VIBE LA WIKI : Kha! Hakuna mdhamini halafu faini kiboko

Wednesday March 13 2019Joseph Damas

Joseph Damas 

By Joseph Damas

LIGI Kuu Bara ni miongoni mwa ligi maarufu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa sasa. Ndio! Mbona hili halina ubishi kabisa kwani ni ligi inayovutia wachezaji wengi wa kulipwa kutoka kila kona ya Afrika, viwanja vinajaa mashabiki kutazama na kuzipa mzuka mwingi klabu zao. Si unajua kwanini, Watanzania ni wendawazimu wa soka kama ilivyo kwa watawala wetu, Waingereza.

Waingereza huwaelezi kitu kabisa linapokuja suala la mpira na wako tayari kwa lolote ili kuhakikisha wanatimiza kiu na malengo yao katika soka.

Huwezi kukuta viwanja vya Kenya ama Uganda vikiwa vimefurika mashabiki kwa ajili ya kushangilia timu zao tena wakiwa wamelipia viingilio ambavyo vinatosha kabisa kuwawezesha kukidhi mahitaji ya mlo wa siku inayofuata. Lakini, aaah wapi mbele ya mpira Wabongo tuko tayari hata kukopa kwenda kuangalia machama yetu ya Simba, Yanga, Azam, Mbeya City na mengine kibao yanayoshiriki Ligi Kuu.

Hata hivyo, kwa taarifa yako ni kuwa pamoja na mzuka wa mashabiki, lakini unafahamu kuwa soka la Bongo limo kwenye orodha ya yanayoongozwa kienyeji, mihemko na kukomoana?

Sawa, kuna sheria, kanuni na taratibu, lakini kuna wakati zimekuwa zikivunjwa ili kuishikisha adabu timu, mchezaji ama kiongozi fulani kwa maslahi ambayo hata mwenyewe siyajui! Acha kushangaaa kwani, huna rekodi hapo ama hujawahi kusikia fungia fungia tena ya maisha ya viongozi kibao kwenye soka. Ndio hivyo ukijifanya mjanja mjanja tunakula shingo tu.

Kama huamini na hujasikia basi nenda kamuulize nanii!

Advertisement

Sasa iko hivi. Kwa sasa Yanga na Simba zinaparurana kinoma kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini mpaka sasa haijawekwa bayana bingwa atakayenyanyua kwapa mwishoni mwa msimu atapata zawadi yake ama ndio itakuwa Asanteni kwa Kushiriki. Kwa sababu mpaka sasa hakuna mdhamini mkuu wa ligi, ambaye ndiye hubeba jukumu la kutoa zawadi na hata vifaa vya michezo kwa timu shiriki. Jamani eeh hakuna mdhamini zaidi ya Azam Tv ambaye kajikita zaidi kwenye kupeperusha mechi laivu.

Hata hivyo, timu shiriki zimeendelea kuonyesha ukomaavu wa kupambana huku zingine zikiwa na njaa kali kiasi cha kushindwa kulipa mishahara wachezaji na makocha. Wenye jukumu la kusimamia mpira wetu wapo tu na wamepiga bunda kama hawaoni wala kusikia. Watu bana.

Sasa pamoja na changamoto hizo bado Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo hutegemea kupata mkate wake wa kila siku kupitia soka, limeibuka na mbinu mpya za kukusanya mapato ili kupoza ukali wa maisha. Sasa unataka nitumie neno gani rahisi kama kupoza makali ya maisha kwani, hujui kuwa kwa sasa rhumba kali na mjini wamebaki wanaume tu wenye kazi zao wale misheni town kwa sasa wamesogea zao Mvomero, Nangurukuru, Rufiji wanatafuta mashamba ya kulima.

TFF kupitia bosi wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura imetangaza rungu la maana kwelikweli kwa kuwafungia wachezaji mechi kadhaa kwa utovu wa nidhamu, lakini ikashusha rungu la faini za maana kwa wachezaji, makocha, viongozi na timu kwa kukiuka kanuni na miiko ya soka.

Kwani nani kasema anapinga? Ni sawa mtu anapokosea anastahili kuadhibiwa na anapofanya vizuri basi apongezwe. Lakini, hii ya TFF imekaa vibaya aisee, adhabu za sasa ni kama wamepania anaambiwa. Kwanza walipiga kimya wakakusanya matukio kisha wakayaamua kwa pamoja na kutoa adhabu kali. Mbona matukio mengine ni ya muda mrefu na yalitakiwa yawe yameemuliwa na kutolewa ufafanuzi wakati yakiwa bado yamoto. Kulikuwa na ulazima gani wa kupiga kimya ama wajumbe wa kamati walikuwa likizo?

Kinachoshangaza zaidi ni kwamba, TFF inafahamu kabisa maisha ya klabu nyingi ni ya kuungauunga kama ilivyo kwa Yanga ambayo licha ya kupambana na hali yake bado imekuwa ikionyesha kukimbizana na wapinzani wao, Simba kwenye mbio za ubingwa.

Yanga ambayo njaa ni kali peke yake imetozwa faini ya Sh 6 milioni kwa utovu wa nidhamu, lakini ni kweli kila kosa lazima liwe na adhabu ya faini. Hakuna onyo wala wahusika kuitwa na kuonywa hadharani? Hapa TFF mmegeuka kuwa TRA bana. Vipi hao akina Alliance, Stand United, Coastal ambao maisha yao Mungu ndio anajua. Watalipa kwa vyanzo vipi cha mapato kwani, kuna baadhi ya timu zinapocheza zinaweza kuambulia 300,000 kutokana na viingilio sasa watalipa lini ama ndio mtawadai?

Pia, nikasikia eti aliyekuwa Kocha wa Azam Fc, Hans Pluijm naye ana msala na amepelekwa kwenye kamati ya naniii....nikacheka mbona huyu jamaa kasepeshwa pale Azam na hayupo tena nchini kwa sasa yuko zake Ghana anakula kuku!

Yaani hapa nilipo nawaza mwenyewe tu kama kuna klabu itaomba kuwa itakuwa tayari kulipa faini hizo mwishoni mwa msimu kupitia zawadi za washiriki ama ubingwa ndio hapo tutaona majanga. Nawaza tu si unajua Mzee wa Vibe kwa kuwaza yasiyowezekana.

Advertisement