TIMUA VUMBI : Simba sasa wanaanza kurudi, Yanga wanajipanga

Thursday May 23 2019

 

By Mwanahiba Richard

SIMBA ilikaa miaka mitano bila kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, walikuwa katika wakati mgumu kweli kweli, walitamani kupanda ndege japo washiriki shindano hata moja la kimataifa ila haikuwa rahisi kwao.

Simba kwa kipindi chote hicho walikuwa wanasikilizia tu huku wakiwaona watani zao Yanga wakielekea Kipawa njiapanda ya Ulaya wakikwea Pipa kwenda kushiriki michuano ya kimataifa, hata waliporejea walisikia habari zao. Kiukweli walitamani hasa.

Katika kipindi chote hicho cha mateso ya kutamani kushiriki michuano ya kimataifa, pia walikuwa wanatamani japo watwae ubingwa wa ligi japo walishike kombe hilo kubwa hapa nchini, lakini yote hayo hayakuwezekana kwa wakati huo. Walivumilia.

Viongozi walipambana kweli kweli hadi ilifikia hatua kila usajili walikuwa wanafumua kikosi chao wakiamini kikosi kipya kitatwaa ubingwa lakini kumbe walikuwa wanaharibu zaidi, walitimua makocha wakidhani huenda wao ndiyo chanzo lakini haikuwasaidia na wakati huo mambo ya uchumi kwao hayakuwa mazuri kama ilivyo kwa watani zao sasa.

Kwa hakika Yanga ilitawala katika ufalme wa soka la Bongo wakati huo wapo chini ya Mwenyekiti wao, Yusuf Manji, walisajili mchezaji yoyote waliyemhitaji na hata mishahara yao haikuwa ya kubabaisha. Kwa sasa Manji hayupo na tangu aondoke ndiyo shida walizokuwa nazo Simba zikahamia kwao.

Simba uwezo wao ulikuwa mdogo, walilipa mishahara wachezaji wao kulingana na kile walichonacho, hivyo hata kama wakati huo wakikwama kulipa mishahara wachezaji wao lakini walikuwa na uwezo wa kutafuta pesa wenyewe na kulipa pasipo kumtegemea mtu mmoja.

Advertisement

Simba waliamua kwenda kwenye mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu kutoka klabu ya wanachama hadi kampuni na wanachama wao sasa watapaswa kuwa na hisa, mfumo ambao waliamini utawavusha kutoka kule walikokuwa na kufikia hatua ya kimataifa ambayo sasa wamefikia.

Simba walianza kufanya usajili wa maana chini ya Mwekezaji wao ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’, ingawa kabla ya hapo walianza kujifunza kuishi na wachezaji kwa muda mrefu na kupunguza zile sajili za kikosi kizima wakati wa dirisha dogo na ligi ikiisha kufumua upya, sasa hawafanyi hivyo, wachezaji wao wamekaa pamoja angalau kwa zaidi ya miaka miwili.

Sasa hivi Simba imekata tiketi tena kushiriki michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo msimu huu imeishia hatua ya robo fainali ingawa lengo lao ambalo wanaamini walikuwa wanajijenga walitaka kuishia hatua ya makundi.

Nia yao ilitimia na walivuka malengo, ni jambo kubwa sana kwa Simba ambapo hivi sasa huenda lengo likavuka zaidi kutoka robo fainali hadi nusu fainali ya ligi hiyo, hata kuwashangaza wadau wa soka kufika hatua ya fainali kabisa.

Yote hayo yatatokana na usajili bora utakaofanywa na Simba, uwekezaji wao bila kujali watapata nini huko mbele kwani kwenye biashara yoyote hupaswi kuangalia faida tu bali hata hasara inakubalika kwani soka sasa ni miongoni mwa biashara kubwa.

Katika hili Simba watahitaji kutumia pesa nyingi sana kufikia malengo yao tofauti na pesa iliyotumika msimu huu, ni kujipanga tena kujipanga kweli kweli bila kujali wala kuumia wanapotoa pesa zao mfuko.

Huenda wakati watani wao Yanga wanaendelea kukisuka kikosi chao pengine Simba nao watakuwa wamechukua ubingwa wa ligi mara tatu mfululizo kama walivyofanya Yanga.

Kuyumba kwa Yanga si kwamba ndiyo mwisho wao, hapana, huko mbele kama watasajili vizuri na kuwa na kikosi kipana basi ushindani wa kuwania ubingw autakuwa mkubwa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kabla Simba haijapotea na baada ya Simba kurudi kwenye mstari.

Hongera Simba kwa kutetea ubingwa wa TPL na kuonyesha kwamba mmeanza kurudisha taratibu mataji waliyobeba Yanga wakati wao wanaendelea kujipanga.

Advertisement