Tumsifu Kakolanya au tumsifu Mganga wao?

Muktasari:

  • Ubishi wa mechi ya Simba na Yanga ulimalizika bada ya timu hizo kukamilisha dakika 90 zikitoka suluhu. Ubishi haukuishia uwanjani ulikwenda mbali hadi njia ya uwanja. Mashabiki wa Simba walimuona kipa wa Yanga Benno Kakolanya kama ndiye aliyewakatili kuziona nyavu za wapinzani wao. Hii ni kutokana na kipa huyo kuokoa hatari nyingi langoni kwake.

MARA ya kwanza nilipomuona Mbwana Samatta nilijua atafika mbali. Kwa muda mrefu sikuwahi kumuona mshambuliaji asiye na hofu kama yeye. Sio hofu ya kugombana. Hapana. Hofu akiwa na mpira. Alijua aupeleke wapi.

Mbwana akiingia katika boksi anajua afanye nini. Anatulia. Anajua anaupeleka wapi mpira. Hapelekeshwi na kelele za mashabiki. Anapelekeshwa na anachokiamini. Na ndio maana mpaka sasa kuna Mbwana Samatta mmoja tu.

Na baada ya suluhu ya Simba na Yanga juzi nikamkumbuka Samatta. Kama angekuwa mshambuliaji wa Simba angeondoka uwanjani bila ya bao? Sina uhakika. Siamini katika uchawi na sitaamini katika uchawi. Naamini katika utulivu wa washambuliaji wetu.

Juzi kulikuwa na mawazo tofauti baada ya suluhu ya Simba na Yanga. Mashabiki wa Simba hadi mabosi wao wanaamini kwamba Yanga waliroga sana. Hapo hapo Yanga wakaondoka uwanjani wakimsifu kipa wao, Beno Kakolanya. Tuamini lipi?

Ni suala la kisaikolojia zaidi. Katika mechi za watani wa jadi, baada ya bao la kwanza la wazi kukoswa, kisha likakoswa la pili, baadhi ya wachezaji uwanjani huanza kuvunjika moyo kwamba huenda sio siku yao.

Baadaye hisia hizo zinakwenda kwa mashabiki. Huku majukwaani mashabiki wanaamini zaidi katika uchawi. Hawaamini katika utulivu wa washambuliaji wala ubora wa makipa. Hili ndilo tatizo la msingi la soka la Tanzania.

Washambuliaji wetu wakifika katika boksi la adui wanakuwa na papara katika vile mpira una moto au miili ya mabeki ina moto. Ukichunguza mabao mengi ambayo Simba wamekosa juzi huwa yanakoswa kila siku katika mechi mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Katika mechi ya juzi, vichwa vya mashabiki wa Simba, wachezaji na viongozi vilianza kuharibika wakati Ibrahim Ajib alipoanzisha mpira kwa kuupiga nje kwa makusudi kabisa. Hapo hapo vichwa vikavurugika bila ya sababu za msingi.

Kama uchawi ungekuwa unafanya kazi naamini leo hii tungekuwa mbali zaidi. Lakini, kama mganga wa Yanga ni huyu huyu siku zote sijui kwanini siku nyingine huwa wanaruhusu mabao. Kwa ninavyofahamu hata kama klabu zetu hazina pesa, lakini waganga huwa hawahitaji pesa nyingi. Kwanini siku nyingine hazuii mabao?

Siamini kama Yanga walikuwa wanataka kutolewa kirahisi katika michuano mikubwa ya kimataifa. Walifungwa ovyo ovyo na Gor Mahia hivi karibuni. Mganga alikuwa wapi? Alidhulumiwa pesa yake? Tusiaminishe vizazi vijavyo kuhusu masuala ya kishirikina katika soka.

Tumgeukie huyu Kakolanya. Kwa muda mrefu nilikuwa najiuliza kwanini hakai katika lango la Yanga. Ni kipa maridadi na aliwahi kuchaguliwa kuwa kipa bora wa msimu wakati akiwa na timu yake ya zamani Tanzania Prisons. Inashangaza nini kufanya uokoaji alioufanya na kugeuka kuwa mchezaji bora wa mechi? Inashangaza sana.

Atakaporudi nyumbani mwenyewe atakuwa amechanganyikiwa sana. Labda anafahamu ubora wake langoni na mazoezi anayofanya kila siku. Atakapoambiwa kuwa mganga ndiye aliyeiokoa timu nadhani atashangaa sana.

Mwisho wa siku naamini kwamba, mechi ijayo ya Simba na Yanga kuna uwezekano mkubwa watu wanaoitwa Waganga wa Simba wakachukua pesa nyingi sana.

Shukrani kubwa iende kwa Simba wenyewe. Walibakia hapa hapa jijini kuelekea katika mechi yao ya juzi. Hawakwenda Pemba wala Bagamoyo. Na bado walitawala mechi kwa kiasi kikubwa.

Hii inaonyesha kwamba ukiwa na timu nzuri hauhitaji baadhi ya imani ambazo tumejiwekea. Simba wana timu nzuri kuanzia nyuma mpaka mbele. Ilionekana juzi kwa jinsi walivyotawala mechi kwa muda wote. Kwenda Pemba ni kusumbua wachezaji tu na kuwapa hofu ambayo haipo.

Wakati mwingine hata Waganga wanamaliza pesa za wachezaji tu. Pesa chafu ambazo anapelekewa mwamuzi au wachezaji wa timu pinzani zinapaswa kutumika katika kuongeza morali kwa wachezaji tu.

Simba walichukua maamuzi ya busara na hawawezi kusema hawakushinda mechi kwa sababu hawakwenda Pemba wala Kigoma. Tuanze kuondoa imani za ajabu ajabu katika mpira. Hata hili la Simba kukosa mabao ya wazi katika mechi ya juzi linewafanya wachezaji waliokuwa wazembe wapone katika lawama kwa sababu ya imani ya kishirikina iliyojengeka.

Yanga kushangilia sare? Inaonyesha pengo kubwa lililopo baina yao na Simba. Na inaonekana wamelikubali. Umaskini fulani unaowakabili kwa sasa. Walilikubali pengo hili wakati wa usajili na sasa inaonekana wamelikubali pengo hili wakati Ligi inaendelea.

Ni kama vile wanaamini kimoyomoyo kwamba, sare ni ushindi kwao. Maisha haya hayatabadilika mpaka nao watakapoamua kwa dhati kabisa kwamba, wanahitaji mapinduzi katika mfumo wa uendeshaji wa timu yao. Wawe na akaunti za benki ambazo pesa zake zinaendana na ukubwa wao. Sijui kama bado wanamsubiri tajiri wao. Sijui.