Sasa kwa urafiki wa Wema na Kajala kwa kipindi hicho, Wema alizitoa fedha hizo zote milioni 13 na kumlipia faini hiyo Kajala na akawa huru.


KWA UFUPI BABY SHOWER

April 17, 2024 Warehouse, Masaki jijini Dar es Salaam kulifanyika Sherehe ya Baby Shower ya Paula.

Paula na mpenzi wake, Marioo walisherehekea ujio wa mtoto wao, tukio lililoandaliwa kwa ustadi mkubwa na kuhudhuriwa na wageni wengi wa aina mbalimbali wakiwamo wasanii wa Bongo Flava.

Sherehe hiyo ilipambwa na shamrashamra mbalimbali, huku MC Garab aliwafahamisha wageni waliohudhuria kuhusu jinsia ya mtoto mtarajiwa, akibainisha Paula atajifungua mtoto wa kike hivi karibuni.

Mbali na hayo sherehe ya Baby Shower ya Paula ilihudhuriwa na baba yake mzazi, P Fanky Majani.

Hilo liliwashangaza wengi hasa wakikumbuka mtayarishaji muziki huyo maarufu aliwahi kunukuliwa akisema hafurahishwi na tabia, malezi ya mzazi mwenzake Kajala kwa mtoto wao Paula.