Simba na Yanga ziko mawindoni

Friday March 1 2019

 

By CHARLES ABEL, THOBIAS SEBASTIAN

SIMBA na Yanga ziko kwenye vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu lakini hapana shaka wakati zinapigia hesabu taji hilo, mabenchi yao ya ufundi yanatazama nyota ambao watawanasa ili wazitumikie timu hizo msimu ujao.

Kutokana na ufanisi wa vikosi vyao msimu huu, ni wazi kuna baadhi ya maeneo ambayo klabu hizo zitayaimarisha kwa kuwaongeza nyota kadhaa wa kigeni na wale wazawa ambao wanamudu kucheza kwenye nafasi husika.

Ingawa usajili wa nyota wa kigeni ndio unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu hizo, lakini wapo wachezaji wachache wa ndani ambao huenda klabu hizo zikawasajili ili kuziba mapengo ya wale ambao wataonyeshwa mlango wa kutokea kwenye timu hizo.

Tathmini iliyofanywa na gazeti hili katika Ligi Kuu Tanzania Bara, imebaini nyota watano kutoka klabu tofauti nchini wanaweza kuziingiza vitani Simba na Yanga katika dirisha kubwa la usajili baada ya msimu kumalizika. Kikubwa ni kutokana na viwango bora ambavyo wamekuwa wakivionyesha pamoja na udhaifu ambao timu hizo kongwe zinao kwenye nafasi wanazocheza.

Nyota wa kwanza ambaye huenda akageuka kuwa lulu kwa timu hizo kwenye dirisha la usajili ni kipa, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons ya Mbeya ambaye kwa misimu takribani mitatu mfululizo amekuwa akionyesha kiwango bora ambacho kinaweza kuzitoa udenda timu mbalimbali.

Kipa huyo msimu uliopita alikuwa ni miongoni mwa wanaowania Tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu kutokana na uwezo wake wa kuokoa mipira ya kona na krosi, mashambulizi ya ana kwa ana na kuipanga timu. Kipa huyo ameruhusu mabao 21 kwenye nyavu zake msimu huu.

Kalambo amekuwa akionyesha kiwango bora na amekuwa akiangushwa na udhaifu wa safu yake ya ulinzi.

Ni wazi Simba na Yanga zitaingia sokoni kumsaka kipa wa kuongeza nguvu kwenye idara hiyo kuweza kuwapa changamoto, Aishi Manula kwa upande wa Simba na Ramadhani Kabwili na Klausi Kindoki kwa upande wa Yanga.

Pia, timu hiyo ya Jangwani itahitaji kuziba pengo la kipa wake Beno Kakolanya ambaye huenda ikaachana naye.

Pia, mawinga, Vitalis Mayanga wa Ndanda FC, Rafael Siame wa Mbao FC na Dickson Ambundo wa Alliance FC, viwango vyao bora wanavyoonyesha kwenye Ligi Kuu ni wazi vitaziingiza timu hizo vitani.

Simba kwa sasa inasaka winga wa kuziba nafasi ya Shiza Kichuya aliyeuzwa Misri, Marcel Kaheza iliyemtoa kwa mkopo AFC Leopard huku pia ikitajwa kuwa kwenye mpango wa kutomuongeza mkataba Haruna Niyonzima wakati Yanga ina mawinga wachache ambao ni Mrisho Ngassa na Deus Kaseke ambao pia wamekuwa hawana mwendelezo wenye ubora.

Katika kundi hilo la mawinga watatu, Ambundo ndiye anayeonekana ataweza kuzigharimu timu hizo kiasi kikubwa cha fedha iwapo zitaingia sokoni kumuwinda kwani ameonyesha ubora wa hali ya juu katika kutengeneza nafasi za mabao, pamoja na kufumania nyavu licha ya kucheza pembeni.

Na kwa kulidhihirisha hilo, hadi sasa ameshapachika mabao tisa kwenye Ligi Kuu. Lakini iwapo Alliance itamwekea ngumu Ambundo, mshambuliaji kiraka Vitalis Mayanga anaweza kuingia kwenye hesabu kutokana na kasi, uwezo wa kufumania nyavu na kumiliki mpira akiwa pia na uwezo wa kucheza nafasi tofauti uwanjani,

Winga mwingine ambaye hapewi nafasi kubwa mbele ya Mayanga na Ambundo ni Siame wa Mbao ambaye anasifika kwa kupiga krosi na kutengeneza nafasi za mabao pamoja na kupiga chenga.

Ingawa mshambuliaji wa Mwadui FC, Salim Aiyee hadi sasa anaongoza kuzifumania nyavu akiwa amefanya hivyo mara 13, jina la mshambuliaji wa Coastal Union Ayoub Lyanga ndilo linaonekana linaloweza kupewa nafasi kubwa na timu hizo iwapo zitaamua kusaka mshambuliaji mzawa badala ya nyota huyo wa Mwadui.

Lyanga mwenye mabao tisa, ameonyesha uwezo wa hali ya juu katika kumiliki mpira, kukaa kwenye nafasi sahihi, kupiga pasi za mwisho, kufumania nyavu na kupambana na mabeki. Nyota huyo amekuwa akifunga mabao ya vichwa na miguu yote miwili nje na ndani ya eneo la hatari.

Advertisement