TIMUA VUMBI : Wazo la Zahera zuri, ila awaachie mabosi wake

Thursday January 31 2019

 

By Mwanahiba Richard

KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera ametangaza kuanzisha kampeni ya kuichangia timu hiyo kwa wanachama ama mashabiki wenye mapenzi ya dhati ya kuona Yanga inapata mafanikio makubwa kwenye ligi.

Kampeni ya Zahera si ya kwanza ndani ya Yanga, kwani aliyekuwa Katibu Mkuu Boniface Mkwasa aliifanya na kuuendelezwa na Kaimu Katibu wao, Omary Kaya na sasa haijulikani imefia wapi.

Wanachama na mashabiki wa Yanga hawakuwekewa kiwango cha kuichangia timu yao bali ni kiasi chochote kile ambacho mtu anaguswa, fedha hizo zilielezwa kusaidia kuiendesha timu yao ambayo kiuchumi imeyumba.

Mpango wa Zahera si mbaya ila inaonyesha kubeba mzigo mkubwa kwa maana ya majukumu kuwa mengi zaidi ya yale yaliyokusudiwa kwake ambayo ni kuifundisha timu pekee pamoja na kusajili yaani kupambana na mambo ya timu tu.

Zahera huenda ameona mambo ndani ya Yanga yanakwama kukamilika kutokana na ukata unaowakabili ambapo umepelekea hata kushindwa kulipa mishahara ya wachezaji kwa wakati jambo linalopelekea baadhi ya wachezaji kushuka morali ya kujituma huku wengine wakiigomea timu.

Wengi huenda wanashangazwa na uamuzi wa kocha huyo na kuona kwamba ni jambo ambalo haliwezekani hasa kwa kocha tena wa kigeni kujitoa kwa kila hali ndani ya klabu yake.

Baadhi ya mashabiki na wanachama wa Yanga, wanajiuliza juu ya majukumu hayo mapya ya kocha wao na kwenda mbali kwamba amevuka mipaka ila inawezekana mpaka ameamua kuweka hadharani amepewa ruhusu na uongozi wa klabu hiyo.

Uchangishaji pesa ndani ya Yanga ama taasisi yoyote ni jambo kubwa ambalo linahitaji makubaliano na uongozi wote hivyo si rahisi kwa mtu mmoja tena mtaalamu wa benchi la ufundi aamke na kutangaza hadharani jambo kubwa kama hilo.

Lakini jambo hilo nadhani viongozi wa Yanga wao wangelibeba maana ni kubwa na zito ukizingatia Zahera ana kazi ngumu ndani ya timu hasa kuhakikisha wanabeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Jukumu hilo ni kubwa sana kwani ikitokea ameshindwa kupelekea ubingwa Jangwani wapo watakaomwelewa na wengine hawawezi kumwelewa kwa kile kitakachoelezwa kwamba alijipa majukumu mengi na kusahau jukumu lake lililompeleka hapo.

Nadhani Zahera na wazo lake zuri angebaki tu kwenye nafasi yake, angeo wazo kwa viongozi na kupendekeza watu sahihi anaowaamini yeye kusimamia fedha zitakazopatikana ili yeye aendelee na jukumu moja ndani ya Yanga ambapo fedha ambayo ikipatikana basi apatiwe na kuifanyia kazi aliyokusudia ndani ya timu yake.

Mabosi wa Yanga mliopo sasa hebu msaidieni Zahera kupambania mafanikio ya Yanga ili pesa ipatikane atimize ndoto yake, maana baadaye asijelaumiwa iwe kwa kumruhusu kumwongezea majukumu ya kutafuta pesa za timu ingawa pengine Zahera ameamua kusimamia mwenyewe kuogopa wapigaji. Hilo Sh1 milioni moja ambayo tayari ameiweka kwenye akaunti kama kianzio cha michango hiyo kusaidia timu na mambo ya usajili msimu ujao basi viongozi anzieni hapo kusaidia jukumu hilo.

Advertisement