VIBE LA WIKI : Ruge hakuwa adui, aliwaonyesha njia sahihi

Wednesday March 6 2019

 

By Joseph Damas

RUGE Mutahaba ndio ameondoka zake na kuachana na changamoto za duniani. Ameifanya kazi yake kwa weledi mkubwa na kila mtu ameikubali, japo kuna wengine wana sababu zao binafsi tu. Si unajua tena Wabongo huwa hatuishiwi maneno kabisa.

Unachotakiwa kukifanya wewe ni kutupa picha tu, maneno tutaandika wenyewe kwa sababu tunayo mengi sana. Ilikuwa huzuni na simanzi kubwa baada ya taarifa za kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, aliyefariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu kule Afrika Kusini.

Zilikuwa taarifa mbaya na zenye kushtua sana, lakini ghafla tu zikageuka kuwa sherehe katikati ya vilio na Watanzania kuanza kusherehekea ‘Maisha ya Ruge’. Ndio, ilikuwa sherehe za maisha yake na watu wakasahau kuwa ni msiba, vilio vilikuwepo kila kona na wengi walijitokeza barabarani kumlaki wakati akipitishwa kwenye mitaa mbalimbali.

Wakubwa kwa wadogo walikuwa wakimlilia Ruge na hili lilitosha kukufahamisha kwamba, jamaa alikuwa mtu wa aina gani.

Hakuwa bosi serikalini na hakuwa mtu wa kupenda kiki kwenye vyombo vya habari, lakini utu na moyo wake wa kupambana kwa ajili ya watu waliomzunguka ndio vimeufanya msiba wake kuwa sherehe. Ilianza hivi. Taarifa za kifo chake zilivuruga kinoma huko kwenye mitandao ya kijamii, kila mtu alifungua ukurasa wake wa Twitter, Instagram, Facebook na huko kwenye makundi ya WhatsApp ndio ilikuwa balaa zaidi. Baadhi wakaona ni jambo la kawaida kwa sababu kuposti tu, kila mtu anaweza kwa sababu ana simu ya mkononi. Shughuli yenyewe ikaanza siku mwili wake ulipowasili nchini kutoka Afrika Kusini, umati ukatanda wakati wa mapokezi pale Uwanja wa Ndege Dar es Salaam. Kuanzia hapo huku mitaani, mamia ya watu walikuwa wametanda pembezoni mwa barabara kumlaki Ruge Mutahaba.

Watu walibeba mabango kuelezea hisia zao kwa Ruge, wengine walinyanyua maua na majani juu kama ishara ya kumuaga. Hapo watu wakaanza kujiuliza kwanini Ruge. Hivi huyu Ruge ni nani katika nchi hii.

Hakuna aliyepata jibu la haraka wala kufahamu sababu za watu kuacha shughuli zao na kupigwa jua barabarani ili tu kupata fursa ya kuliona tu gari na msafara unaosindikiza mwili wa Ruge. Pale Karimjee pakafurika, vigogo wa juu wa serikali wakiongozwa na Rais John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya walikuwa pale na wasanii wote unaowajua wewe hadi nanii na nanii, walikuwa pale.

Kwenye mitandao vilio vya maandishi vikaongezeka na kila anayeandika unakutana na neno ‘Baba umeondoka, Bosi umetuacha. Kaka bila wewe sijui ningekuwa wapi. Hashi tag ya Jasiri Muongoza Njia ikashika hatamu na kuwasahaulisha watu kila kitu.

Hata ile habari ya Waziri Mkuu Mstaafu na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, kurejea CCM tena wakati huu na Mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe yuko lupango, ikawa sio stori ya kushtusha kabisa na tayari imesahaulika.

Yote hiyo ni sababu ya huyu Ruge Mutahaba. Sasa wakati watu wanajiuliza Ruge ni nani hadi msiba wake ukaisimamisha Tanzania, jibu ni moja tu alikuwa mtu wa watu aliyeishi ndani ya mioyo ya watu sio mdomoni mwa watu. Ndio, kuna watu wa watu wanaoishi kwenye mdomo tu na wengine wanaishi kwenye mioyo ya watu, Ruge alikuwa ndani ya mioyo yao. Kwa kilichotokea katika msiba wake, kama utajitokeza hadharani na kumsema Ruge alikuwa mtu mbaya ama alikufanyia jambo baya, jamii itakushangaa sana kwani, kila mtu anamkumbuka Ruge kwa kufanyiwa mazuri, kubadilishwa kimaisha, kifikra, kiakili na kujenga mawazo chanya na wengine wanakiri wamefanikiwa kimaisha kwa sababu ya Ruge.

Tatizo la baadhi ni uelewa mdogo tu kwani, wachache waliodai Ruge aliwabania, wanayasema hayo baada ya kuwa wamefanikiwa kwa namna moja ama nyingine baada ya kutolewa shimoni na kuleta juu na Ruge.

Wakasikika, wakapendwa huko mitaani kisha wakapata kiburi na kudhani jamaa sio lolote na walipoachwa wakapambane wenyewe na walipokutana na changamoto wakadhani tatizo ni Ruge.

Wakati mko chini ya Ruge hizo changamoto ziliishia kwake, sasa mnataka kusimama wenyewe pambaneni nazo tu. Yaani ni sawa na kukataa ugali na maharage kisha baba yako akakwambia kua uyaone. R.I.P RUGE.

Advertisement